Friday, March 13, 2015

TUFANYE NINI MWAKA HUU KUWA NA UCHAGUZI HURU NA WA HAKI?

Padre Baptiste Mapunda. 
Na Padre Baptiste Mapunda,

HOFU ya kukataliwa kwa katiba  mpya kumeifanya serikali ya awamu ya nne ivunje kabisa makubaliana na TCD, kwamba kura ya maoni ingesitishwa hadi  baada ya uchaguzi 2016.

Hadi sasa hatujui nani atakuwa madarakani ni mpinzani au  mwanaCCM mwenzao, hivi wanaona afadhali waendelee kulazimisha  kura ya maoni kwa mtindo ule ule wa kulazimisha. Watanzania tunaelekea pabaya  hii ni alama ya chama hiki tawala kukata tamaa na kuanguka.

Matokeo yake inafanya kila hila, ili daftari la kudumu la wapiga kura lisiboreshwe na waweze kuchota kura kirahisi,  na ushahidi ukosekane.


Swali langu hapa ni kwamba, mbona Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi alisema wafadhili walishatoa pesa ya kuboresha daftari la wapiga kura? Pia alisema hakuna uchaguzi utaendeshwa kuanzia sasa, bila kuboresha daftari hilo?

Najiuliza nini kimetokea hapo katikati? na hofu yao nyingine ni katiba hii pendekezwa kuja kukataliwa na umma, hivi Rais na serikali yake ya CCM wameona heri waendelee kuisukuma ili ikubalike na umma wa Tanzania kwa kutumia haya mabavu.

 Lakini ukweli ni kwamba, katiba hii imekataliwa na wananchi wengi  na ina maana imekataliwa pia na Mungu, kwa sababu “sauti ya wengi ni sauti ya Mungu.” Ukiisoma katiba pendekezwa binafsi nasema utagundua kuwa ni ya kulinda maslahi ya watu wachache, ndani ya chama na serikali hii ya CCM.

Kuvuruga uchaguzi kwa kutumia katiba mbaya na kanuni mbaya, ndiyo mwanzo wa kuleta  machafuko, vita na mauaji kama yale yaliyotokea nchini Kenya  katika uchaguzi wa mwaka 2007.

Kibaki alilazimisha ushindi na akaapishwa usiku usiku, mbele ya watu wachache tu. Ukisoma alama za nyakati unagundua kwamba hayo ndiyo yanayokuja mbele yetu je tukae kimya?

Natambua ili kuielimisha jamii tunaandika bila hofu, ili wananchi mjue  kwamba serikali yetu sasa imepuuzia kufanya maandalizi mazuri, ili kuhakikisha uchaguzi huru na wenye haki.

Uchaguzi wa haki na huru ndiyo ukomavu wa demokrasia unaoweza kuepusha machafuko, vurugu, malalamiko na mauaji hapa nchini kupitia siasa chafu zenye fitina, majungu na ukandamizaji.

Sasa kwa watanzania ili kuepusha katiba pendekezwa  ya chama hiki tawala, isilete maafa kuna mambo sita ya kufanya wananchi, vyama vya upinzani, madhehebu ya dini, wanaharakati, wasomi na wananchi wenye mapenzi mema.

Mosi ni kwamba wadau wa demokrasia, utawala bora na amani ambao ni wanasiasa, viongozi wa dini, wanaharakati na wananchi wadai kuboreshwa kwa daftari la kupigia kura, ili kuwapa watu wengi fursa ya kutumia haki ya kikatiba kupiga kura hasa vijana.

Kama kweli serikali ya CCM, ina amini juu ya demokrasia na inasema inakubalika basi, wasiwe na hofu kukataa kuboreshwa kwa daftari hilo.

Pili, wapinzani na wadau wa siasa  lazima wailazimishe  serikali hii kuunda tume huru ya uchaguzi, ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki kwa kila chama.

Jambo la tatu ni kwamba, sheria za uchaguzi ziboreshwe ili kujenga mazingira ya usawa katika ushindani kwa vyama vyote. Kila chama kifuate sheria na kanuni  bila kujali CCM ni chama tawala au la.

Mgombea binafsi aruhusiwe kama ilivyoamriwa na mahakama ya rufaa. Hii ni katika kupanua uwigo wa demokrasia ya kweli kama kweli tunajigamba kudumisha demokrasia na utawala  nchini Tanzania.

Jambo la nne na la msingi vyombo vya dola kwa maana ya Polisi, Jeshi la wananchi (WTZ), FFU na usalama wa taifa visiingilie mchakato wa uchaguzi, hata pale wanaponusa kwamba CCM inashindwa waiache kwani hii ndiyo demokrasia ya kweli.

Zisitumike nguvu kubwa, bila sababu ya maana na hilo litaepusha vurugu kwani mara nyingi wanaoanzisha fujo na vurugu, katika  vituo vya uchaguzi ni polisi na vyombo vingine vya dola kwa kisingizio cha kulinda amani.

Hoja ya tano, kila chama kisaini makubaliano kwamba, kutokana na mazingira hayo ya uwazi, basi atakayeshindwa akubaliane na matokeo. Hii ndiyo demokrasia ya kweli inayoambatana na utawala bora.

Jambo la sita wananchi wote wenye mapenzi mema na nchi yao wahamasishwe, kujiandikisha katika daftari la wapiga kura na siku ya uchaguzi wakafurike vituoni, kwenda kupiga kura kwa kuchagua viongozi bora na siyo bora viongozi, kwa sababu tu umepewa rushwa ya uchaguzi.

Kuhusu kura ya maoni ya katiba mpya, kuna ushauri mwingi unaoendelea kutolewa na wasomi, viongozi wa dini, wanaharakati, watu binafsi kwamba ni vyema kura hiyo ikahairishwa kwa maslahi mapana ya taifa lote.

Kuna wanaotoa hoja kwamba, kuna haraka gani katika kupata katiba mpya, kwani hata ikipitishwa haitaweza kutumika katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Mheshimiwa Rais Kikwete ameanzisha mchakato, basi ni hatua kubwa na ya kumpongeza ili Rais ajaye awe wa CCM au wa upinzani basi ataendeleza hilo.

Ukawa walisusia mchakato wa katiba mpya na hivi inasemekana wasingependa kushiriki, katika kuipigia kura katiba mpya kwani sio tunda la mawazo na maoni ya wananchi kupitia Tume ya Mzee Warioba, bali ni mapandikizi ya mawazo ya wanaccm walioteka Bunge nzima la katiba kule Dodoma.

Wananchi wengi wanafikiri kwamba, ikiwa mchakato mzima wa upatikanaji wa katiba pendekezwa umekiuka sheria ya mabadiliko ya katiba maana yake, katiba pendekezwa ni “feki” yaani haina uhalali wowote wa kisiasa, sababu mojawapo ikiwamo ukosefu wa maridhiano hivi kushindwa kukubalika na wananchi.

Ee Mungu wape hekima na busara viongozi wa serikali ya chama hiki tawala,  ili waupeleke mchakato huu katika njia ya amani  kwa manufaa ya  taifa nzima, na sio kundi la watu wachache.

Ee Mungu uwajalie Watanzania ujasiri wa kukataa kuburuzwa na serikali yao kwa sababu Siasa zinapita, lakini Tanzania haitapita kamwe. Tukumbuke kuwa uchaguzi wa mwaka huu ni kipimo cha ukomavu wa demokrasia na utawala bora katika nchi yetu ya Tanzania Je, mtihani huu tutafaulu au tutafeli?  Mungu utusaidie!


Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa barua pepe; frmapunda91@gmail.com

No comments: