Monday, March 2, 2015

MWILI WA KAPTENI KOMBA WAWASILI MJINI SONGEA, UMATI MKUBWA WA WANANCHI WASHIRIKI KUUAGA








Mwili wa marahemu Kapteni John Komba, ukishushwa uwanja wa Majimaji, Songea mjini mkoa wa Ruvuma kwa ajili ya kuagwa na umati mkubwa wa wananchi waliokuwa wamewasili uwanjani hapo.

Na Kassian Nyandindi,
Songea.

MJI wa Songea mkoani Ruvuma, leo wananchi wake simanzi na majonzi viliendelea kutawala baada ya mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi wilaya ya Nyasa mkoani humo, Kapteni John Komba kuwasili kwenye uwanja wa ndege mjini hapa.

Mwili huo baada ya kuwasili umati mkubwa wa waombolezaji wakiongozwa na Mkuu wa mkoa huo, Said Mwambungu kutoka wilaya zote za mkoa huo walikuwepo uwanjani hapo, wakati wa mapokezi.

Aidha baadhi ya viongozi mbalimbali wa chama na serikali kutoka nje ya Ruvuma, nao walikuwepo ambapo mwili baada ya kushushwa kutoka kwenye ndege, ulihifadhiwa kwenye gari ndogo ya Jeshi, na kuelekea uwanja wa Majimaji uliopo mjini Songea.


Baada ya kuwasili katika uwanja huo, viongozi na wananchi walipata fursa ya kuuaga na kutoa heshima zao za mwisho, kwa mpendwa wao aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, marahemu Kapteni Komba.

Watu walishindwa kujizuia huku wengine wakiomboleza kwa sala na wengine wakidondosha machozi, hasa pale ilipofika wakati wa kuruhusiwa kwenda kuuaga mwili huo.

Mara baada ya kuuaga kwenye viwanja hivyo, mwili wake umesafirishwa jioni hii, kuelekea kijijini kwao alikozaliwa, Lituhi wilayani Nyasa. 

Kapteni Komba alifariki dunia, Februari 28 mwaka huu majira ya jioni katika Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam, wakati akiendelea na matibabu.

Rais Jakaya Kikwete atawasili kesho, Marchi 3 mwaka huu majira ya asubuhi mjini Songea na kuelekea kijijini huko, kwa ajili ya kuongoza mazishi yatakayofanyika kwenye makaburi ya kijiji cha Lituhi wilayani humo, majira ya mchana.

No comments: