Monday, March 16, 2015

CCM TUNDURU WATOFAUTIANA JUU YA KALOLO KUWA MGOMBEA PEKEE

Na Steven Augustino,
Tunduru.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, kimetofautiana na tamko la vijana wa chama hicho, katika tarafa ya Matemanga juu ya maamuzi yao  ya kukishinikiza kumtawaza Omary Ajili Kalolo, kuwa mgombea pekee kwa nafasi ya ubunge Jimbo la Tunduru Kaskazini kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Hilo linakuja pia, kwa chama hicho kuwataka wabunge, madiwani na viongozi wengine waliochaguliwa na wananchi kutimiza ahadi walizoahidi wakati wa kampeni ya uchaguzi uliopita, ili kujiwekea akiba ya kuchaguliwa tena vinginevyo wasitegemee kubebwa ili waweze, kushinda katika uchaguzi ujao.

Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tunduru, Hamisi Kaesa alipokuwa akizungumza na maelfu ya wananchi, ambao walikusanyika na kuhudhuria sherehe za ushindi wa chama hicho, katika kijiji cha Mtengashari kata ya Ligunga wilayani hapa.


Akifafanua taarifa hiyo Kaesa, aliwataka pia makatibu wote wa CCM na watendaji wengine ndani ya chama kuanzia ngazi ya tawi, shina na kata kupeleka ofisini kwake majina ya wagombea watakaokubalika na wanachama wengi, vinginevyo wao ndio watakaokuwa wa kwanza kuwajibishwa, ikiwa ni pamoja na kuwafukuza kazi. 

“Mchakato utakapofikia wakati wake wagombea kujinadi, tendeni haki kwa kupendekeza majina ya wagombea, wanaokubalika na wanachama wengi”, alisema Kaesa.

Kaesa aliongeza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa viongozi, ambao watapeleka mapendekezo yatakayotumia utaratibu wa kuchukua au kutumia, maelekezo ya mtu mmoja mmoja kulingana na mapenzi ama nguvu ya fedha. 

“Binafsi siwezi kuwa msemaji wa mgombea fulani, kati ya wanachama ambao watatumia haki yao ya kikatiba, kuomba nafasi za uongozi kupitia chama”, alisisitiza.   

No comments: