Sunday, March 15, 2015

MICHANGO YA WAZAZI MBINGA YACHOTWA KIAINA, YADAIWA KUINGIZWA KWENYE AKAUNTI YA MZABUNI ALIYEPATIKANA BILA KUFUATA TARATIBU

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WAKATI serikali ikiwataka viongozi wake katika Halmashauri mbalimbali hapa nchini kufanya kazi kwa uwazi na kufuata taratibu husika, hali hiyo imekuwa kinyume kwa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, ambapo inadhihirisha pale agizo lililotolewa na Kaimu Afisa elimu msingi wa wilaya hiyo, Alphonce Mwamwile juu ya michango wanayochanga wazazi kwa ajili ya kuendeshea mitihani ya kata na shule mwishoni mwa mwezi na kuingizwa kwenye akaunti ya Rukwa Computer Training Centre, imezua mapya kufuatia baadhi ya Madiwani na Wenyeviti wa shule za msingi wa wilaya hiyo, kudai kuwa hakuna kikao kilichoketi na kujenga makubaliano kwamba fedha hizo zipelekwe huko.

Madiwani na wenyeviti hao walidai kwa nyakati tofauti kuwa, hata mchakato wa zabuni haujafanywa juu ya kumpata mzabuni huyo ambaye hafahamiki ni wa kutoka mkoa au wilaya gani na amepewa jukumu la kuchapa mitihani ya watoto wao, badala yake wanashangaa kuona waratibu elimu kata na walimu wakuu mashuleni wakiagizwa kukusanya michango hiyo na kuiingiza kwenye jina la akaunti hiyo. 

Imeelezwa kuwa agizo hilo lililotolewa na Ofisa elimu huyo linatekelezwa baada ya kuagizwa na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo, Hussein Ngaga kwamba afanye hivyo na fedha ziingizwe kwenye jina la akaunti hiyo jambo ambalo wamesema, kitendo hicho ni wizi wa fedha za wananchi hivyo ni vyema zikafuatwa taratibu husika za kumpata mzabuni kwa kufuata taratibu zenye uwazi na sio vinginevyo, hivyo kutozingatia hilo ni kukosa utawala bora na kuleta migogoro isiyokuwa ya lazima katika jamii.

Mwandishi wa habari hizi amefanikiwa kupata barua yenye kumbukumbu namba W/E/MB/10/VOL.111/66 ya Januari 15 mwaka huu, ambayo inawaagiza waratibu na walimu wakuu wote shule za msingi wilayani Mbinga, kukusanya michango hiyo ya wazazi kwa ajili ya kuendeshea mitihani hiyo na kuiingiza kwenye akaunti namba 62101600263 benki ya NMB, ambayo ni ya Rukwa Computer Training Centre.

Sehemu ya barua hiyo inaagiza kwamba itafanyika mitihani sita ya wilaya kwa darasa la saba mwaka huu, mitihani minne fedha zitatoka kwa wananchi na miwili itatoka kwenye akaunti ya Capitation Grant, hivyo mwanafunzi mmoja kwa mtihani mmoja anapaswa kuchangia shilingi 1,500 kwa masomo ya Hisabati, Kiswahili, Sayansi, Historia, Uraia, Jiografia na Kiingereza.

Kadhalika kwa upande wa darasa la sita, watakuwa na mitihani miwili ambapo nao wanapaswa kuchangia shilingi 1,500 kwa kila mitihani hiyo, kwa muhula wa kwanza mmoja na muhula wa pili mmoja.

Pamoja na mambo mengine nimezungumza na wadau mbalimbali wa elimu wilayani humo, walisema kuwa kitendo hicho hakipaswi kuvumiliwa kwani awali mitihani ya wanafunzi mashuleni ilikuwa ikichapwa kwa kumpata mchapaji ambaye amepatikana kupitia mchakato halali wa zabuni husika, hivyo wanashangaa jambo hilo kufanyika kwa siri na kuwaagiza waratibu na walimu wakuu hao, wakusanye michango hiyo na kuiingiza kwenye akaunti ya mtu ambaye wao hawamfahamu.

Hata wajumbe wa kamati za shule nao walieleza kuwa, michango hiyo inayokusanywa kutoka kwa kila mzazi ambaye ana mtoto anayesoma kwenye shule husika, na kuingizwa kwenye akaunti hiyo ni utaratibu mbaya wenye kuonesha maslahi binafsi ndani yake, ambapo hivi sasa unaleta gumzo na malalamiko yasiyokuwa ya lazima.

Walifafanua mfumo wa uendeshaji mitihani hiyo hasa wakati wa likizo ni mpango ambao hata wazazi wa wilaya hiyo, walijiwekea mikakati yao wenyewe na kujenga makubaliano juu ya namna ya kuinua kiwango cha taaluma, kupitia vikao vya Mabaraza ya kata (WDC) hivyo wanashangaa kuona agizo hilo lilitolewa na fedha ziingizwe kwenye akaunti ya mzabuni ambaye hafahamiki.

“Hapa tunavyozungumza kuna baadhi ya waratibu na walimu wakuu wenzetu ambao wamekwisha ingiza fedha kwenye akaunti ya Rukwa Computer Training Center, ni jambo ambalo sasa madiwani na wenyeviti wa shule za msingi wamekuwa wakija juu na kuhoji kwa nini mambo yanafanyika bila kufuata taratibu”, ? walisema.

WAZAZI NAO WATOA YA MOYONI

Pia nimezungumza na Wazazi kwa nyakati tofauti nao walisema, wanamshangaa Mkurugenzi huyo kuanzisha taratibu za kwake bila kushirikisha wadau husika kupitia vikao mbalimbali, ambapo walifafanua kuwa awali makubaliano yao kupitia vikao vya WDC haikuwa hivyo huku baadhi yao wakisema ni vyema mfumo wa watoto kufanya mitihani mwishoni mwa mwezi, akaziacha taratibu za awali kama wazazi walivyokubaliana katika vikao vyao ambapo asipofanya hivyo mbele wanaona giza kwa maendeleo ya watoto wao kielimu wilayani Mbinga.

“Kiongozi mzuri ni yule ambaye anashirikisha wenzake na sio kuamua mambo yeye binafsi, kwa jambo hili tunamtaka afuate taratibu ambazo sisi wazazi kwa kushirikiana na walimu wetu mashuleni kupitia vikao halali, tulikwisha kaa na kuweka mikakati madhubuti ya kufanikisha watoto wetu wakue kielimu hivyo tunasema hatuhitaji kurudishwa nyuma na mtu yeyote ambaye hana uchungu na maendeleo ya wanambinga”, walisema.

Waliongeza kuwa Ngaga tokea amefika katika wilaya ya Mbinga, ni mtu wa kupenda kutengeneza migogoro ya hapa na pale kila kukicha badala ya kufikiria kufanya maendeleo ya wananchi, hivyo ni wakati sasa kwa serikali kumchukulia hatua za kinidhamu ili iwe fundisho kwake, na watu wengine wenye tabia kama hiyo.

Walieleza kuwa michango wanayochanga wazazi kwa watoto wao ili wajisomee hata wakati wa likizo, sio mpango uliowekwa na serikali bali ni makubaliano yao na walimu mashuleni ambapo kufikia hatua ya kuingiza fedha hizo kwenye akaunti ya mtu ambaye hajulikani ni wizi, na kuingilia matakwa yao ambayo wamejiwekea wao wenyewe hivyo wamemtaka aache kufanya hivyo badala yake afuate taratibu na sio vinginevyo.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Ngaga alipotafutwa ili aweze kuzungumzia madai hayo, hakuweza kupatikana ofisini kwake na simu yake ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa.

Hata hivyo mwandishi wetu, alipozungumza na kaimu Afisa elimu msingi wa wilaya ya Mbinga, Mwamwile alithibitisha kutolewa kwa agizo hilo kwenda kwa waratibu elimu kata na walimu wakuu shule za msingi wilayani humo, akiwataka fedha hizo ziingizwe kwenye akaunti hiyo ili mitihani ya watoto mashuleni iweze kuchapwa.


No comments: