Monday, March 2, 2015

JOTO LA UCHAGUZI NA AJIRA KWA VIJANA



Na Mwandishi wetu,

WAKATI tukielekea uchaguzi mkuu mwaka huu, huku joto la uchaguzi likiendelea kupanda miongoni mwa vyama vya siasa na wagombea wake, huenda wakaanza kuonesha dalili ya kuibuka na sera mbalimbali ambazo huenda zikapewa kipaumbele, katika uchaguzi huo.

Tumeshaona baadhi yao wakisema; ajira kwa vijana huku wakibashiri kwamba endapo chama au mgombea ambaye katika ilani yake hatahusisha ajira kwa vijana, huenda akapewa nafasi finyu katika kinyang’anyiro cha uchaguzi huu, ni wosia toka kwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai.

Wapo  waliodai “vijana ni bomu” kwa kutaka tu kutoa tahadhari endapo hatutakabiliana na kutatua tatizo la ajira kwa vijana, miongoni mwao hasa kwa wale wanaomaliza vyuo vikuu, sekondari na shule ya msingi huenda ipo siku itafika na kuweza kuingia katika wimbi la machafuko kama yalivyotokea katika nchi nyingine kama vile Misri, Algeria na kwingineko.

Vivyo hivyo, tumewasikia wengine wakisema uchaguzi mkuu 2015 uwe wa vijana ambapo katika kundi hili wao wanataka rais kijana ili aje atatue kero au matatizo ya vijana, kwa sababu anayafahamu hivyo ni rahisi kwake kuyatatua na kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu huku wakipigia chapuo, katika ajira kama nguvu kazi ya taifa hili.


Binafsi sina tatizo na kundi lolote lile, ambalo limeibuka na hoja hii ya ajira kwa vijana bali nawapongeza kwa kuliona hili mapema, ili liweze kupata nafasi miongoni mwa watanzania walijadili na kuona ni kwa namna gani, wanaweza wakaliweka sawa ili ifikapo kipindi cha uchaguzi waweze kupima mgombea kutokana na sera zake na mikakati aliyonayo, katika kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana nchini.

Hoja yangu hapa ni kwa namna gani tunaitafsiri ajira kwa vijana kulingana na mazingira ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Ni wakati sasa tukaupanua mjadala kuliko kuuminya ili kuweza kujenga mawazo mbadala yatakayoweza kukabiliana na mazingira yetu ya kiuchumi na kijamii, kwa kuangalia ni kwa namna gani tunaweza kuichanganua sera ya ajira kwa vijana.

Pia kabla ya kuidadavua kiundani sera ya ajira kwa vijana ni vyema tukaweka angalizo ni kwa namna gani, tunajenga mazingira yanayoweza kukidhi mahitaji ya muda mrefu kwa watoto na wazee pale tunapoitafsiri mikakati ya ajira kwa vijana, kama nguvu kazi ili sera kwa vijana iwe na tija zaidi kwa uchumi wa nchi na mahitaji muhimu ya watoto na wazee kwa ujumla wao.

Sambamba na hilo pia ipo haja ya kuangalia kwa kina na kujifunza ni kwa namna gani nchi za wenzetu zilizoendelea, zimeweza kukabiliana na tatizo la ajira licha ya kuwa na idadi kubwa ya watu wake wenye kisomo cha hali ya juu, wakiwa na rasilimali chache huku sisi katika mazingira yetu tuna rasilimali nyingi na kushindwa kuzitumia ipasavyo pale tunapokabiliana na tatizo hili la ajira kwa vijana. 

Pia tujifunze ni kwa namna gani, tunaweza tukageuka nyuma na kutazama sera zetu na kuzibadili kimfumo, kwa mfano licha ya Iran kuwa na msuguano mkubwa na mataifa makubwa wamekubali kukaa meza ya mazungumzo na mataifa hayo, na kwamba hadi sasa dalili zimeanza kuonekana za kuondoa vikwazo huku lengo la wananchi wa Iran ni kulinda uchumi wao na ajira kwa vijana na sio tu mitambo ya  nyukilia ambayo wanayo tokea miaka mingi iliyopita.

Mifano ipo mingi kwa kuanzia China, USA na nchi nyinginezo hivyo ni vyema sasa tukapata kujifunza bila woga, na kamwe tusijifunge kimawazo kwa hoja dhaifu eti hizo ni nchi zilizoendelea kiuchumi, sio rahisi kuweza kuitumia mikakati waliyoitumia na sisi tukafanikiwa.

Mosi suala  la sera lisiwianishwe kwa vigezo tunavyotaka kuvitumia mfano umri wa mgombea, kufanya hivi tunaweza tukashindwa kuitafsiri vema sera ya ajira kwa vijana endapo tutakubali kuegemea katika vigezo vinavyoweza vikaathiri uchanganuzi mpana zaidi, bali vimwandae au iwe ni nguzo katika kumpata kiongozi atakaye tekeleza ajenda ya ajira kwa vijana kwa ufasaha zaidi.

Pili ni kwa namna gani tunalinda ajira kwa vijana wazalendo, nashauri ni vyema tukabainisha ni mikakati ipi tutaiendeleza na kuibua kwa manufaa zaidi ili kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana. 

Mfano tunaona mamlaka zetu zinatoa vibali kwa kupunguza kodi kwa malighafi zetu kusafirishwa nje ya nchi.

Tatu ni kwa namna gani tunawatambua waajiri wadogo wadogo wanaoweza kutoa ajira kwa vijana, mfano kuanzia watano na kuendelea ili waweze kujenga uwezo mkubwa zaidi wa kuwaajiri vijana wetu na kutoa tija zaidi, katika ujira na ajira kwa vijana wengi zaidi je upo mkakati huo na kama upo tunausimamiaje na kama haupo tunawaza nini?

Nne tunawangaliaje wale waliojiajiri hata kwa zile sekta ambazo sio rasmi, ila zina mchango mkubwa katika jamii. Mfano waponda kokoto (zege) wauzaji vyakula maeneo ya barabarani, wale wanaojiita wapiga debe maeneo ya stendi na wengine wengi katika nyanja tofauti.

Tano tunakabilianaje na kazi au ajira zinazoathiri mazingira mfano kilimo maeneo yenye vyanzo vya maji, uchomaji wa mkaa, ufugaji usio na tija. Licha ya juhudi za kusambaza umeme hata maeneo ya vijijini, nishati kubwa yakupikia imekuwa ni kuni na mkaa hivyo tujipe tafakari endapo tutaendelea kuona kila shughuli ni ajira, tujue ipo siku ukame utatufukarisha je, akinamama ambao ni walezi wa familia watayapata maji wapi ukizingatia kwamba uharibifu wa mazingira, ni kukaribisha ukame ambao baadaye ni balaa kwa viumbe hai.

Sita tuangalie ni kwa namna gani, waajiriwa wanakumbana na changamoto mbalimbali hasa mikataba yao katika ajira na sheria zinazolinda ajira zao, mfano tumeshawahi kuona serikali ikitangaza mishahara ya ajira katika sekta binafsi lakini hadi leo imekuwa ni vigumu kujua ni kwa namna gani, maagizo hayo yanatekelezwa mfano ajira za wafanyakazi majumbani, mashambani na kadha wa kadha.

Saba inatupasa tuangalie mifumo yetu ya uwekezaji kama inakidhi matakwa na matarajio ya watanzania kwa kiasi gani?, ni kwa namna gani rushwa na uwajibikaji finyu unaathiri mchakato mzima wa kulinda na kutetea ajira kwa vijana wetu wa kitanzania?, endapo tumeshindwa kukabiliana na rushwa ndogo ndogo na ufisadi ambao unaendelea je hatuoni suala la rushwa na ufisadi linaathiri mchakato mzima wa ajira kwa vijana wetu.

Nane tuangalie tija ya ajira na ujira kwa mapana zaidi, ili iweze kukidhi matakwa ya kiuchumi na kijamii na tufikirie zaidi kutokana na mazingira yetu ni kwa namna gani huyu kijana wakati ana nguvu analiingizia taifa faida, je ni ipi kinga yake afikiapo uzeeni?, ipi kinga ya huyu kijana kwa familia yake mfano watoto wake pamoja na mambo mengi zaidi ya hapo, tusiishie kuimba wimbo wa ajira tu.

Tisa tunawianishaje suala la ajira na sekta mbalimbali za uzalishaji mali ni kwa namna gani, tunabuni miradi mikubwa na midogo ya muda mfupi na muda mrefu ili kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana wetu kutokana na historia ya siasa yetu, maana tulishawahi kuambiwa ajira millioni moja lakini hadi leo tunaona vijana wetu wakijaa uwanja wa taifa kugombania nafasi 70, je ndio hizo tulizoahidiwa million?

Kwa maoni yangu binafsi tunapochambua sera na mikakati ya ajira kwa vijana, ni lazima tuichambue kwa mapana zaidi na kuiwekea mikakati kwa misingi ya sekta na idara tofauti tofauti, ili ajira ziweze kuongezeka kwa vijana kujiajiri wenyewe na wengine kuajiriwa, iwe ndani ya nchi au nje ya nchi.

Hitimisho langu ni kwamba tunapozungumzia ukosefu wa ajira tujue hakuna kiwanda kinachozalisha ajira, bali sera za uchumi ndizo zitakazozalisha ajira hivyo siasa isiyo na mipango na mikakati ya kiuchumi sio mwafaka na tija katika kukuza uchumi na kuzalisha ajira, hivyo mgombea atakayesema ataongeza ajira, lazima apambanue ni kitu gani atafanya sio ajira za hewani au kama anatoka usingizini, aeleze pia mipango na mikakati ya kiuchumi itakayoibua ajira na sio kuishia katika propaganda za kisiasa tu ambazo nimejifunza katika maeneo mbalimbali utekelezaji wake unakuwa mgumu.

No comments: