Saturday, March 21, 2015

ASHIKILIWA KWA KOSA LA UBAKAJI

Na Amon Mtega,
Songea.

MKAZI mmoja ambaye anaishi mtaa wa Changalae kata ya Mletele Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Hamis Milanzi (68) anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani humo, kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi mwenye umri wa  miaka (13) anayesoma shule ya msingi Luhila seko iliyopo mjini hapa.

Akizungumza na Waandishi wa habari, Kaimu kamanda wa polisi wa mkoa huo, Yahaya Athumani alisema tukio hilo lilitokea majira ya jioni katika mtaa huo ambapo mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo, baada ya kumtishia mtoto huyo kwamba akikataa kufanya naye mapenzi atamfanya kitu kibaya huku akimrubuni kwa kumpatia shilingi 30,000.

Yahaya alisema kuwa mwanafunzi huyo, ambaye jina lake linahifadhiwa anaishi kata ya Mletele ambapo alikwenda nyumbani kwa mtuhumiwa huyo kumdaifedha za kuni ambazo alimkopesha na alipowasili huko, aliambiwa na mtuhumiwa huyo aingie ndani ili apewe fedha hizo.


Alisema baada ya kuingia ndani, ghafla mwanafunzi huyo alijikuta anakamatwa kinguvu na kuanza kubakwa huku akimtishia kuwa kama atapiga kelele atauwawa na kwamba asimwambie mtu yeyote, kutokana na tendo alilofanyiwa.

Mara baada ya mtuhumiwa kukamilisha kufanya unyama huo, alimwambia mwanafunzi huyo aendelee kubakia hapo nyumbani kwake na kwamba alimuahidi kumpa fedha kiasi cha shilingi 30,000.

Kwa mjibu wa kaimu kamanda huyo, alisema wazazi wa mwanafunzi huyo waliendelea kumtafuta kwa muda wa siku nne mtoto wao, ambapo walimkuta kwenye duka lililopo maeneo hayo akiwa ananunua mahitaji tayari kwa kwenda kufanya maandalizi ya kupika chakula nyumbani kwa mtuhumiwa huyo ambaye alimgeuza mwanafunzi huyo akiwa mwandani wake.


Pamoja na mambo mengine, baada ya wazazi hao kumuona walimfuata taratibu ili wajue anaingia nyumba gani, ndipo waliona akiingia kwa Hamis Milanzi na ndipo taratibu za kumkamata na kutoa taarifa kwenye vyombo husika zilianza kuchukua mkondo wake ambapo mpaka sasa polisi wanaendelea na uchunguzi juu ya tuhuma hizo na mara utakapokamilika mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani kujibu kosa linalomkabili.

No comments: