Saturday, March 14, 2015

MAASKOFU JUKWAA LA WAKRISTO WAKOLEZA MOTO KUIKATAA KATIBA MPYA

Padre Baptiste Mapunda.
Na Padre Baptiste Mapunda,

GAZETI la mwananchi, ijumaa iliyopita, Machi 13 mwaka huu lilikuwa limebeba ujumbe mzito kwa Watanzania wenzangu, katika kichwa cha habari,  “Maaskofu: Pigieni Katiba kura ya hapana.”

Maaskofu wa Jukwaa la Wakristo ambao ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo (CCT) Askofu Dokta Alex Malasusa, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu katoliki Tanzania (TEC) Askofu Tarcicius Ngalalekumtwa  na Mwenyekiti wa Kanisa la Pentekoste Tanzania (CPCT) Askofu Daniel Awet kwa sauti moja, wamewataka waumini wao kujiandikisha kwa wingi katika daftari la wapiga kura, kuisoma vyema katiba pendekezwa na hatimaye kuikataa “kata kata” kwa kuipigia kura ya hapana.

Sababu kuu za kuwahamasisha waumini wao na Watanzania kuikataa katiba pendekezwa ni mbili.

Mosi ni kulazimisha kura ya maoni ya katiba mpya, kufanyika bila maandalizi ya kutosha yakiwamo maridhiano ambayo yameligawa taifa katika vipande vipande.

Pili viongozi waandamizi wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuupigia debe muswada wa Mahakama ya kadhi, wakati wanajua kwamba kufanya hivyo ni kukiuka misingi ya taifa ambayo Baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere, aliunda taifa lenye serikali isiyo na dini.

Tamko hili nyeti ambalo limesambaa katika makanisa mengi ya kikristo iwapo litasomwa kwa waumini wote na kuhamasishwa na mapadre, wachungaji, na wainjilisti basi unaweza ukawa ndiyo mwisho wa katiba pendekezwa kupigiwa kura 30 April mwaka huu.

Viongozi wa Jukwaa hilo wanawajibu wa kushiriki kikamilifu katika zoezi hili la kuandika katiba mpya, ambalo linawahusu waumini wao pia. Tunatambua, katiba si suala la siasa bali ni la Watanzania wote.

Itakumbukwa kuwa CCM, ilitumia mabavu na pesa nyingi sana katika  kusimamia mijadala ya katiba mpya wakati mwingine hata kwa mitutu ya bunduki, wakapitisha  katiba pendekezwa  kwa kutumia  vyombo vya dola na  wakakabidhiana kwa kutumia mabavu pia.

Hofu ya kukataliwa kwa katiba mpya, kumeifanya serikali ya Jakaya Kikwete ivunje kabisa makubaliano na TCD, kwamba kura ya maoni ingesitishwa hadi  baada ya uchaguzi mwaka 2016. 

Lakini kwa sababu tu ya hofu ya kuanguka madarakani kwa CCM, wameamua kuendelea kulazimisha kura ya maoni kwa kutumia  mabavu  na kuwaburuza wananchi. Hii naweza nikasema ni alama au ishara ya kuanguka kwa serikali iliyopo madarakani.

Matokeo yake inafanya kila hila ili daftari hili la wapiga kura, lisiboreshwe na waweze kuchota kura vizuri  kiholela holela. Nionavyo mimi hofu kuu hapa ni katiba hii kuja kukataliwa na umma, hivi  Rais Kikwete ameona heri aendelee  kuisukuma walau ikubalike na umma.

Lakini ukweli ni kwamba katiba hii imekataliwa na wananchi wengi pia hata na Mungu kwa sababu “sauti ya wengi ni sauti ya Mungu”.

Sababu nyingine kubwa ya kukataliwa na wananchi, wakiwamo Maaskofu ni katiba pendekezwa yenye kulenga kulinda maslahi ya watu wachache ndani ya chama na serikali ya  CCM.

Kuvuruga uchaguzi kwa kutumia katiba mbaya na kanuni mbaya ndiyo mwanzo wa machafuko, vita na mauaji kama yale yaliyotokea nchini Kenya  mwaka 2007, Kibaki alipolazimisha ushindi na akaapishwa usiku usiku mbele ya watu wachache tu.

Katiba mpya inabidi ilete amani na siyo machafuko. Ukisoma alama za nyakati hayo ndiyo yanayokuja mbele yetu hivyo Watanzania tujiulize tunataka nini?

Katika mkutano wa Maaskofu hao uliofanyika tarehe 10 Machi mwaka huu walisema kwamba; “Katiba inayopendekezwa imeleta mgawanyiko mkubwa katika taifa hili, kwani imepatikana kwa njia zisizo za kiadilifu na mchakato wake umeendeshwa kwa hila na ubabe”.

Viongozi hao kama wadau wa demokrasia, amani, na ustawi wa taifa letu  wamewaomba waumini wao kujiandikisha kwa wingi  katika daftari la wapiga kura na kwenda kupiga kura ya “hapana” kwa katiba pendekezwa.

Maaskofu wana wajibu na haki ya kutoa mwelekeo kwa waumini wao ili wachague kitu kizuri na siyo kibaya kitakachokuja kuwadhuru hapo baadaye. Kama viongozi wa dini na jamii hawawezi kuacha kuitahadharisha jamii juu ya hatari iliyopo mbele yao hatuwezi kulipeleka taifa hili katika misingi ya uatwala bora.

Kwa upande wa UKAWA  wanaonekana kama walipata maono  ya kusoma alama za nyakati wakasusia bunge la katiba, uamuzi wa kutoshiriki uovu huo ulikuwa mzuri na leo wapo huru kwamba hawakushiriki dhambi hii, ya mauaji ya demokrasia nchini Tanzania.

Ikiwa mchakato mzima wa upatikanaji wa katiba pendekezwa umekiuka sheria ya mabadiliko ya katiba maana yake ni  kwamba katiba pendekezwa ni feki, haina uhalali wowote wa kisiasa, umekosa maridhiano na wala haukubaliki kwa wananchi   wazalendo wa Tanzania.

Lakini tamko hili  la Maaskofu hao wa Jukwaa la Wakristo linasema wazi  kabisa na kushangazwa na kitendo cha serikali kuahidi kuwapatia Waislamu Mahakama ya Kadhi kinyume  na katiba ya nchi yetu. Tamko linasema kwamba “kwa hali kama hii, Kanisa haliwezi kuunga mkono kupitishwa  kwa katiba inayopendekezwa.”

Nimeshangazwa na tamko la Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kwamba makundi ya dini mbalimbali yamekuabiliana juu ya uwepo wa mahakama ya kadhi. 

Ninamwomba  waziri Mkuu “aache kuwa sehemu ya tatizo la katiba na imani za dini  bali awe jawabu lenye kuleta amani, umoja, upendo na mshikamano” kwa Watanzania kama alivyofanya Baba wa Taifa.

Maaskofu hao wanaendelea kubainisha jinsi usalama wanchi na raia ulivyozorota na kuanza kuzalisha vikundi vya kihuni na ujambazi kama “Panya road, Mbwa mwitu nakadhalika. Kama wadau wakubwa wa amani nchini wana haki ya kuongelea suala hili nyeti kwa sababu amani ikitoweka viongozi wa dini wanakuwa wa kwanza kulaumiwa kama ilivyotokea nchini Rwanda.

Tamko la Maaskofu hao “Kataeni katiba” naliona la “kinabii na la kimapinduzi” lililokuja muda mwafaka ambapo waumini wa Kikristo walikuwa hawana mwelekeo juu ya suala la kura ya maoni ya katiba pendekezwa, na suala la Mahakama ya kadhi, ndiyo maana naandika Maaskofu wa Jukwaa la Kikristo wachochea moto wa kuikataa katiba pendekezwa.
Mungu ibariki Tanzania na watu wake.


Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa barua epepe; frmapunda91@gmail.com

No comments: