Saturday, March 14, 2015

RUVUMA NAO WAPINGA MAUAJI YA ALBINO, WASEMA SERIKALI IWEKE MIKAKATI MADHUBUTI KUDHIBITI VITENDO HIVYO

Na Kassian Nyandindi,   
Songea.

KUTOKUWEPO kwa matukio ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi Albino mkoani Ruvuma,  wananchi wa mkoa huo wameendelea kulaani vitendo hivyo vya ukatili dhidi ya kundi hilo tete, ambavyo vimekuwa vikiendelea kujitokeza katika maeneo ya kanda ya ziwa hapa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Katibu msaidizi wa chama cha watu wenye ulemavu wa ngozi mkoani hapa, Fatuma Jumbe alisema kundi hilo la watu wenye ulemavu wa ngozi linahitaji uangalizi wa hali ya juu na kuitaka serikali, kuweka mikakati madhubuti ambayo itaweza kufanikisha katika kupambana na kuwakamata watu wenye kushiriki kwa namna moja au nyingine kuua albino.

Lakini alipongeza uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kukutana na wawakilishi wa kundi hilo, pamoja na kuahidi kuunda tume ya kushughulikia vitendo hivyo vya kikatili, dhidi ya watu hao wenye ulemavu wa ngozi.


Fatuma alieleza kuwa vitendo hivyo vya ukatili dhidi ya kundi hilo, ambalo limekuwa likiishi kwa hofu kubwa dhidi ya vitendo viovu wanavyofanyiwa linaleta wasiwasi hata kwa makundi mengine ya walemavu, ambayo alishauri pia nayo yawe katika uangalizi mkubwa na sio kungojea mpaka pale tatizo linapotokea ndipo hatua zichukuliwe.

“Hali hii kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele, tunajikuta tupo katika wakati mgumu sana, sijui tufanyeje lakini tunazidi kuomba Mungu atuepushe na majanga haya”, alisema.

Naye, Prisela Chales mwanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana Songea ambaye ni mlemavu wa ngozi, alisema kuendelea kuwepo kwa vitendo hivyo kunawatia hofu wao na kuwakatisha tamaa ya kuendelea na masomo kwa kutojua hatima yao hasa pale wanapoamka mapema alfajiri, kwa ajili ya kuelekea shuleni kuhudhuria masomo darasani.

Naye makamu mkuu wa shule ya sekondari ya wasichana Songea, Winna Likiliwike akizungumzia hali hiyo alifafanua kuwa shule yake ina watoto wenye ulemavu wa ngozi na vitendo hivyo, ambavyo vinaendelea kufanyika hasa maeneo ya kanda ya ziwa vimekuwa vikiathiri wanafunzi wake katika kuhudhuria masomo.

Ameziomba mamlaka husika kufikia hatua ya kuchukua maamuzi magumu, dhidi ya wahusika ambao wamekuwa wakithubutu kukata viungo vya watu wenye ulemavu na hata kukatisha maisha ya watu wa kundi hilo, ni vyema nao wakaadhibiwa kulingana na kosa hilo kwa mujibu wa sheria zilizopo.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, kilichofanyika hivi karibuni kijiji cha Mpitimbi B wilayani Songea, alisema serikali mkoani Ruvuma haitamvulia mtu yeyote atakayetajwa kuhusika na vitendo hivyo vya ukatili hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa haraka iwezekanavyo.

Mwambungu aliongeza kuwa kundi hilo lenye ulemavu wa ngozi, lina haki sawa ya kuishi na hakuna mtu yeyote mwenye haki ya kukata kiungo chochote cha binadamu mwenzake, au kukatisha uhai wake kwa lengo la kujipatia kipato sasa ni lazima sheria ichukue mkondo wake na huku akiziagiza mamlaka zote kuanzia ngazi ya familia mpaka mkoa, kuhakikisha kwamba hakuna vitendo vya namna hiyo ambavyo vitaweza kujitokeza.


No comments: