Tuesday, March 24, 2015

UKOSEFU WA FEDHA WASABABISHA MRADI WA MAJI KUTOKAMILIKA KWA WAKATI

Na Julius Konala,
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa kutokamilika kwa wakati, ujenzi mradi wa maji Kihongo uliopo katika kijiji cha Kihongo, kata ya Mapera wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, unatokana na ukosefu wa fedha hivyo serikali imeombwa kutekeleza hilo ili mradi huo, uweze kujengwa kwa haraka na wananchi waweze kuondokana na adha ya ukosefu wa maji.

Hayo yalisemwa kupitia taarifa fupi iliyosomwa na Afisa mtendaji wa kijiji cha Kihongo, Danstan Hyera kwenye maadhimisho ya kilele cha wiki ya maji yaliyofanyika kimkoa katika kijiji hicho wilayani Mbinga.

Aidha Hyera alisema kuwa, hivi sasa hata kazi za ujenzi zimesimama hivyo kuna kila sababu kwa serikali kuona umuhimu wa kuwezesha mradi huo uweze kukamilika kwa wakati ili wananchi wapate huduma bora ya maji.


Katika maadhimisho hayo mgeni rasmi mkuu wa wilaya hiyo, Senyi Ngaga ambaye alikuwa akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu aliwataka wananchi kutunza vyanzo vya maji na kuacha kuharibu mazingira ili kuepukana na ukame unaoweza kujitokeza baadaye baada ya mazingira hayo kuharibiwa.

Ngaga alieleza kuwa vitendo vya ukataji miti, kulima kwenye vyanzo vya maji na uchomaji moto wakati wa kiangazi ni mambo ambayo ni adui wa mazingira, yanapaswa kukemewa wakati wote ambapo wananchi wanapaswa pia kupewa elimu mara kwa  mara juu ya hilo, ili waweze kuachana navyo.

“Natoa wito kwa wananchi wote wa wilaya hii, tuache tabia ya kukata miti hovyo na kuchoma moto misitu wakati wa kiangazi, ikiwemo hata kulimna kwenye vyanzo maji endapo hatutazingatia haya tutakaribisha ukame na kufanya shughuli nyingi za kimaendeleo zishindwe kusonga mbele kutokana na kukosa maji”, alisema.

Kadhalika Ngaga aliweza kuweka jiwe la msingi katika ujenzi mradi wa maji wa wananchi wa kijiji hicho cha Kihongo, ambapo hadi kukamilika kwake utagharimu kiasi cha shilingi milioni 827,329,140.

Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga, alitumia pia fursa hiyo kuwataka wananchi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la wapiga kura, mara zoezi hilo litakapoanza kutekelezwa katika wilaya hiyo.


Pamoja na mambo mengine, naye Mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (MBIUWASA) Salvatory Mugarula alisema ili kuziwezesha taasisi za umma kutoa huduma bora kwa raia na wateja wake, kuna kila sababu kwa taasisi kuzingatia viwango na ubora wa huduma ili kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya lazima, miongoni mwa jamii.

No comments: