Saturday, March 21, 2015

PADI YAWAPIGANIA WAZEE KUTENGEWA BAJETI WAWEZE KUONDOKANA NA CHANGAMOTO MBALIMBALI KATIKA MAISHA YAO

Mkurugenzi wa PADI Iskaka Msigwa, akipokea tuzo ya kutoa huduma bora kwa wazee, na kuweza kutoa fedha za matibabu kwa wazee walioko mkoa wa Ruvuma kupitia shirika hilo Novemba 26, 2011. 
Na Julius Konala,
Songea.

HALMASHAURI ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, imetakiwa kutenga fedha katika bajeti yake kila mwaka, kwa ajili ya kuwahudumia wazee wasiojiweza ambao wamepoteza nguvu zao kutokana na kupigania taifa hili, katika mambo mbalimbali hususani ya kimaendeleo.

Mkurugenzi mtendaji wa shirika la kuhudumia wazee Tanzania (PADI) Iskaka Msigwa, alisema hayo alipokuwa akizungumza na timu ya wataalamu wa Halmashauri ya wilaya hiyo, kwenye mkutano wenye lengo la kuhamasishana juu ya masuala ya wazee kuingizwa kwenye bajeti, uliofanyika mjini Songea.

Msigwa alisema kuwa hatua hiyo, imefikiwa baada ya kuona kwamba kundi hilo limesahaulika kwa muda mrefu huku likikabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo kushindwa kumudu gharama za maisha, na kubeba mzigo mzito wa kuwatunza watoto yatima ambao wameachwa na wazazi wao baada ya kufariki dunia kutokana na ugonjwa wa ukimwi au ajali, hivyo ameiomba serikali na jamii kwa ujumla kuwajibika katika kuwatunza.

Kufuatia hali hiyo, taasisi mbalimbali za kifedha nazo zimeombwa kuangalia uwezekano wa kuyasaidia makundi hayo kwa kuyakopesha hata fedha, kwa madai kwamba wazee wanakopesheka kutokana na kuwa waaminifu lakini pia serikali ione umuhimu wa kuwalipa pensheni, kwa ajili ya kuwapunguza ukali na ugumu wa maisha.


Mkurugenzi huyo alifafanua kwamba, katika kukabiliana na changamoto hizo ambazo wazee hukabiliana nazo, shirika la PADI limeweza kuwanufaisha wazee 4,500 kwa kuwakopesha kuku kupitia mradi wake wa kopa kuku, lipa kuku na kudai kwamba mpango huo malengo yake ni kuwafikia wazee 1,500.

Aliongeza kwa kusema kuwa shirika hilo, pia lina mpango wa kujenga kliniki ya wazee ambayo itasaidia kutibu magonjwa yasiyoambukiza yanayowasumbua mara kwa mara, ili kuweza kuwaepushia usumbufu na msongamano wa kukaa kwenye foleni kwa muda mrefu katika hospitali nyingine ambazo hutoa huduma kwa makundi hayo.

Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa mkutano huo, walipozungumza na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti,  walipongeza shirikahilo la PADI kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha, kusaidia na kupigania haki za wazee hao, huku wakitambua mchango wao mkubwa walioutoa katika taifa hili.

Walisema ukakasi wa kutenga fedha kwa ajili ya kuwasaidia wazee, unatokana na sera na miongozo mibovu, inayotolewa na serikali ndio maana imekuwa kikwazo kikubwa kwao katika kufanikisha jambo hilo, hivyo ni vyema serikali ikaona umuhimu wa kuliingiza  jambo hilo ili liweze kutambulika katika sheria kwa ajili ya utekelezaji zaidi.

Naye Afisa maendeleo ya jamii kutoka kata ya Mpandangindo wilayani Songea, Teodora Ilomo alisema wazee wanapaswa kuenziwa kutokana na mchango wao mkubwa walioutoa katika taifa hili na kuwa tegemeo kubwa katika jamii, kutokana na kazi mbalimbali wanazozifanya ikiwemo katika suala la utatuzi wa migogoro, kuosha maiti na kuzalisha watoto hali inayopelekea baadhi yao kuathirika na magonjwa ya ukimwi kutokana na kutochukua tahadhari wakati wa kuosha na kuzalisha, jambo ambalo ameomba elimu ya afya iendelee kutolewa dhidi yao.


Kaimu afisa elimu wa wilaya hiyo, Tanu Kameka ameitaka jamii kutambua kuwa wazee ni hazina kubwa lakini inashangaza baadhi ya watu wanathubutu kuwauwa kwa kisingizio cha kuwaita wachawi, huku akiiomba serikali kuwashirikisha wazee katika suala la kutoa elimu kwa vijana juu ya kujifunza utamaduni, mila na desturi za kitanzania, ambazo ni nzuri zinafaa kwa ajili ya kuibadili jamii kimaadili kwa kutokana na wengi wao kupoteza mwelekeo.

No comments: