Saturday, March 14, 2015

WATANZANIA WATAKIWA KUISHI KWA KUZINGATIA SHERIA

Na Amon Mtega,
Songea.

WATANZANIA wakati wote wa maisha yao ya kila siku, wametakiwa kuishi kwa kuzingatia sheria zilizowekwa, ili kuepusha migogoro ambayo inaweza kujitokeza baadaye katika jamii hasa pale inapotokea kundi moja au jingine, hukiuka taratibu na kutozingatia miongozo ya sheria.

Naibu Askofu wa Jimbo kuu la Songea mkoani Ruvuma, Padre Camillius Haulle alitoa rai hiyo alipokuwa kwenye sherehe ya kuwaaga wahitimu wa mafunzo ya msaada wa kisheria (Paralegle) yaliyofanyika katika kituo cha  kisheria cha, African Institute for Comparative and International Law (AICL) kilichopo Mahenge mjini hapa.

Haulle alisema kuwa kama watanzania watatambua umuhimu huo, huenda hata migogoro ambayo hujitokeza mara kwa mara katika jamii ikapungua au kwisha kabisa na kulifanya taifa, kuwa na watu ambao ni mfano bora mbele ya mataifa mengine.


Alisema, nchi yeyote ambayo watu wake wanaishi bila kuzingatia sheria ambazo zimewekwa kwa mujibu wa taratibu husika, ni lazima kutakuwa na machafuko makubwa kutokana na kila mmoja kutaka kutumia mabavu kulingana na nafasi aliyonayo.

“Ndugu zangu sheria ni kama mlango ambao unazuia kutoka au kuingia, bali kuwepo na sababu zinazoufanya ufunguliwe au ufungwe, hivyo ndiyo inavyotakiwa Mtanzania aishi  kwa kuzingatia haya”, alisema Askofu Camillius.

Kwa upande wake, Mrakibu msaidizi wa Jeshi la Polisi (ASP) Anna Tembo kutoka kituo cha Songea alisema wahitimu hao watasaidia kutoa misaada ya kisheria kwa jamii na kupunguza migogoro, ambayo huwa inaleta migongano ndani ya familia.

Anna ambaye pia ni Mwenyekiti wa dawati la jinsia na watoto mkoani Ruvuma, alibainisha kuwa uwepo wa migogoro mingi ndani ya jamii, hasa kwa watu wa ndoa husababisha kuyumbisha familia zao na kuzifanya zishindwe kusonga mbele kimaendeleo.


Mwenyekiti huyo alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo, aliongeza kuwa hivi sasa kumekuwepo na wimbi la baadhi ya mabinti, kutoa mimba na kuvitupa vichanga, huku akiitaka jamii kuachana na vitendo hivyo na endapo wahitimu hao watafanya kazi ya kutoa msaada wa kisheria juu ya madhara yanayoweza kujitokeza baadaye, hakika jamii itabadilika na hatimaye kuweza kuondokana na hali hiyo.          

No comments: