Saturday, March 14, 2015

TEKINOLOJIA MPYA YA UHIFADHI MAZAO YAZINDULIWA RUVUMA

Na Nathan Mtega,
Songea.

KITUO cha hifadhi ya taifa ya chakula (NFRA) cha Songea mkoani Ruvuma, kwa kushirikiana na kampuni ya uhifadhi wa chakula ya AGRA kimezindua teknolojia mpya ya uhifadhi wa mazao, ambao utasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti uharibifu wa mahindi ambayo zaidi ya tani 78,000 yamehifadhiwa nje ya maghala, huku mengine yakiendelea kuharibika kutokana na kituo hicho kuelemewa na wingi wa zao hilo ambayo huzalishwa na wakulima mkoani humo.

Maghala ya kituo hicho, yana uwezo wa kuhifadhi tani 26.000 na kwa mujibu wa Mkurugenzi wa hifadhi ya chakula taifa, Charles Warwa alisema zaidi ya tani 78.000 yameshindwa kuhifadhiwa ndani ya maghala na kulazimika kuyaweka nje, ambapo baadhi ya magunia ya mahindi yameanza kuharibika na kuliwa na wadudu, kutokana na teknolojia duni ya uhifadhi wa chakula unaofanywa katika kituo hicho.

Alisema hali hiyo inawafanya wafanyakazi wa hifadhi ya chakula katika ngazi ya mikoa na taifa, kuwakosesha usingizi lakini ujio wa teknolojia mpya ya uhifadhi wa chakula iliyoletwa na kamuni washirika ya AGRA, itakuwa ni ufumbuzi tosha wa changamoto hiyo ambapo kwa kituo cha Songea kuna tani zaidi ya 78,000 zimehifadhiwa nje kwa kutumia telnolojia ya zamani, ambayo hudhoofisha ubora wa mazao na kuharibu soko la ndani na nje.


Akizungumzia hilo, mwakilishi wa kampuni hiyo ya AGRA Tanzania, Dokta Mary Mgonja alisema kampuni hiyo imekuja na teknolojia mpya ya kunusuru uharibifu huo kwa kutumia uhifadhi wa kisasa wa chakula, wakianzia ngazi ya jamii hadi hifadhi ya chakula ya taifa ambao hauna gharama ya kutumia madawa, ambayo wakulima wengi wamekuwa wakishindwa kumudu kuyanunua na kujikuta mazao yao yakiishia kuharibika.

Baadhi ya wakulima wa mahindi wilayani Songea mkoani Ruvuma, pamoja na kuonesha wasi wasi wa mbinu hiyo ya uhifadhi wa chakula lakini wamepongeza kampuni hiyo kwa kuja na njia mbadala ya uhifadhi wa mazao yao, ambayo haina gharama kubwa na itapunguza uharibifu wa mazao huku mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu akisema mpango huo ni mzuri na umekuja wakati muafaka kwa sababu uzalishaji wa mazao yanayohitaji uhifadhi huo, yamekuwa yakiongezeka kwa kasi kubwa.


No comments: