Friday, June 21, 2013

MAKAO MAKUU YA CCM TAIFA YASITISHA UCHAGUZI WA MWENYEKITI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA MBINGA KUFUATIA VURUGU ZILIZOJITOKEZA

Madiwani wa Mbinga, wakitoka nje ya Ukumbi wa CCM wilaya ya Mbinga mara baada ya kupewa taarifa ya kusitishwa kufanyika kwa uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo.(Picha na Kassian Nyandindi)



Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

HALI ya kisiasa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, imeendelea kuwa katika hali mbaya yaani sintofahamu, kufuatia Makao makuu ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Taifa kusitisha zoezi la uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, kutokana na vurugu zilizojitokeza.

Usitishaji huo umefanyika leo majira ya saa 10:00 baada ya Katibu wa CCM wa mkoa huo Verena Shumbusho kutoa taarifa mbele ya Madiwani wa wilaya hiyo kwamba, uchaguzi huo hauwezi kufanyika mpaka taarifa rasmi itakapotolewa kutoka ofisi ya makao makuu ya chama hicho.

Sababu za msingi za kutofanyika kwa uchaguzi huo zimebainishwa katika kikao hicho kilichoketi kati ya Katibu huyo, Madiwani na Uongozi wa Chama hicho wilaya ya Mbinga, ambapo Shumbusho alieleza bayana mbele ya Wajumbe (Madiwani) kwamba wawe na subira mpaka taarifa hiyo itakapotolewa juu ya kufanyika kwa uchaguzi huo, kwamba utafanyika lini.

Wajumbe ambao ni madiwani waliokuwepo kwenye ukumbi wa CCM ambako mkutano huo wa dharula ulikuwa ukifanyika, ndani ya kikao hicho walimweleza Katibu wao wa mkoa wa Ruvuma wa chama cha mapinduzi kwamba, endapo kama watataka kuwepo na amani ni vyema majina matatu ya wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti yarejeshwe na sio kuletewa majina mawili kama ilivyokuwa awali.


Wengine walionekana kujawa jazba huku wakisema hawapendi tabia za viongozi wa wilaya na mkoa kwa ujumla, kuwapangia safu za uongozi hivyo wanachohitaji itumike demokrasia huru na yenye haki.

Hatua hiyo imefikia kufuatia Madiwani hao kujenga msimamo wa kutokubali kufanya uchaguzi huo, kutokana na kile kinachodaiwa kuwa uongozi wa CCM mkoa wa Ruvuma, kutotenda haki katika uteuzi wa majina ya wagombea wa nafasi hiyo ya Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga.

Hali si shwari ambapo baadhi ya madiwani walionekana wakija juu na kuutaka uongozi husika kutenda haki, na kwamba ifikapo kesho Juni 22 mwaka huu halmashauri ya wilaya ya Mbinga inatarajia kuvunja baraza lake la madiwani ili kujenga uongozi wa pande mbili za wilaya ya Mbinga na Nyasa.

Wilaya ya Nyasa imekwisha fanya uchaguzi lakini kwa upande wa wilaya ya Mbinga, imeshindwa kufanya uchaguzi kutokana na vuguvugu hilo ambalo bado linaendelea kufukuta wilayani humo.

Hivyo kwa siku ya kesho ambayo Madiwani wanataraji kuvunja baraza la halmashauri kwa upande wa wilaya ya Mbinga ambako hakuna uchaguzi uliofanyika, utaratibu unasema kwamba wilaya hiyo katika kikao cha kuvunjwa kwa baraza hilo Mwenyekiti wa CCM wa wilaya,Chiristantus Mbunda ndiye atakayeweza kusimamia mustakabali mzima wa zoezi hilo kwa upande wa Mbinga.

Taarifa zilizotufikia hivi punde zinaeleza kwamba wilaya ya Nyasa aliyekuwa Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Oddo Mwisho ndiye ambaye amepata ushindi wa kuongoza wilaya ya Nyasa huku makamu wake akiwa bwana Vurma Whero. (Matokeo zaidi tutawajulisha juu ya uchaguzi huo wa wilaya ya Nyasa ulivyofanyika.)

Awali Madiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Mbinga walionekana wakisota kwa muda mrefu, katika eneo karibu na viwanja vya ofisi ya chama hicho wakisubiri hatma ya uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti, wa kuongoza halmashauri ya wilaya hiyo.

Madiwani hao ambao walionekana wakiwa na jazba huku wengine wakisema “hapa leo hakitaeleweka endapo kama hatutatendewa haki kwa kile kinachotakiwa”.

Mwandishi wa habari hizi alifanya mahojiano na madiwani hao kwa nyakati tofauti ambapo walisema wanachosubiri ni hekima ya chama na kama hakutakuwa na busara ambayo itatumika wao hawatelewa kitu na msimamo wao utaendelea kubaki pale pale.

Awali kufuatia vurugu hizo, katika hali isiyokuwa ya kawaida usiku wa kuamkia leo ofisi ya Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, imenusurika kuteketea kwa moto kufuatia watu wasiojulikana, kuichoma moto kwa kutumia mafuta aina ya petroli.

Ofisi hiyo imechomwa madirisha na mlango mmoja huku ndani yake mapazia yaliyowekwa madirishani, yakiwa yameteketea kwa moto.

Katibu wa CCM wilaya ya Mbinga Anastasia Amasi alisema kuwa yeye akiwa nyumbani kwake alipata taarifa za kuchomwa moto kwa ofisi hiyo majira ya saa 2:07 asubuhi ya leo, ambapo alipofika katika eneo la tukio aliona uharibifu huo ukiwa umekwisha fanyika.

Taarifa zilizotufikia zinaarifu kwamba huenda Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu akawasili kesho hapa Mbinga, kwa ajili ya kuweka sawa hali hii ya upepo wa kisiasa ili isiweze kuendelea kuvurugika. (Ndugu Wasomaji wa mtandao huu, tutaendelea kuwajuza nini kinachoendelea juu ya tukio hili, endelea kufuatilia mkasa huu kupitia mtandao huu)

No comments: