Saturday, June 29, 2013

MWENYEKITI WA KUONGOZA HALMASHAURI YA WILAYA YA MBINGA APATIKANA LEO


Baadhi ya Madiwani wa CCM wakibadilishana mawazo nje ya ukumbi wa chama hicho mjini hapa, mara baada ya kumaliza kazi ya kupiga kura ya kumchagua Mwenyekiti wao wa kuongoza halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.(Picha na Kassian Nyandindi)

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WANACHAMA wa chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, leo wamekamilisha adhima yao ya kuwachagua viongozi watakao waongoza katika nafasi ya Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, uchaguzi ambao awali kulikuwa na mvutano na utata mkubwa ambao ulisababisha hata kuzua vurugu za hapa na pale.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida amani na utulivu vilitawala, huku askari polisi nao wakionekana kuwa imara katika viwanja hivyo vya ukumbi wa CCM mjini hapa, ambako uchaguzi ulikuwa ukifanyika.

Ni tukio la pekee ambalo wapenzi na wafuasi wa chama hicho leo hii, walikuwa wakilisubiri kwa hamu, juu ya nani ambaye anaweza kushika nafasi hiyo muhimu hapa wilayani.

Mara baada ya uchaguzi huo kufanyika Katibu wa Chama hicho Anastasia Amasi, alitangaza matokeo mnamo majira ya 8:35 ambapo alisema nafasi ya Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga imechukuliwa na ndugu Allanus Ngahi ambaye alipata ushindi wa kura 29.


Aliyefuatia alipata kura 13 ambaye alikuwa ni Allan Mahay na wa mwisho alikuwa Nathaniel Challe aliyepata kura 3.

Kwa upande wa nafasi ya Makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo mshindi alikuwa ndugu Winfrid Kapinga, alipata kura 25 huku akifuatiwa na Prisca Haulle aliyepata kura 19.

Pamoja na mambo mengine hali ya uchaguzi ilikwenda vizuri huku Mbunge wa jimbo la Mbinga Mashariki Gaudence Kayombo, mara baada ya Katibu huyo kutangaza matokeo hayo, aliwataka wajumbe waendeleze mshikamano katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya wananchi wa Mbinga.

Shamra shamra za hapa na pale zilitawala leo katika viwanja vya  Chama cha Mapinduzi wilayani humo, huku makada mbalimbali wa chama hicho wakionekana kufurahi na kuimba nyimbo mbalimbali za chama na za kumtukuza Mungu.

Kwa ujumla majina matatu yaliyogombewa katika nafasi hizo, Diwani Allanus Ngahi anatoka kata ya Mpapa, Nathaniel Challe kata ya Matiri na Allan Mahay kata ya Maguu.

Kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Agness Mahangula Diwani viti maalum kata ya Mbuji, Prisca Haulle viti maalum kata ya Namswea na Winfrid Kapinga kata ya Ngima.

No comments: