Friday, June 14, 2013

MKUU WA WILAYA YA MBINGA AMSHUKIA KATIBU WA CWT, ASEMA NI KIKWAZO CHA MAENDELEO YA ELIMU WILAYANI HUMO

Upande wa kulia ni Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga akizungumza na wadau mbalimbali wilayani Mbinga hivi karibuni.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga amemshukia Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) tawi la Mbinga Samwel Mhaiki, akidai kwamba ni kikwazo cha maendeleo ya elimu wilayani humo, kutokana na katibu huyo kupenda kuendesha migogoro na kuchonganisha walimu mashuleni.

Ngaga alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake, juu ya maendeleo ya sekta ya elimu ya wilaya hiyo.

Alisema kuwa katibu huyo amekuwa kinara namba moja wa kupita mashuleni na kushinikiza walimu waache kufundisha (Wagome) hadi watakapolipwa madai yao, jambo ambalo alilieleza kuwa limekuwa likileta mgogoro usio na tija katika jamii.


Alieleza kwamba yeye na kamati yake ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Mbinga, walimwita Mhaiki na kuketi naye pamoja wakimtaka aache kuendeleza mgogoro huo na alikiri kutofanya hivyo lakini wanashangaa kumuona akiendelea.

“Mimi na kamati yangu ya ulinzi na usalama tulimwita katibu huyu wa CWT lakini amekuwa akitusumbua sana, anaandika barua na kuzisambaza mashuleni akishinikiza walimu wagome waache kufundisha, tulimwambia serikali inashughulikia madai ya hawa walimu na watalipwa,

“Akatuomba radhi na kusema hatarudia tena, malumbano haya anayoyaendeleza sasa ningelikuwa na uwezo mimi nikiwa Mkuu wa wilaya hii ningemhamisha, kwa sababu ni kikwazo kwa maendeleo ya elimu hapa wilayani, leo walimu wakigoma watoto wetu watafundishwa na nani”, alisema Ngaga.

Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga awali alisema wilaya yake hivi sasa imejipanga katika kukuza kiwango cha elimu kwa shule za msingi na sekondari, ambapo hivi sasa kwa kushirikiana na ofisa elimu wa wilaya hiyo Mathias Mkali wameanzisha utaratibu wa watoto wanaotarajia kumaliza darasa la saba hivi karibuni, wameweka vituo vya kujisomea (Makambi) kwa kila kata mashuleni wilayani humo wakati huu wa likizo ili waweze kujiandaa na mitihani yao ya kuhitimu elimu ya msingi.

Alisema wazazi wameitikia wito kwa kiasi kikubwa juu ya suala hilo na kukubaliana kutoa michango ya chakula, katika vituo hivyo ambavyo watoto wao wanasoma.

Pamoja na mambo mengine alisisitiza kuwa mtu yeyote atakayeonekana anakwamisha mikakati waliyojiwekea ya kukuza kiwango cha elimu wilayani Mbinga, yupo tayari kumwajibisha ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

No comments: