Monday, June 24, 2013

SOMA RATIBA YA OBAMA AKIWA TANZANIA


Dar es Salaam, 
Tanzania. 

IKULU ya Marekani na Idara ya Habari (Maelezo) Tanzania wametangaza rasmi ratiba ya Rais Barrack Obama atakapozuru Tanzania huku ikionyesha atakaa kwa siku mbili tu kuanzia Julai 1 na kuondoka Julai 2, mwaka huu.

Tanzania itakuwa nchi ya mwisho ya Afrika kutembelewa na Obama baada ya Senegal na Afrika Kusini. Atatua Senegal keshokutwa.

Mara atakapowasili Julai 1 na ndege yake kubwa ya Air Force One, Rais Obama atazindua barabara mpya katika upande wa mashariki wa geti la kuingia Ikulu.

Rais Obama, ambaye atafuatana mkewe Michelle pia siku hiyo ya Julai 1, pia atazungumza kwa nyakati tofauti na  kundi la wafanyabiashara kutoka nchi za Afrika na Marekani kwenye hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.


"Pia amepanga kuzungumza na maofisa wa Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania," ilisema taarifa ya Maelezo.

Baada ya shughuli hiyo, Rais Obama atahudhuria dhifa ya taifa atakayoandaliwa Ikulu jijini Dar es Salaam na mwenyeji wake Rais Jakaya Kikwete.

Siku inayofuata Rais Obama ataweka shada la maua kwenye sehemu ulipokuwa Ubalozi wa Marekani kama kumbukumbu ya watu waliofariki kufuatia shambulizi la kigaidi la bomu lililofanyikwa mwaka 1998.

Watu 11 walifariki na 85 kujeruhiwa kufuatia shambulizi hilo ambalo lilifanywa siku moja na Ubalozi wa Marekani nchini Kenya.

Rais Obama pia atatembelea mitambo ya kufua umeme ya Kampuni ya Symbion na atatoa hotuba akizungumzia mikakati ya Marekani ya kulisaidia bara la Afrika kuzalisha nishati ya umeme.

"Tanzania ni mshirika muhimu wa Marekani," anasema Ofisa wa Ikulu ya Marekani, Ben Rhodes wakati alipozungumza na waandishi wa habari wikiendi iliyopita kwenye Ikulu ya Marekani jijini Washington kuhusu ratiba ya ziara ya Obama barani Afrika.

"Tanzania ni washirika wetu katika masuala mbalimbali ya usalama kwenye ukanda wa Afrika Mashariki. Pia tunasaidia katika miradi mingi na tunaiona kama nchi yenye utawala bora," amesema Rhodes, ambaye pia ni msemaji wa Baraza la Usalama la Marekani.

Pia mke wa Obama atakuwa na ratiba yake, ambapo atapata staftahi na mwenyeji wake Mama Salma Kikwete, Julai 1 katika ofisi za Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (Wama) jijini Dar es Salaam.

Pia atatembelea sehemu ubalozi wa zamani wa Marekani na baadae atashuhudia onyesho la utamaduni la Kikundi cha Baba wa Watoto, ambacho kinajumuisha watoto wa mitaani wenye umri kuanzia miaka mitano hadi 18 kwenye Makumbusho ya Taifa.

Mama Obama amepangiwa Julai 2, kuhudhuria mkutano wake wa marais wa nchi za Afrika.

Laura Bush, ambaye ni mke wa Rais wa zamani wa Marekani, pia atahudhuria mkutano huo wenye lengo la kuunga mkono jitihada za kuwakomboa kiuchumi wanawake wa Afrika.




No comments: