Friday, June 28, 2013

UCHAGUZI WA NAFASI YA MWENYEKITI WA HALMASHAURI YA MBINGA KUFANYIKA KESHO

Christantus Mbunda, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mbinga.



















Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

UCHAGUZI wa nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma ambao uliahirishwa siku kadhaa zilizopita, sasa unatarajiwa kufanyika rasmi kesho Juni 29 Mwaka huu, katika ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliopo mjini hapa.

Kamati kuu ya chama hicho makao makuu ya taifa ilichukua jukumu la kuahirisha uchaguzi huo, kutokana na vuguvugu la kisiasa lililoshamiri mjini hapa ambalo linadaiwa kusababisha hata uchomaji moto wa ofisi ya Katibu wa CCM na kunusurika kuungua kabisa.

Vurugu hizo zinadaiwa kupinga ubabe uliokuwa umefanywa na kamati ya siasa ya mkoa huo,  ambayo inashutumiwa kukata jina la mgombea mmojawapo kimakosa kwa maslahi yao binafsi.

Ukataji wa jina hilo ambalo ni la Diwani Allanus Ngahi wa kata ya Kipapa, ulisababisha Wajumbe kugoma kufanya uchaguzi hadi watakapopata ukweli juu ya kwa nini jina hilo lilikatwa kimakosa au la.


Lakini baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya ndio Kamati kuu ya chama cha mapinduzi taifa ilichukua jukumu la kuahirisha uchaguzi huo, mpaka itakapoyafanyia kazi madai hayo ya madiwani waliogoma kufanya uchaguzi huo.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida ofisi ya Katibu huyo ilinusurika kuteketea kwa moto kufuatia watu wasiojulikana, kuichoma moto kwa kutumia mafuta aina ya petroli.

Ofisi hiyo ilichomwa madirisha na mlango mmoja huku ndani yake mapazia yaliyowekwa madirishani, yakiwa yameteketea kwa moto.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi Katibu wa CCM wa wilaya ya Mbinga Anastasia Amasi alisema, uchaguzi huo unafanyika kesho kutokana na Kamati kuu ya chama hicho kurejesha majina ya wagombea sita ambao waliomba kuwania nafasi hiyo.

Alisema nafasi ya Mwenyekiti inagombewa na majina matatu ambayo ni Allanus Ngahi kutoka kata ya Mpapa, Nathaniel Challe kata ya Matiri na Allan Mahay kata ya Maguu.

Kadhalika kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni Agness Mahangula Diwani viti maalum kata ya Mbuji, Prisca Haulle viti maalum kata ya Namswea na Winfrid Kapinga kata ya Ngima.

No comments: