Friday, June 28, 2013

UJUMBE WA OBAMA WAONYWA KUACHA LAPTOP HOTELINI NA KULA KACHUMBARI

Rais Obama.


Dar es Salaam, 
Tanzania. 
LICHA ya ujumbe wa Rais wa Marekani, Barrack Obama kutarajiwa kufikia katika hoteli kubwa zenye hadhi wakati kiongozi huyo atakapowasili nchini Julai Mosi mwaka huu, Ikulu ya Marekani imetoa tahadhari ya vyakula ambavyo hawatakiwi kuvigusa wakiwa nchini ikiwa ni pamoja na kutumia maji ya bomba.

Kwa mujibu wa taarifa ya maelekezo ya Ikulu ya Marekani, watu watakaokuwa kwenye msafara wa Obama wametakiwa kutotumia kachumbari. Pia imewataka kutumia maji ya chupa zaidi.


“Kutokana na mfumo wa maji uliopo, tunashauri watu wetu kutumia maji ya chupa zaidi kwa kunywa na hata kwa kupiga mswaki,” imesema taarifa hiyo.

Kwa kuelewa fika tatizo la ugonjwa wa malaria nchini, ujumbe wa Obama umeshauriwa kutumia dawa ya mbu ya kupaka na kupuliza inayoitwa Deet.

Deet ni dawa maarufu huko Marekani na ikiwa katika aina tofauti ikiwamo ya kupaka na kupuliza na imekuwa ikitumiwa na Jeshi la Marekani kwenye vita mbalimbali tangu miaka ya 1940 kabla ya kuanza kutumiwa na raia mwaka 1957.

Maelekezo katika ATM

Pia watu watakaokuwa kwenye msafara wa Rais Obama wametakiwa kuhakikisha wanatumia mashine za kutolea fedha (ATM) zilizoko karibu na hoteli watakazofikia.

“Kuna tatizo la uhalifu kwa hiyo siyo vizuri kutumia ATM ambazo ziko katika sehemu zisizo salama. Pia katika kipindi watakachokuwa Tanzania watu wanapaswa kutumia teksi ambazo zimeidhinishwa na hoteli.

“Pia siyo vizuri kuacha kompyuta ya fedha kwenye vyumba mtakavyolala. Pia kina mama wanapaswa kuchukua tahadhari ya mabegi yao watakapokuwa wanapita mitaani,” ilitahadharisha taarifa hiyo.

No comments: