Tuesday, October 29, 2013

KERO YA UPATIKANAJI WA MAJI MJI WA SONGEA YAZIDI KUKERA WANANCHI

Mji wa Songea.























Na Muhidin Amri,
Songea.


WAKAZI wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wametakiwa kutumia maji kwa uangalifu kutokana na huduma hiyo kutolewa kwa mgao ambao unasababishwa na  ukosefu wa umeme wa uhakika katika Manispaa  hiyo, kutokana na mashine za kusukuma maji kwenda kwenye makazi ya watu kushindwa kufanya  kazi yake ipasavyo.


Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni, na afisa uhusiano wa Mamlaka ya maji safi na mazingira (SOUWASA) Neema  Chacha, alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Songea.


Chacha alisema kufuatia tatizo  la umeme unaotolewa kwa mgao mjini Songea, mamlaka hiyo  hulazimika kutoa maji  kwa mgao pele umeme unapowaka na wao ndipo waweze kuwasha mashine zao.

UKOMBOZI SACCOS JIMBO LA SONGEA YAJIVUNIA MAFANIKIO YAKE

Rais Jakaya Kikwete.























Na Dustan Ndunguru,
Songea.

CHAMA cha akiba na mikopo cha Ukombozi Jimbo la Songea (SACCOS) kilichopo katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, kimekopesha wanachama wake shilingi bilioni 2.2 katika kipindi cha miaka saba tangu kuanzishwa kwake.


Meneja wa SACCOS hiyo Rainer Ngatunga alisema kuwa fedha hizo zilizokopeshwa ni kutokana na akiba za wanachama, na sasa chama kina wanachama 1104.


Ngatunga alisema kuwa kati ya fedha hizo shilingi bilioni 1.6 zimekwisha rejeshwa huku akiwataka wanachama wake, watumie fedha wanazokopeshwa kwa malengo yaliyokusudiwa sambamba na kujenga tabia ya kurejesha mikopo wanayokopa kwa wakati.  

WAZAZI NA WALEZI WATAKIWA KUFUATILIA MIENENDO YA WATOTO KWA KUHAKIKISHA WANAZINGATIA MASOMO

Waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi, Shukuru Kawambwa.


























Na Dustan Ndunguru,
Songea.

SERIKALI mkoani Ruvuma imewataka  wazazi na walezi kuhakikisha wanafuatilia kwa ukaribu mienendo ya watoto wao, ili wasijiingize katika vitendo viovu ambavyo vinawafanya washindwe kuendelea na masomo yao.


Mkuu wa mkoa huo Said Mwambungu alisema baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa na kawaida ya kutofuatilia watoto wao, jambo ambalo halipaswi kuendelea kuvumiliwa, kutokana na ukweli kuwa madhara yake ni makubwa pale wanapojiingiza katika matendo yasiyokubalika mbele ya jamii.


Mwambungu alisema alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi, huku akisisitiza kila mtoto anayefikisha umri wa kuanza shule anapaswa kuandikishwa na awapo shuleni maendeleo yake yanapaswa kufuatiliwa kwa ukaribu, kwa ushirikiano kati ya walimu na wazazi au walezi.


Alisema walio wengi wanadhani kwamba mwalimu pekee ndiye mwenye jukumu la kufuatilia maendeleo ya mwanafunzi,  wakati inafahamika wazi kuwa yeye anakuwa nao tu pindi wawapo shuleni lakini mara wakishatoka na kwenda majumbani kwao, wazazi ndio wanapaswa kubeba jukumu hilo.

KITUO CHA AFYA MCHOTEKA KINA HALI MBAYA, WANANCHI WAIOMBA SERIKALI KUNUSURU HALI HIYO

MKuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.



















Na Dustan Ndunguru,
Songea.


KITUO cha afya cha Mchoteka kilichopo katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma kinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo upungufu  wa watumishi, majengo na ukosefu wa  dawa na vifaa tiba huku wagonjwa wanaofika katika kituo hulazimika kutafuta huduma hiyo kwenye hospitali za misheni kwa gharama kubwa.


Mganga mkuu wa kituo hicho Dokta Tigrida Sanga alisema kituo hicho kinahudumia  wananchi wa kutoka  tarafa mbili ya Nalasi kwa wilaya ya Tunduru na Sasawala, na kwa upande wa wilaya ya Namtumbo na nchi jirani ya Msumbiji kutoka jimbo la Nampura.


Kituo hicho  kinatoa huduma ya chanjo kwa wajawazito na watoto, upimaji wa virusi vya UKIMWI na UKIMWI kwa wajawazito na kutoa elimu ya uzazi wa mpango, lakini wamekuwa wakikwama kutoa huduma hizo kutokana na kukabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo pia upungufu wa watumishi, majengo na vifaa tiba.


Alisema kwa sasa kituo kina watumishi wa sekta zote wapatao  saba kati ya 23 wanaohitajika, nyumba za watumishi zilizopo tatu kati ya 27, hakuna  jengo la maabara, hakuna jengo la upasuaji, jengo la ushauri nasaha na hawana  gari la kubeba wagonjwa, huku akidai hali hiyo inasababisha  watumishi wa kituo hicho  kufanyakazi katika mazingira mgumu.

UWT YAWATAKA WAZAWA WA NYASA KURUDI NYASA NA KWENDA KUWEKEZA

Ziwa Nyasa.


















Na Dustan Ndunguru,
Nyasa.


JUMUIYA ya Umoja wa wanawake Tanzania(UWT) wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma  imeanza kutoa elimu ya  ujasiriamali kwa wanawake,  ambapo imewataka  waunde vikundi ambavyo vitawasaidia kuwainua kiuchumi na kuwaongezea pato katika familia zao.


Mwenyekiti wa jumuiya hiyo wilayani humo Grace Millinga alisema wamechukua hatua hiyo ya kupita kuhamasisha wanawake wenzao kwa kuwapatia elimu ya ujasiliamali, ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya chama cha Mapinduzi  ya mwaka 2010 baada ya kubaini wanawake wa wilaya hiyo bado wanaishi maisha duni tofauti na wenzao wa wilaya nyingine mkoani humo.


Alisema pamoja na kuwapatia elimu ya ujasiriamali bado wamekuwa wakiwataka kuunda vikundi na kubuni miradi ambayo itawasaidia kuwapatia soko la uhakika, kwa kuuzia bidhaa zao na kuwa na akaunti benki kabla ya kusajili na kutambulika kisheria kama moja ya njia rahisi ya kuweza kukopa fedha, kwenye taasisi za kifedha.


Alisema kazi hiyo wameanza kwa kuifanya kwa kuanzia kwenye vijiji vya mwambao wa ziwa Nyasa, na wamebaini  wengi wao wamekosa elimu ya ujasiriamali ambapo hujikuta wakijiingiza  kwenye vitendo viovu vya uasherati  kwa lengo la kujipatia fedha, huku wakikabiliwa na uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa.

MFANYABIASHARA MWENYE ASILI YA KIARABU APANDISHWA KIZIMBANI KATIKA MAHAKAMA YA WILAYA YA MBINGA KWA KOSA LA KUTUNZA SILAHA KWA UZEMBE

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman.


























Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MFANYABIASHARA mmoja ambaye ni raia mwenye asili ya kiarabu amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, kwa kosa la kutunza silaha kwa uzembe kitendo ambacho ni hatari katika jamii.

Kwa mujibu wa Mwendesha mashataka wa polisi Inspekta Mwamba alimtaja raia huyo kuwa ni Karama Abdallah Karama (37) ambaye anaishi Mbinga mjini, alitenda kosa hilo Oktoba 10 mwaka huu majira ya saa 5:30 asubuhi.

Mwendesha mashataka huyo alidai mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama wilaya hiyo Geofrey Mhini kuwa, silaha hiyo ni Pisto aina ya Bereta yenye namba za usajili H 30436Y.

Alisema  raia huyo alikamatwa na maofisa wa Jeshi (JWTZ) ambao walikuwa kwenye oparesheni “Okoa Maliasili”, ambapo walipobaini uzembe huo walimuamuru mfanyabiashara huyo aitoe silaha ambayo ilikutwa ikiwa imehifadhiwa katika eneo la kituo cha mafuta cha Oil Com kilichopo mjini hapa, ikiwa katika mazingira ya hatari.

Maofisa hao wa Jeshi wakati huo walikuwa wakimfanyia upekuzi Bw. Karama, baada ya kuihisiwa anafanya biashara ya kusafirisha Nyara za serikali pasipo kibali maalum ndipo walipobaini kuwepo na tatizo la uzembe wa utunzaji wa silaha, ambayo anaimiliki kisheria.

Monday, October 28, 2013

MKUU WA WILAYA YA TUNDURU APONGEZWA KWA UAMUZI WAKE WA KUINGIA DARASANI KUSHIKA CHAKI NA KUFUNDISHA


Na Steven Augustino,
Tunduru.

UMOJA  wa  Vyama vya Walimu Tanzania (CWT) Kanda ya kusini inayoihusisha mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi(UWARUMLI) umempongeza Mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho kwa uamuzi wake wa kushika chaki na kufundisha somo la Hisabati, katika shule ya sekondari  ya Mataka wilayani humo.

Pongezi hizo zilizotolewa kwenye kikao chao kilichofanyika katika ukumbi wa Klasta ya walimu mlingoti mjini Tunduru.
 
Mwenyekiti wa Mkutano huo wa CWT, mkoa wa Lindi  Mwalimu Mlami Seba  ndiye alitanguliza pongezi hizo wakati akifungua mkutano huo kwa wajumbe wa Umoja huo kanda ya Kusini ambao walikuja kuhudhuria ambapo alisema huo ni mfano wa kuigwa na ni moyo wa pekee.

Seba aliendelea kufafanua kuwa Nalicho anapaswa kutolewa mfano kutokana na  upendo aliouoonyesha kwani  wapo viongozi wengi  ambao baada ya kuchaguliwa ama kuteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali, huacha kuzifanyia kazi taaluma walizonazo ambazo wamezisomea  kwa madai ya kuwa na kazi nyingi za Kitaifa.

Saturday, October 26, 2013

HALMASHAURI YA WILAYA YA MBINGA LAWAMANI KWA KUTELEKEZA BUSTANI MAMA ZA KUZALISHIA MICHE YA KAHAWA, MENEJA ASEMA TATIZO HILO LIKIENDELEA KUFUMBIWA MACHO UCHUMI WA WILAYA HIYO HUENDA UKADOROLA

Meneja wa Kanda ya Kusini Godbless Shao, alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya Bustani mama za kuzalishia miche ya kahawa zilivyotelekezwa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma. (Picha na Kassian Nyandindi)




Na Kassian Nyandindi,
Songea.

BUSTANI Mama za kuzalishia miche ya kahawa, wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma zipo katika hali mbaya na huenda uzalishaji wa miche hiyo ukashindwa kuendelea, kutokana na Halmashauri ya wilaya hiyo kuzitelekeza bustani hizo kwa kutosimamia na kufuata taratibu husika.

Sambamba na hilo uongozi husika wa wilaya hiyo umeshushiwa shutuma nzito juu ya uzembe huo, kwa kile kilichoelezwa kuwa licha ya Taasisi ya Utafiti wa zao la Kahawa Tanzania (TaCRI) – Ugano Kanda ya kusini, kutoa ushauri wa mara kwa mara juu ya kuendeleza bustani hizo hali ambayo hivi sasa imekuwa tete na hakuna utekelezaji unaofanyika.

Meneja wa Kanda ya Kusini Godbless Shao, alisema hayo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari mjini hapa ambapo alitahadharisha kuwa, endapo suala hilo litaendelea kupuuzwa huenda uchumi wa wilaya ya Mbinga ukashuka kwa kasi, kutokana na tegemeo kubwa la kukua kwa uchumi wilayani humo hutegemea zao la kahawa.

Shao alieleza kuwa bustani hizo ambazo zilianzishwa na TaCRI baadaye kukabidhiwa halmashauri hiyo kwa ajili ya kusimamia na kuendeleza uzalishaji wa miche ya kahawa, hivi sasa zinaelekea kufa kutokana na kuwepo usimamizi duni wa wataalamu husika.

Saturday, October 19, 2013

WAZIRI MKUU AOMBWA KUIOKOA NFRA, NI BAADA YA KUDAIWA KUISHIWA FEDHA ZA KUNUNULIA MAHINDI

Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

 

 

 

 

 

 

 

 


Na Mwandishi Wetu,
Makambako.

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, ameombwa na wakulima wa mahindi katika mikoa ya Iringa, Ruvuma na Njombe, kuisaidia Wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), kupata fedha za kuendelea kununua mahindi kwenye vituo vyake.

Wakulima hao wamedai kufikia hatua hiyo, baada ya kutangaziwa na NFRA kusitishwa kwa zoezi lililokuwa likiendelea kwa miezi miwili sasa ya kununua mahindi kutoka kwao, huku wakiishauri ofisi yake kuangalia uwezekano wa kumsaidia mkulima.

Wakizungumza na gazeti hili, wakulima wao wamedai kusikitishwa na uamuzi huo na kudai kuwa unaweza kuathiri mfumo wa kilimo kwa vile wao waliamini ushawishi wa serikali katika kuhimiza vijana kuingia katika sekta hiyo.

Wakulima hao wamedai kuwa wanaimani na ofisi ya Waziri Mkuu Pinda pekee, kuweza kuwasaidia kwa kuchukua uamuzi mgumu wa kuipatia NFRA fedha za kununua kiasi cha tani 200,000 zilizobaki kwa wakulima.

Friday, October 18, 2013

UHARIBIFU WA VYANZO VYA MAJI KATIKA MJI WA MBINGA, TISHIO LA KUKAUKA VYANZO VYA MAJI SERIKALI YATAKIWA KUCHUKUA HATUA MAPEMA

Mwenyekiti wa kitongoji cha Mbuyula Issack Nduguru akichangia hoja katika kikao cha baraza la Mamlaka ya mji mdogo wa Mbinga mkoani Ruvuma, ambapo alikemea uharibifu wa vyanzo vya maji unaofanywa katika mji huo na kuitaka serikali kuchukua hatua za haraka kunusuru hali hiyo isiweze kuendelea.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya mji mdogo wa Mbinga Oscar Yapesa akisikiliza kwa makini hoja mbalimbali zilizokuwa zikitolewa na wajumbe katika kikao hicho, katikati ni Mwenyekiti wa Mamlaka hiyo Steven Matteso na upande wa kulia ni Diwani wa kata ya Mbinga mjini Kelvin Mapunda.

Baadhi ya Wenyeviti wa vitongoji vya Mamlaka ya mji mdogo wa Mbinga wakifuatilia kwa makini hoja mbalimbali katika kikao chao kilichoketi ukumbi wa jumba lka maendeleo mjini hapa. (Picha zote na Gwiji la matukio mkoani Ruvuma)

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa vitendo vya uharibifu wa vyanzo vya maji katika eneo la Mamlaka ya mji mdogo wa Mbinga mkoani Ruvuma, endapo havitadhibitiwa mapema huenda vikashindwa kuendelea kutoa maji, kutokana na wakazi wa mji huo kuendesha shughuli za kilimo katika vyanzo hivyo.

Aidha uharibifu huo unatokana na wakazi hao kukata miti iliyorafiki ya maji ambayo ipo kwenye vyanzo, jambo ambalo nalo linahatarisha kutoweka kwa uoto wa asili.

Hayo yamejitokeza katika kikao cha Baraza la Mamlaka la mji huo, kilichoketi kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa, ambapo wajumbe wa baraza hilo walilalamikia hali hiyo na kuutaka uongozi wa wilaya kuchukua hatua mapema kabla ya tatizo kuwa kubwa.

“Hili suala inabidi tuliangalie kwa kina zaidi hapa wataalamu wanaosimamia mazingira tunao hatuelewi wanafanya nini, tufute mambo ya siasa turudishe uoto wa asili katika vyanzo vyetu ili tuweze kuepukana na tatizo linaloweza kutokea hapo baadaye”, alisema Issack Ndunguru Mwenyekiti wa kitongoji cha Mbuyula.