Friday, January 8, 2016

BENKI YA POSTA YAJIVUNIA MAFANIKIO YAKE

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifungua tawi la benki ya Posta Songea mkoani Ruvuma.

Na Kassian Nyandindi,
Songea.

TATIZO la kutokuwa na wafanyakazi wabunifu katika Benki ya Posta Tanzania, imeelezwa kuwa ni moja kati ya changamoto ambayo ilichangia kudorola kiuchumi na kuifanya benki hiyo, ishindwe kusonga mbele kimaendeleo katika kuwahudumia wateja wake.

Aidha imefafanuliwa kuwa baada ya kubaini tatizo hilo, benki hiyo imeunda utaratibu mwingine mpya ambao hivi sasa kasi yake ni kubwa ya uendeshaji wa huduma za kibenki, na kufanikiwa kutengeneza faida ya shilingi bilioni 10.3 katika miaka mitatu iliyopita.

Sabasaba Mushinge ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa benki ya Posta hapa nchini, alisema hayo juzi katika hafla fupi ya uzinduzi wa tawi jipya la benki ya Posta Songea mkoani Ruvuma, ambayo ilizinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.

Mushinge aalisema kuwa wameweza kufikia asilimia 70 ya ukarabati wa matawi yote yaliyopo hapa nchini, na kwamba mafanikio hayo yametokana na mabadiliko ya kiuongozi baada ya benki kwa muda mrefu kudorola kiuchumi.

Alisema hivi sasa wanavikundi 30,000 vya wajasiriamali ambao wamejiunga na benki wamepewa mikopo, ambayo huendesha shughuli zao mbalimbali za kimaendeleo katika familia zao.

Vilevile hutoa huduma ya mikopo kwa wastaafu, ambapo jumla ya wastaafu 21,000 hapa nchini wamepewa mkopo wa shilingi bilioni 41 na kwamba wateja wake wameunganishwa na mfumo wa Sim banking, ambao hutoa huduma popote pale walipo.
“Tumeweza pia kutumia shilingi milioni 150 kwa ajili ya kutoa misaada ya ujenzi wa madarasa ya kusomea wanafunzi katika maeneo mbalimbali hapa Tanzania na utengenezaji wa madawati ya kukalia watoto hawa, ombi langu nawaomba watanzania wenzangu watumie huduma za kifedha katika benki yetu ili waweze kuondokana na umaskini”, alisema Mushinge.
Kwa upande wake Waziri Mkuu, Majaliwa alipongeza jitihada zinazofanywa na benki hiyo ya Posta hasa kwa kukuza mtaji wake wa ndani na kuboresha matawi yake huku akisisitiza kwa kuwataka watendaji wake, kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili banke hiyo iweze kusonga mbele.
“Wanaruvuma hii ni bahati kubwa kwenu, ni lazima sasa tuonyeshe kwamba tunahitaji maendeleo makubwa kutoka katika benki hii, ili hawa Posta waweze kufungua matawi mengi katika mkoa wetu”, alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Pamoja na mambo mengine, Waziri Mkuu Majaliwa aliutaka uongozi wa benki ya Posta kuhakikisha kwamba inafungua milango kwa kutumia matangazo ili elimu husika iweze kuwafikia wananchi kwa wakati, na kusisitiza kuwa kutembea na fedha mifukoni kumepitwa na wakati hivyo Watanzania wanapaswa kubadilika kwa kuwa na mazoea ya kuweka fedha benki.

No comments: