Wednesday, January 6, 2016

WAZIRI MKUU MAJALIWA AITAKA NFRA KUPELEKA MAGUNIA KWA WAKULIMA VIJIJINI



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

WAZIRI Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa, ameutaka uongozi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) hapa nchini, kuhakikisha kwamba wanajipanga kikamilifu katika kuhakikisha kwamba wakulima wa zao la mahindi wanapatiwa magunia ya kuhifadhia zao hilo, katika maeneo ambayo yametengwa huko vijijini msimu ujao wa mavuno ya mazao ya chakula.

Agizo hilo amelitoa leo katika ziara yake ya siku tatu ya kutembelea na kuona maendeleo ya sekta mbalimbali mkoani Ruvuma, na kuhakikisha kwamba anatekeleza agizo la Rais John Magufuli linalosema hakuna Mtanzania atakayekufa njaa.

Alieleza kwamba, wafanyabiashara ambao wamekuwa wakipatiwa magunia na NFRA kwa ajili ya kununulia mahindi na wakulima wanapojaribu kutafuta namna ya kuyapata magunia hayo, imekuwa ni tatizo kwao kuyapata kwa urahisi.


Vilevile Waziri Mkuu, Majaliwa alionesha kusikitishwa na vitendo hivyo vinavyofanywa na wafanyabiashara wajanja, ambao wamekuwa wakipita vijijini kuwarubuni wakulima na kununua mahindi kwa bei ndogo ambayo hailingani na uzalishaji wa zao hilo.

Alisema kuwa kumekuwa na mianya ya rushwa inayofanywa na wafanyabiashara hao kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa Wakala huyo, kwa lengo la kujinufaisha watu wachache huku mkulima wa kawaida akiendelea kuteseka na mazao yake shambani, jambo ambalo hivi sasa limekuwa ni kero kubwa hasa katika maeneo ambayo mazao ya chakula huzalishwa kwa wingi.

“Magunia yanayonunuliwa na serikali kwa ajili ya kuhifadhia zao hili, ninazo taarifa za kutosha kwamba hayamfikii mkulima kule kijijini, badala yake yanaishia kwa watu wachache”, alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Vilevile alieleza kuwa serikali inawajibu wa kuhifadhi chakula katika mazingira yanayokubalika ili kisiweze kuharibiwa na wadudu waharibifu wa mazao, hivyo ameitaka Wakala wa hifadhi ya taifa ya chakula kanda ya Songea kuhakikisha kwamba mahindi yaliyohifadhiwa chini ya ardhi yanatafutiwa sehemu nyingine ya kuhifadhia ili yasiharibike.

Alifafanua kuwa uhifadhi wa nje wa zao hilo, usalama wake ni mdogo kwa asilimia 75 tu na kwamba mlundikano huo wa magunia yaliyosheheni mahindi katika hifadhi hiyo ya chakula unasababishwa na hifadhi kuwa na upungufu mkubwa wa maghala. 

Pamoja na mambo mengine, Waziri Mkuu Majaliwa alihoji juu ya msongamano wa magari aina ya malori yaliyopo kando kando ya barabara ya kutoka Songea kwenda Mbinga, huku akieleza kuwa hali hiyo imekuwa ikileta malalamiko mengi kutoka kwa wasafirishaji kuwa magari yanayoingia NFRA kupakia mahindi, huwapatia watu wanaojulikana kwanza, ndipo huruhusu wengine kitendo ambacho kinaonyesha kuwa kuna upendeleo.

“Utaratibu unaotumika kuingiza malori hapa kwenu una malalamiko mengi, taarifa nilizonazo huingiza kwanza mtu anayejulikana, jambo hili likiendelea linaweza kuleta mtafaruku au matatizo yasiyokuwa ya lazima, nahitaji tatizo hili liwe mwisho na zingatieni haki na kupanga utaratibu mzuri”, alisisitiza.

Awali Mbunge wa Jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma, Leonidas Gama alisema kuwa tatizo la soko la mahindi katika mkoa huo ni kubwa hivyo ameiomba serikali ya awamu ya tano, iangalie namna ya kutafuta masoko ili wakulima wadogo waweze kupata fursa ya kuuza mazao yao.

Gama alisisitiza kuwa ni vyema serikali irejeshe utaratibu wa awali, wa NFRA kununua mahindi vijijini kwa wakulima na kuachana na mfumo wa kuwatumia mawakala ambao hupita huko na kumkandamiza mkulima, kwa kununua mazao yao kwa bei ndogo.

No comments: