Friday, January 22, 2016

UJENZI KIWANDA CHA KUSAGA NAFAKA PERAMIHO KUPUNGUZA UKOSEFU WA SOKO LA MAHINDI



Na Julius Konala,
Songea.

IMEELEZWA kuwa ujenzi wa Kiwanda cha kusaga nafaka katika mtaa wa Namiholo kata ya Peramiho wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, utagharimu zaidi ya shilingi milioni 300 hadi kukamilika kwake na kusaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa soko la kuuzia mahindi, kwa wakulima wa vijiji vinavyozunguka eneo la mradi huo.

Hayo yalisemwa na msimamizi wa mradi huo, Fredrick Lunje alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu mara baada ya kutembelea eneo la mradi kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali za ujenzi, ambazo zinaendelea katika mji huo mdogo wa Peramiho.

Lunje alisema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho upo katika hatua za mwisho, kwa madai kwamba vifaa vyote vya ujenzi vimekamilika  na kwamba kinachosubiriwa ni  mafundi wa kufunga mashine hiyo kutoka Afrika ya kusini, ili ifikapo mwezi Mei mwaka huu kianze kufanya kazi.


Alisema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa kiwanda hicho, pia kutasaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana linaloikabili serikali pamoja na kuchangia pato la taifa kwa kulipa kodi, itakayoelekezwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kiwanda hicho kitakuwa kinatoa huduma ya kusaga sembe aina mbili, ikiwemo  yenye kiini na isiyokuwa na kiini ambapo wanatarajia kusambaza ndani na nje ya mkoa wa Ruvuma, huku akiongeza kuwa mashine hiyo ikifungwa itakuwa na uwezo wa kusaga gunia kumi kwa saa moja.

Aidha ameiomba serikali kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wazawa, hasa katika suala la kusaidia kupata mikopo ya fedha, kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao badala ya kuwathamini wawekezaji wa nje peke yake.

Kwa upande wao baadhi ya wakulima wa vijiji vya Peramiho, wamempongeza mwekezaji huyo kwa jitihada zake za kuanzisha mradi huo ambapo walieleza kuwa utakuwa ni mkombozi mkubwa kwao, kwa kuwatatulia tatizo la ukosefu wa soko la kuuzia mahindi yao lililokuwa likiwakabili kwa muda mrefu.

No comments: