Friday, January 22, 2016

ULIPUAJI MIAMBA MGODI WA MAKAA YA MAWE NGAKA WAATHIRI WANAFUNZI



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WANAFUNZI wanaosoma shule ya msingi Ntunduaro iliyopo katika kata Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, majengo wanayotumia kusomea yapo katika hali mbaya na huenda yakabomoka wakati wowote kutokana na kujenga nyufa zinazosababishwa na mtetemeko mkubwa wa ulipuaji wa miamba, kwenye mgodi wa makaa ya mawe Ngaka uliopo katika kijiji hicho.

Hali ya mazingira ya shule hiyo hivi sasa ni mbaya na kwamba husababishwa na kuendelea kwa shughuli hizo za ulipuaji wa baruti katika miamba, jambo ambalo huenda likaleta madhara makubwa katika jamii.

Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga alisema hayo alipokuwa kwenye kikao maalumu, katika kata ya Ruanda na uongozi wa kampuni ya Tancoal Energy ambao ndio wamiliki wa mgodi huo, wakiwemo na baadhi ya wananchi wa kata hiyo wakijadili juu ya athari mbalimbali zitokanazo na mgodi huo.


Ngaga alisema kuwa ulipuaji wa baruti unaofanywa na kampuni hiyo unahatarisha usalama wa wananchi wanaoishi jirani na mgodi, hivyo kuna kila sababu ya kuchukua jitihada ya kunusuru hali hiyo ikiwemo kufanya taratibu za kuwahamisha kwenda maeneo mengine ili wasiweze kuathirika.

“Ulipuaji huu unafanywa kwa kishindo kikubwa kiasi ambacho hata majengo ya shule hii na baadhi ya nyumba za wananchi, hutikisika na kujenga nyufa ambazo baada ya miezi michache mbele endapo hali hii itaendelea kufanyika huenda zikabomoka”, alisema Ngaga.

Awali akichangia hoja katika kikao hicho, Diwani wa kata ya Ruanda Edimund Nditi alisema kuwa watoto wanaosoma katika shule hiyo ya msingi wakati ulipuaji huo unapofanyika, hulazimika kukatisha masomo yao darasani na hukimbia kutoka nje ya madarasa yao wakihofia majengo wanayotumia kusomea huenda yakabomoka kutokana na kuwa katika hali mbaya.

Alisema kuwa athari za mazingira hata kwa walimu wanaofundisha katika shule hiyo ni kubwa, na kwamba serikali inapaswa kuingilia kati ili kuweza kunusuru hali hiyo.

“Mheshimiwa Mkuu wa wilaya, suala la kuwahamisha hawa wananchi ni muhimu lifanyike ili kuweza kunusuru makazi na maisha ya watu wanaoishi katika kijiji hiki, athari za mazingira zitokanazo na shughuli zinazofanywa na mgodi ni kubwa mno”, alisema Nditi.

John Nyimbo Mwenyekiti wa kijiji cha Ntunduaro alisema kuwa uwekezaji unaofanywa na kampuni hiyo, hauna tija katika jamii kutokana na hali ya ulipuaji wa miamba unaofanywa huathiri makazi ya watu.

Naye Kamishina msaidizi wa madini kanda ya ziwa Nyasa mkoani Ruvuma, Fredy Mahobe alithibitisha juu ya milipuko hiyo na kueleza kuwa inatokana na uwingi wa baruti zinazoingizwa kwenye miamba mgodini na kulipuliwa.

Mahobe alifafanua kuwa Tancoal Energy hutumia kiasi cha tani mbili za ulipuaji, ambacho ni kikubwa na huathiri mazingira ya maisha ya wananchi wanaozunguka mgodi huo.

Kamishina huyo alieleza kwamba hali hiyo husababisha mtetemeko kuwa mkubwa na kuwafanya wananchi waishi kwa hofu, kutokana na nyumba zao kujengwa chini ya kiwango wakihofia kubomoka.

Aidha kikao hicho kimefanyika kufuatia agizo lililotolewa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipokuwa katika ziara yake ya kikazi Januari 12 mwaka huu hapa mkoani Ruvuma, alipotembelea mgodi huo na kujionea changamoto mbalimbali. 

Profesa Muhongo aliagiza kwa kumtaka Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Ngaga akae na uongozi kampuni hiyo inayozalisha makaa ya mawe katika mgodi wa Ngaka wakiwemo baadhi ya wananchi na uongozi wa kata hiyo, ili waweze kujadili changamoto zilizopo mbele yao na kuzifikisha ngazi ya juu serikalini ili ziweze kufanyiwa kazi.

No comments: