Thursday, January 14, 2016

WAZIRI MUHONGO AYATAKA MAKAMPUNI KUTUMIA MAKAA YA MAWE YANAYOZALISHWA HAPA NCHINI



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MAKAMPUNI yanayotumia makaa ya mawe kufua umeme ambao huendesha viwanda vyao kwa ajili ya kuzalisha bidhaa mbalimbali hapa Tanzania, yametakiwa kutumia makaa yanayozalishwa hapa nchini na sio kuagiza nchi za nje.

Waziri wa Wizara ya nishati na madini, Profesa Sospeter Muhongo alitoa agizo hilo jana alipokuwa ametembelea mgodi wa makaa ya mawe Ngaka uliopo katika kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda, katika ziara yake ya siku moja wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma.

Profesa Muhongo alifafanua kuwa makampuni hayo yanafanya hivyo kwa lengo la kukwepa kulipa ushuru wa ndani, kwa sababu mkaa unaotoka nje ya nchi wamekuwa hawalipi ushuru au kodi ya aina yoyote ile.

“Tunataka makampuni yanayotumia makaa ya mawe hapa kwetu yatumie mkaa unaozalishwa hapa nyumbani, malighafi hii tunazalisha kwa wingi na yana ubora unaokubalika, kwa nini wasitumie mkaa wa kwetu”?, alihoji Profesa Muhongo.


Kufuatia kuwepo kwa hali hiyo, Profesa Muhongo aliagiza Wizara yake ifikapo Januari 14 mwaka huu majira ya asubuhi, atafanya kikao na baadhi ya makampuni yanayotumia makaa ya mawe ambayo waliingia mkataba wa kutumia mkaa unaozalishwa hapa nchini, ili waweze kutoa ufafanuzi kwa nini wanaagiza nje ya nchi na kuacha kutumia ya hapa nyumbani.

Alisema kuwa lengo la kufanya mkutano huo ni kujenga makubaliano ambayo yatafikia muafaka wa kutumia mkaa unaozalishwa hapa kwetu, na sio kama ilivyo sasa makampuni hayo hufanya hivyo kwa lengo la kukwepa kulipa ushuru au kodi.

Pamoja na mambo mengine, Waziri Muhongo aliuagiza uongozi wa mgodi wa makaa ya mawe Ngaka uliopo wilayani Mbinga uhakikishe unashirikiana kwa karibu na wananchi wanaozunguka mgodi huo, ili kuweza kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya lazima.

Alisisitiza pia suala la ulipaji wa fidia kwa baadhi ya wananchi ambao waliondolewa katika eneo la mgodi, lifanyiwe kazi haraka na wahusika wapewe haki zao wanazostahili kupata.

Naye Mkuu wa wilaya hiyo, Senyi Ngaga alipotakiwa kutoa ufafanuzi juu ya matatizo yaliyopo katika mgodi huo alimweleza Profesa Muhongo kuwa, tayari hatua husika za upembuzi yakinifu juu ya madai ya wananchi hao zimeanza kutekelezwa kwa kushirikiana na kampuni ya TANCOAL Energy, ambao ni wamiliki wa mgodi huo wanaopaswa kulipa fidia wananchi hao.

Ngaga alisema kuwa tayari wananchi 400 walikwisha lipwa fidia zao kabla ya mradi huo kuanza kufanya kazi na kwamba, waliobakia sasa baada ya kufanya tathimini ya pili juu ya malipo yao ni watu 350 ambao nao wanatarajia kulipwa wakati wowote kuanzia sasa.

Mradi huo wa makaa ya mawe unamilikiwa na kampuni ya ubia ya TANCOAL Energy, ambayo asilimia 30 ya hisa zake zinamilikiwa na serikali kupitia shirika la maendeleo la Taifa la NDC na asilimia 70 ya hisa zinamilikiwa na mwekezaji wa kampuni ya Intra Energy.

No comments: