Friday, January 15, 2016

WAZIRI WA AFYA ASIKITISHWA NA WANAWAKE KUTUPA WATOTO

Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, wazee na watoto Ummy Mwalimu kushoto, akimjulia hali  mkazi wa mtaa wa Mshangano Manispaa ya Songea Cosma Mvulla (65) aliyekuwa katika zamu ya kusubiri kuonana na madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo katika hospitali ya mkoa wa Ruvuma.


Na Muhidin Amri,
Songea.

WAZIRI wa afya, maendeleo ya jamii, wazee na watoto Ummy Mwalimu amewataka wanawake  kujiepusha na matumizi ya dawa za asili pindi wanapokuwa wajawazito, ili waweze kujiepusha na uwezekano wa kupata matatizo mbalimbali wakati wa kujifungua.

Mwalimu ametoa rai hiyo jana mjini Songea, alipokuwa akizungumza na  madakatari na wauguzi   wakati alipotembelea hospitali ya mkoa Songea, ambapo alijionea uhaba wa vitanda katika wodi namba ya tatu  inayotumiwa na akinamama waliojifungua pamoja na mlundikano wa wagonjwa.

Alisema kuwa sera ya afya serikali awamu ya tano, inalenga kuboresha huduma za matibabu kwa wananchi wake kwa kuongeza vifaa tiba, wauguzi na madakatari na kwamba alieleza kuwa ni jambo la kushangaza kuona baadhi ya watu hadi tunaingia karne hii ya 22 bado wanaendelea kutumia  madawa ya asili   kutibu maradhi waliyonayo.

Alibainisha kuwa serikali itaendelea kuboresha huduma zake za matibabu katika vituo vya afya, zahanati na hospitali zote bhapa nchini, hivyo ni vyema wananchi wajitokeze kupata huduma za matibabu pale wanapohisi  dalili za homa badala ya kutumia dawa za asili ambazo wakati mwingine zina madhara makubwa kwa mtumiaji.


Mbali na hilo, amewaasa wananchi kuendelea kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na wa afya ya jamii (CHF) ili kuwa na uhakika wa matibabu na kupunguza, matumzi makubwa ya fedha kuliko kuweka fedha nyumbani au kutembea nazo mifukoni.

Aidha ameuagiza uongozi wa mkoa wa Ruvuma, kuangalia namna wanavyoweza kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali hiyo kwa kuboresha huduma za matibabu kwenye zahanati, vituo vya afya na kuimarisha hospitali za wilaya.

“Nawasihi  viongozi wa mkoa wa Ruvuma, mmejionea wenyewe msongamano uliopo katika hospitali zetu angalieni namna ya kukabiliana na tatizo hili kwa kuboresha huduma katika hospitali zenu za wilaya, tuweze kuondoka na kero ya mlundikano wa wagonjwa”, alisema Waziri Mwalimu.

Kwa mujibu wa Waziri huyo ni kwamba, licha ya serikali kukabiliwa na tatizo la fedha hata hivyo itaendelea kuimarisha huduma za afya hasa kwa akina mama wajawazito na watoto ili kuwa na vizazi salama na kusaidia kuokoa maisha ya wanawake  wakati wa kujifungua.

Mwalimu amesikitishwa na vitendo  vilivyokithiri katika mkoa huo, vya wanawake kutupa watoto mara baada ya kujifungua  ambapo amewashauri  kutumia njia za kisheria kupata haki ya matunzo ya mtoto, kwa wanaume wanaowapa mimba.

Kutokana na hilo amewaagiza watendaji wa vijiji, mtaa na kata kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo katika maeneo yao kuwachukulia hatua wanawake wanaotupa watoto, kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa la jinai.

Alisema kuwa, mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa iliyokithiri kwa vitendo vingi vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, hivyo ameitaka jamii kuunganisha nguvu ili kupunguza vitendo hivyo ambavyo pia ni kinyume na maagizo ya mwenyezi Mungu.

No comments: