Friday, January 15, 2016

SERIKALI KUZICHUKULIA HATUA HOSPITALI ZINAZOKIUKA TARATIBU

Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, wazee na watoto Ummy Mwalimu akisalimiana na Abate msaidizi wa Abasia ya Peramiho wilaya ya Songea mkoani Ruvuma Padri Lucius O.S.B  juzi alipotembelea hospitali ya rufaa ya Mtakatifu Joseph Peramiho mkoani Ruvuma, ambapo Waziri huyo alizungumza pia na watumishi wa hospitali hiyo.


Na Mwandishi wetu,
Songea.

SERIKALI imesema kuwa, itazichukulia hatua kali baadhi ya hospitali na vituo vya afya vya serikali ambavyo huwatoza fedha akina mama wajawazito, watoto wadogo walio chini ya umri wa miaka mitano na wazee ambao wanapaswa kupatiwa matibabu bure.

Kauli hiyo imetolewa jana wilayani Songea na Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, wazee na watoto Ummy Mwalimu wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa hospitali ya rufaa ya Mtakatifu Joseph Peramiho wilayani  humo.

Alisema sera ya afya, huduma za kujifungua, matibabu kwa wazee na watoto zinatolewa bure hivyo hospitali hazipaswi kuwatoza fedha makundi hayo badala yake zifuate maelekezo ya serikali,  kwani ni utekelezaji wa ahadi yake wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.


Mwalimu alilazimika kutoa ufafanuzi huo, kufuatia taarifa ya uongozi wa hospitali  hiyo kuwa wanawake wanaofika kwa ajili ya huduma za kujifungua wanalazimika kulipa kiasi cha shilingi 15,000 jambo ambalo ni kinyume na sera ya afya na maagizo ya serikali.

Aidha ameutaka uongozi wa hospitali hiyo, kuiga mfano mzuri wa hospitali ya rufaa Songea ambayo inatoa huduma hizo bila malipo, kwani ina wajibu wa kutoa huduma hizo bila malipo kwa sababu baadhi ya gharama zake kama vile madaktari wanaolipwa na serikali na dawa zinachangiwa na serikali.

Vilevile amefurahishwa na hatua ya hospitali hiyo, kutumia baadhi ya malighafi kama vile chupa kwa ajili ya dawa za maji (drip) zinazotengenezwa hapa nchini badala ya kuagiza nje ya nchi, na hivyo kupunguza gharama kubwa.

“Nimefurahishwa na hatua ya kutengeneza dawa za maji maji ninyi wenyewe, nitakwenda kukaa na wataalamu wangu  ili  na sisi tuanze kutengeneza wenyewe badala ya kuendelea kuagiza kutoka nje ya nchi”, alisema.

Awali mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Venance Mushi alisema kuwa licha ya hospitali hiyo kuhakikisha inaendelea kutoa huduma bora za matibabu kwa bei nafuu, lakini bado wanakabiliwa na changamoto nyingi.

Dkt. Mushi alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na  uhaba wa madawa, pamoja na vifaa tiba kutoka kwa makampuni yanayotengeneza vifaa hivyo, jambo linalosababisha kuingia gharama kubwa kuagiza vifaa  kutoka kwa makampuni mengine yanayojihusisha na uuzaji wa madawa.

Vilevile alisema kuwa, gharama za uendeshaji katika hosptali ya Peramiho inategemea wafadhili kutoka nje ya nchi na wanachama wachache wanaochangia huduma za matibabu kwa hiyo ni vema serikali ikaendelea na utaratibu wa kuiangalia kwa jicho la huruma ili iweze kukabiliana na idadi kubwa ya wananchi wanaokwenda kupata matibabu.

Kwa mujibu wa Dkt. Mushi alifafanua kuwa kwa siku hospitali hiyo, imekuwa ikipokea wagonjwa kuanzia 200 hadi 300  hivyo ni eneo ambalo wadau wengine ikiwemo serikali ni lazima kuiongezea nguvu ya kifedha, watumishi na vifaa tiba ili iweze kutoa huduma bora na za haraka.

No comments: