Tuesday, January 19, 2016

TANESCO WATAKIWA KUBADILI MWENENDO WA KAZI ZAO



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

WAZIRI wa Nishati na Madini  Profesa Sospeter Muhongo, amelitaka shirika la umeme Tanzania (TANESCO) hapa nchini, kubadili mwenendo wake wa utendaji kazi, kwa kujenga mahusiano mazuri na wadau, mashirika ya watu binafsi yenye mitambo ya kufua umeme kwa kutumia  maporomoko ya maji, ili kuweza kupunguza tatizo la upatikanaji wa nishati hiyo muhimu.

Profesa Muhongo alitoa  rai hiyo hivi karibuni, alipokuwa kwenye ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma, akikagua na kutembelea mitambo mbalimbali ya kuzalisha umeme pamoja na mgodi wa Ngaka unaozalisha makaa ya mawe uliopo katika kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani Mbinga mkoani humo.

Uchimbaji wa makaa hayo ya mawe hufanywa na kampuni ya Tancoal Energy ambapo Waziri huyo alipokuwa kwenye mgodi huo, alijionea kazi inayofanywa na kampuni hiyo, huku akisisitiza kwamba hakuna sababu ya Watanzania kukosa  umeme kwa sababu makaa hayo yana uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 400 wenye gharama nafuu, ambao utaunganishwa katika gridi ya taifa na kusambazwa katika maeneo mbalimbali.


Aliagiza kwamba kampuni ya Tancoal Energy, kwa kushirikiana na shirika la TANESCO wakae pamoja na kurekebisha bei za uzalishaji wa umeme, ili mitambo ya uzalishaji wa nishati hiyo iweze kujengwa katika mgodi huo na kuanza kazi ya uzalishaji ambao utaendana sambamba na soko lenye gharama nafuu.

 “Naagiza TANESCO jengeni ushirikiano na ondoeni kigugumizi, badala yake kuweni karibu na makampuni haya binafsi ambayo yanauwezo wa kusambaza umeme kwa wananchi kwa bei nafuu, ambayo kila mwananchi ataweza kunufaika nayo”, alisisitiza Profesa Muhongo.

Aidha Waziri huyo alitembelea mitambo miwili ya  kufua umeme kwa njia ya maporomoko ya maji ambayo ni wa Andoya Hydro Electric Power (AHEPO) uliopo katika kijiji cha Lifakara wilayani Mbinga na ule ambao unamilikiwa na shirika la Mtakatifu Benedict, Masista wa Chipole uliopo kijiji cha Tulila Songea vijijini.

Mitambo hiyo hivi sasa inatoa huduma kwa wananchi, chini ya shirika la TANESCO  ambapo umeme umeunganishwa katika njia kuu na kuweza kuwafikia wateja husika.

Kwa upande wake Meneja wa shirika hilo Kanda ya nyanda za juu kusini, Joyce Ngahyoma alisema kuwa shirika hilo lipo tayari kushirikiana na mashirika binafsi yanayojishughulisha na uzalishaji wa umeme, hivyo kilichobaki ni kukaa chini na kujenga makubaliano ya dhati namna ya kuboresha utoaji wa huduma hiyo kwa jamii.

Kadhalika Meneja mauzo wa kampuni ya Tancoal Energy inayochimba makaa ya mawe, Christopher Temba naye aliongeza kuwa makaa hayo yamekuwa ni kati ya makaa bora Afrika na kwamba, mengi yanategemewa kuuzwa kwenye viwanda vinavyozalisha saruji hapa nchini.

Temba alieleza kwamba katika kiwanda cha Dangote kilichopo mkoani Mtwara, walikubaliana kitachukua tani 13,500  kwa mwezi, lakini hivi sasa kimechukua tani 2,000 tu, jambo ambalo Waziri Muhongo aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kutimiza masharti ya mkataba walioingia na Tancoal, ikiwemo kutumia mkaa wa hapa nyumbani na sio kuagiza nje ya nchi kama wanavyofanya sasa kwa lengo la kukwepa kulipa ushuru na kodi mbalimbali.

No comments: