Saturday, January 2, 2016

WAZIRI MKUU MAJALIWA KUFANYA ZIARA YA KIKAZI MKOANI RUVUMA



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa atawasili mkoani Ruvuma kesho Jumapili kwa ajili ya kufanya ziara yake ya kikazi, ikiwemo kukagua shughuli mbalimbali za kimaendeleo na kuzungumza na wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa mkoa huo Said Mwambungu alisema kuwa Majaliwa atawasili majira ya saa 6:00 mchana, katika uwanja wa ndege mjini Songea.

Kassim Majaliwa.
Mwambungu alifafanua kuwa Waziri huyo atakuwa na ziara ya siku tatu ambapo baada ya kupokelewa katika uwanja huo wa ndege, atakwenda Ikulu ndogo Songea na kusomewa taarifa ya maendeleo ya mkoa huo.

Alisema kuwa siku itakayofuatia Januari 3 mwaka huu, atafanya ufunguzi wa ofisi za jengo jipya la shirika la Posta lililopo mjini hapa, ukaguzi wa ghala la chakula (NFRA) na maendeleo ya ujenzi wa ofisi za Halmashauri ya wilaya ya Songea vijijini iliyopo Peramiho wilayani humo.


“Baada ya hapo mheshimiwa Waziri, atasalimiana na wananchi wa Peramiho hivyo nawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kumpokea”, alisisitiza Mwambungu.

Kadhalika aliongeza kuwa siku itakayofuata atatembelea na kukagua wodi za kulaza wagonjwa Hospitali ya mkoa wa Ruvuma iliyopo Songea mjini, ambapo atazungumza na watumishi wa hospitali hiyo na baadaye watumishi wote wa umma waliopo mjini hapa.

Pamoja na mambo mengine ifikapo siku ya Jumatano atahitimisha ziara yake, kwa kufanya majumuisho juu ya mzunguko wote wa ziara yake atakayoifanya.

No comments: