Wednesday, January 20, 2016

SERIKALI YAWATAKA WATUMISHI AMBAO HAWAENDANI NA KASI YA HAPA KAZI TU WAJIONDOE WENYEWE



Na Steven Augustino,
Tunduru.

SERIKALI imewataka wataalamu na watumishi wa idara mbalimbali katika Halmashauri zote nchini, kuondokana na utendaji wa kufanya kazi kwa mazoea katika utekelezaji wa majukumu ya utumishi wa umma, ili kuweza kufikia mabadiliko ya kweli yatakayolifanya taifa lisonge mbele.

Aidha watendaji hao wametakiwa kujipima kama wanao uwezo wa kwenda sambamba na kauli mbiu ya serikali ya awamu ya tano ya ‘Hapa kazi tu’ na kwamba, kama wapo watakaojiona kuwa  hawawezi kuendana na kasi hiyo ya mabadiliko hayo wajitoe mapema wenyewe.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Utawara Bora, Suleiman Saidi Jafo wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa idara za halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, katika kikao kilichofanyika ukumbi wa Klasta ya walimu wa tarafa ya Mlingoti mjini hapa.

Waziri Jafo alisema katika kuleta mabadiliko ya kweli, inatakiwa kila mtumishi ajipange kufanya kazi kwa juhudi na maarifa kwa kujitoa kwa moyo wa dhati kwa manufaa ya Watanzania wote.

"Katika kuhakikisha kwamba dhana ya hapa kazi tu inafanikiwa, kila mfanyakazi katika idara yake afanye kazi kwa  uadilifu na weledi wa hali ya juu vinginevyo mtumishi ambaye hataki kufuata nyayo hizi, hafai kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano", alisema Naibu Waziri Jafo.


Vilevile katika hotuba yake pia alikumbushia agizo lake la kuzitaka halmashauri zote kuhakikisha kwamba zinafunga mfumo wa kielektroniki tayari kwa ajili ya kuanza ukusanyaji wa mapato, kupitia mfumo huo na kwamba halmashauri itakayoshindwa kufanikisha zoezi hilo Mkurugenzi wake ajitoe mwenyewe.

Naibu Waziri huyo aliendelea kusisitiza kuwa lengo la maagizo hayo ni kukata mirija iliyokuwa imewekwa na wajanja wachache, ambao wamekuwa wakijinufaisha kupitia utaratibu mbovu wa kukusanya mapato na kwamba utaratibu wa kukusanya mapato kupitia mfumo huo, utasaidia kuinua mapato ya ndani ili fedha zitakazokusanywa ziweze kufanya kazi ya kuboresha huduma mbalimbali za wananchi.

Alisema utaratibu huo wa kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, fedha zitakazopatikana zitasaidia kuondoa kero ambazo zimekuwa zikisumbua halmashauri nyingi hapa nchini, ikiwemo ulipaji wa madeni ya watumishi. 

Vilevile Waziri Jafo, aliwashukia wakuu wa idara na kuwataka kuachana na tabia za ukiritimba usiokuwa wa lazima wa kukwamisha utekelezaji wa mipango mbalimbali, ambayo imekuwa ikipangwa hadi wahakikishe kuwa wameweka watu wao ndipo wakubali kupitisha malipo husika.

"Ole wenu wakuu wa idara wababaishaji, kwa sasa ofisi yangu imeanzisha sera ya mlango wazi na tumegawa namba za simu katika ofisi zote za Wenyeviti wa hamashauri, manispaa na majiji ili kudhibiti hali hii", alisema. 

Awali Mkuu wa wilaya ya Tunduru,  Agnes Hokororo alimweleza Naibu Waziri huyo kwamba, wilaya yake imejipanga kuhakikisha inasimamia kikamilifu fedha ambazo wamezipata kwa ajili ya kutekeleza dhana ya elimu bure kulingana na maelekezo ya serikali ya awamu ya tano. 

No comments: