Wednesday, January 20, 2016

MKUU WA WILAYA YA MBINGA AITAKA NEMC KUINGILIA KATI JUU YA UCHAFUZI WA MAZINGIRA MGODI WA MAKAA YA MAWE NGAKA



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga amelitaka Baraza la Usimamizi wa Mazingira ya Taifa (NEMC) kuchukua hatua za haraka dhidi ya tatizo la uchafuzi wa mazingira, ambalo linaendelea kufanyika katika mgodi wa makaa ya mawe Ngaka uliopo kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda mkoani humo.

Aidha alifafanua kuwa kampuni ya Tancoal Energy, ambayo ndiyo imepewa dhamana ya uchimbaji wa makaa hayo, licha ya kupewa maelekezo na NEMC mara kwa mara namna ya utunzaji wa mazingira ikiwemo kudhibiti maji taka yasiweze kuingia kwenye mto ambao hutumika kwa shughuli za kibinadamu na wananchi wa kata hiyo, bado wamekuwa wakipuuza na hawazingatii maelekezo husika waliyopewa.

“Jambo hili limekuwa likijirudia mara kwa mara, nitawasiliana na watu wa baraza la mazingira kuona ni namna gani hatua zichukuliwe juu ya tatizo hili, ambalo uharibifu wa mazingira bado unaendelea”, alisema Ngaga.


Ngaga alisema hayo alipokuwa kwenye kikao maalumu, katika kata ya Ruanda na uongozi wa kampuni ya Tancoal Energy wakiwemo na baadhi ya wananchi wa kata hiyo wakijadili juu ya athari mbalimbali, zitokanazo na shughuli za mgodi ambazo zinaendelea kufanyika na kuathiri jamii.

Kadhalika Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga alibainisha kuwa kampuni hiyo inayozalisha makaa ya mawe, imeshindwa kubuni mbinu mbadala ya kuweza kuzuia maji taka ambayo yamechanganyika na chembe chembe za mkaa huo yasiingie kwenye mto Nyamabeva ambao upo katika kata hiyo, jambo ambalo pia ni hatari kwa afya ya jamii inayozunguka katika eneo hilo ambao hutegemea maji hayo.

Vilevile kufuatia hali hiyo, Ngaga ametoa agizo kwa uongozi wa Tancoal Energy kuhakikisha kwamba wanazingatia juu ya suala la upimaji ubora wa maji mara mbili kwa mwaka na sio mara moja kama wanavyofanya sasa, ambayo wananchi huyatumia katika shughuli zao za kibinadamu ili kuweza kujua yana madhara gani na hatua husika ziweze kuchukuliwa katika kunusuru hali hiyo.

Alisema kuwa amekuwa akipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wa kata ya Ruanda kwamba, hata magari yanayosafirisha mkaa huo hayafunikwi maturubai ipasavyo ili kuweza kuzuia vumbi la mkaa lisiweze kuleta madhara kwa wananchi.

Pamoja na mambo mengine, awali alipokuwa akichangia hoja katika kikao hicho juu ya malalamiko hayo, Diwani wa kata ya Ruanda kupitia tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Edimund Nditi alisisitiza kuwa umefika wakati sasa jambo hilo halipaswi kufumbiwa macho hivyo kuna kila sababu kwa mamlaka husika kuchukua hatua, ili kuweza kudhibiti hali hiyo na kuzuia madhara makubwa yanayoweza kutokea hapo baadaye.

Nditi alifafanua kuwa nyakati za masika kumekuwa na tatizo kubwa katika mgodi huo, hasa pale mvua zinaponyesha maji yanayotiririka kutoka kwenye mashimo ya mgodi husafirisha kiasi kikubwa cha sumu ya mkaa wa mawe na kuingia kwenye visima vya asili ambavyo wananchi hutegemea maji yake kuendeshea maisha yao.

Naye Asteria Mahundi ambaye ni mkazi wa kijiji cha Ntunduaro aliongeza kuwa maji yote wanayotumia katika kijiji hicho sio salama kwa afya ya binadamu, ambapo alieleza kuwa wakisha ya chota kutoka kwenye visima hivyo na kuyafikisha nyumbani baada ya muda mfupi yanapo tuama, huwa na rangi nyeusi huku juu yake yakiwa yametanda chembe chembe za mkaa wa mawe.

Pia Mwenyekiti wa kijiji cha Ruanda, Deograthias Haulle alimweleza Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Ngaga kwamba ufanyike utaratibu kwa kampuni hiyo ya makaa ya mawe itoe mchango wake kwa wananchi kwa kuwajengea miundo mbinu ya bomba la maji safi na salama ili wasiweze kuathirika afya zao.

Kikao hicho kimefanyika kufuatia agizo lililotolewa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipokuwa katika ziara yake ya kikazi Januari 12 mwaka huu hapa mkoani Ruvuma, alipotembelea mgodi huo na kujionea changamoto mbalimbali. 

Hata hivyo Profesa Muhongo aliagiza kwa kumtaka Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Ngaga akae na menejimenti ya kampuni hiyo inayozalisha mkaa wa mawe katika mgodi wa Ngaka, wakiwemo baadhi ya wananchi na uongozi wa kata hiyo ili waweze kujadili changamoto zilizopo mbele yao na kuzifikisha ngazi ya juu serikalini ili ziweze kufanyiwa kazi.

No comments: