Thursday, January 14, 2016

MHAGAMA ASEMA SERIKALI AWAMU YA TANO IMERUDISHA HESHIMA



Na Muhidin Amri,
Songea.

WAZIRI wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, sera, uratibu, bunge na walemavu Jenister Mhagama amesema serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dokta John Magufuli imefanikiwa kurudisha heshima ya nchi, ambayo awali ilipoteza matumaini kwa wananchi wake.

Jenister ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma, alitoa kauli hiyo hivi karibuni katika kijiji cha Lundusi wilaya ya Songea mkoani humo wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji hicho katika eneo la ujenzi wa ofisi ya makao makuu ya halmashauri ya wilaya hiyo.

Alisema kuwa wananchi wa jimbo hilo wanahitaji mabadiliko makubwa ya kimaendeleo hivyo viongozi waliopewa dhamana wanapaswa kuongeza jitihada na uwajibikaji katika maeneo yao ya kazi ili kuweza kuleta ufanisi kwa faida ya sasa na baadaye.


Pamoja na mambo mengine Waziri huyo alifafanua kuwa baada ya serikali kufuta ada na michango mbalimbali kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, atahakikisha watoto wote wenye sifa ya kuanza masomo wanakwenda shule ili kupunguza tatizo la watu wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu katika  jimbo hilo.

Mbali na hilo, Jenister ameishukuru serikali kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya makao makuu ya halmashauri hiyo, nyumba ya mkurugenzi na nyumba mbili za wakuu wa idara hatua ambayo itasaidia  wananchi kupata huduma kwa karibu na hivyo kuchochea kuharakisha maendeleo yao na mkoa huo kwa ujumla.

Aidha ameiomba serikali kupitia shirika la ugavi wa umeme nchini (TANESCO) kuhakikisha kwamba linapeleka nishati hiyo katika kata ya Maposeni na baadhi ya maeneo ili kuweza kusaidia kuharakisha maendeleo na kukaribisha baadhi ya watu kuwekeza miradi ya maendeleo.

Akizungumzia kuhusu kilimo Waziri huyo alisema, wananchi wa jimbo la Peramiho ndiyo wanaoongoza kwa uzalishaji mkubwa wa chakula hasa  zao maarufu la mahindi ambapo asilimia 50 ya mahindi yanayolimwa katika mkoa wa Ruvuma yanatoka Peramiho hivyo ni vyema serikali ikaongeza upatikanaji wa pembejeo za kutosha kwa wakulima wa jimbo hilo.

Pia alieleza kuwa suala la upatikanaji wa pembejeo limeleta malalamiko mengi kwa serikali, kwani wanaonufaika na mpango huo ni mawakala na wajanja wachache badala ya wakulima wenyewe, jambo ambalo linarudisha nyuma mpango wa serikali wa kuleta maendeleo kupitia sekta ya kilimo.

Katika msimu wa mwaka huu imeshauriwa kwamba Wizara ya kilimo  inapaswa kuangalia upya suala la kuwatumia mawakala kununua mahindi ya wakulima kwa bei ndogo ya shilingi 120 mpaka 200 kwa kilo, huku wao huiuzia serikali kwa bei kubwa ya shilingi 500 kwani haileti usawa kwa wakulima ambao ndiyo walengwa wakubwa na mawakala hao wanaotumia   mgongo wa watu wengine kujinufaisha.

Tayari  serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa imeshapiga marufuku kwa Wakala wa hifadhi ya chakula hapa nchini (NFRA) kuwatumia mawakala kwenda vijijini kununua mahindi kwa wakulima,  badala yake serikali ndiyo itakayonunua mahindi hayo na kuiagiza NFRA  kufungua vituo vya ununuzi katika maeneo yanayozalisha kwa wingi zao hilo na kununua kwa bei ambayo itapangwa na serikali.

No comments: