Na Steven
Augustino,
Tunduru.
FAMILIA ya Athuman Mbwana, wa kijiji cha Nambalapi kata ya
Masonya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma inawaomba wasamaria wema kutoa msaada
wa kuwawezesha kulea watoto wao watatu, ambao walizaliwa kwa wakati mmoja ndani ya
familia yao.
Mbwana alitoa ombi hilo, alipokuwa akizungumza na mwandishi
wetu baada ya wauguzi na wakunga wa Hospitali ya wilaya hiyo, kumtaarifu kuwa mkewe
kipenzi Rehema Rashid ambaye alipelekwa hospitalini hapo akiwa mjamzito,
kajifungua watoto hao kwa mpigo.
Aidha anaiomba serikali na taasisi binafsi kuwa na jicho la
huruma, ili waweze kumsaidia kutunza watoto hao kutokana na yeye binafsi kuwa
na kipato kidogo cha kumwezesha kuishi.
Alisema kupata watoto hao ni neema ya mwenyezi Mungu, na
matokeo hayo hayakuwa matarajio yake hivyo anaomba msaada wa hali na mali ili
aweze kuwatunza na kuwapatia mahitaji muhimu, ambayo yatawafanya waishi na kukua
vizuri.