![]() |
Baraza maalum la Madiwani Halmashauri ya mji wa Mbinga likiwa limeketi katika kikao chake kujadili ubadhirifu wa fedha za mavuno ya msitu wa Mbambi katika halmashauri hiyo. |
![]() |
Mwenyekiti wa Kamati maalum ya kuchunguza msitu wa Mbambi halmashauri mji wa Mbinga, Kelvin Mapunda akikabidhi taarifa ya uchunguzi kwa Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ndunguru Kipwele. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani
Ruvuma, limetoa mapendekezo yake ya kumkataa Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri
hiyo Robert Kadaso Mageni kwamba hawataki kufanya naye kazi tena, wakimtuhumu ametafuna
fedha za mauzo ya mbao zilizopasuliwa katika msitu wa Mbambi uliopo mjini hapa ambao
ni mali ya halmashauri ya mji huo.
![]() |
Robert Kadaso Mageni. |
Aidha imeelezwa kuwa Mkurugenzi huyo amelipotosha baraza hilo
katika kikao walichoketi Novemba 2 hadi 3 mwaka jana na kutoa taarifa za uongo kwamba
msitu huo una jumla ya miti 5,4040 ambayo inafaa kupasuliwa mbao wakati ukweli
ni kwamba msitu ulikuwa na miti 8,470.
Kufuatia taarifa hizo ambazo hazikuwa sahihi wakati anazitoa
kwenye baraza hilo juu ya uvunaji wa msitu huo, hali hiyo imesababisha
halmashauri kupata hasara ya shilingi milioni 888,000,000.
Baada ya baraza hilo la Madiwani kutoa mapendekezo hayo ya
kumkataa, walimtaka Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye kufikisha kilio chao
kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli ili
aweze kuchukua hatua zaidi za kinidhamu dhidi ya mtumishi huyo.