Thursday, December 31, 2015

JESHI LA POLISI LATOA TAHADHARI KUHUSIANA NA MKESHA WA MWAKA MPYA



TUNAPOELEKEA kumaliza mwaka huu 2015 na kuukaribisha  mwaka mpya wa  2016, wananchi hutumia muda huo kwenda  katika nyumba za ibada ama kusherekea katika maeneo mbalimbali ya starehe, ambapo uzoefu unaonyesha kuwa baadhi ya watu hupenda kutumia fursa hiyo kufanya vitendo  vinavyohatarisha usalama wa raia mali zao.

Jeshi la Polisi nchini, limejipanga vizuri katika mikoa yote kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha kwamba vitendo vyovyote vya uhalifu vitakavyojitokeza  hususan katika kipindi hiki cha kuelekea mkesha wa mwaka mpya vinadhibitiwa. 

Ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote ya ibada, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine yote ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu.

WAZIRI MKUU ANUSA UFISADI KIGOMA




WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa siku mbili kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Eng. John Ndunguru kukamilisha uchunguzi wake na kumpatia taarifa ya maandishi juu ya tuhuma ubadhirifu wa fedha za umma unaohusisha uuzwaji wa jengo la KIGODECO na viwanja 12 vya Manispaa ya Kigoma/Ujiji ambao unadaiwa kukiuka taratibu.

Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumatano, Desemba 30, 2015) kwenye ukumbi wa NSSF, mjini Kigoma wakati akizungumza na viongozi na watendaji mbalimbali wa mkoa huo alipokuwa akifanya majumuisho ya ziara yake ya siku mbili mkonai humo.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema anazo taarifa kuwa jengo hilo liliuzwa kwa sh. milioni 370/- pamoja na jengo jingine la MIBOS kwa sh. milioni 50/- licha ya kupewa barua na Mkuu wa Mkoa huo kusitisha uuzwaji wa jengo pamoja viwanja hivyo, bado liliuzwa.

SERIKALI KUWACHUNGUZA WAGANGA NA WAUGUZI WANAOMILIKI MADUKA YA DAWA BARIDI

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.


SERIKALI imetangaza kuwachunguza waganga na wauguzi, wanaomiliki hospitali, kliniki na maduka ya dawa baridi ili kubaini kama wanahusika na upotevu wa dawa kwenye hospitali za Serikali.

Akizungumza ofisini kwake jana, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alisema Desemba 26 alipotembelea Hospitali ya Ocean Road, aliamua kuunda kamati ya watu watano kuchunguza kama wanahusika na upotevu wa dawa hospitalini hapo na sehemu nyingine.
Alisema bodi ya hospitali hiyo aliyoiunda wiki mbili zilizopita, nayo imeshaanza kufanya kazi ya kubaini chanzo cha uhaba wa dawa hospitalini hapo.

“Hata ukisoma tamko langu, hatukatazi watumishi wa umma wa sekta ya afya kumiliki hospitali, kliniki au maduka ya dawa, lakini tunachoangalia ni namna gani tunaondoa mgongano wa kimasilahi,” alisema.

Wednesday, December 30, 2015

MAKATIBU WAKUU WALIOTEULIWA NA RAIS MAGUFULI HAWA HAPA

GUL1
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akitangaza Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu Ikulu jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, na kulia ni Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue wakisikiliza kwa makini.

GUL2
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwaonesha orodha ya Makatibu na Manaibu Katibu Wakuu aliowateua huku Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue wakishuhudia.

GUL3
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwaonesha orodha ya Makatibu na Manaibu Katibu Wakuu aliowateua huku Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue wakishuhudia.

GUL4
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue Mara baada ya kumkabidhi orodha ya Makatibu na Manaibu Katibu Wakuu aliwateua leo Ikulu jijini Dar es Salaam. Picha zote na IKULU.
...................................................................................................................................................

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefanya uteuzi wa makatibu wakuu na manaibu Katibu wakuu katika Wizara mbalimbali.
Walioteuliwa ni kama ifuatavyo;
  1. Katibu Mkuu Kiongozi
Balozi – Ombeni Sefue
  1. Katibu Mkuu Ikulu
Peter Ilomo
  1. Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
Dkt. Laurian Ndumbaro
  1. Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
Mhandisi Mussa Iyombe (Katibu Mkuu)
Dkt. Deo  Mtasiwa (Naibu Katibu Mkuu – Afya)
Bernard Makali (Naibu Katibu Mkuu – Elimu)
  1. Ofisi ya Makamu wa Rais
            Mbaraka A. Wakili ( Katibu Mkuu)
            Mhandisi Ngosi Mwihava (Naibu Katibu Mkuu)
  1. Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge, Sera, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu)
Erick Shitindi (Katibu Mkuu Kazi na Ajira)
Mussa Uledi (Katibu Mkuu Bunge)
Dkt. Hamis Mwinyimvua (Katibu Mkuu – Sera)
  1. Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
Dkt. Frolence Turuka (Katibu Mkuu – Kilimo)
Dkt. Mashingo (Katibu Mkuu Mifugo)
Dkt. Budeba (Katibu Mkuu – Uvuvi)
  1. Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Mhandisi Joseph. Nyamuhanga (Katibu Mkuu – Ujenzi)
Dkt. Leonard M. Chamuliho (Katibu Mkuu – Uchukuzi)
Profesa Faustine R. Kamuzora (Katibu Mkuu – Mawasiliano)
Mary Sassabo (Naibu Katibu Mkuu Mawasiliano)
  1. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Dkt. Yamungu Kayandabira (Katibu Mkuu)
Dkt. Moses Kusiluka (Naibu Katibu Mkuu)
  1. Wizara ya Maliasili na Utalii
Meja Jenerali Gaudence S. Milanzi (Katibu Mkuu)
Anjelina Madete (Naibu Katibu Mkuu)
  1. Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
Dkt. Adelhem James Meru (Katibu Mkuu – Viwanda)
Profesa Adolf F. Mkenda (Katibu Mkuu – Biashara na Uwekezaji)
Mhandisi Joel Malongo (Naibu Katibu Mkuu)
  1. Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi.
Maimuna Tarishi (Katibu Mkuu)
Profesa Simon S. Msanjila (Naibu Katibu Mkuu)
Dkt. Leonard Akwilapo (Naibu Katibu Mkuu)
  1. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Dkt. Mpoki Ulisubisya (Katibu Mkuu – Afya)
Sihaba Nkinga (Katibu Mkuu – Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto)
  1.  Wizara ya Habari, Utamaduni,  Sanaa na Michezo
Profesa Elisante Ole Gabriel Mollel (Katibu Mkuu)
Nuru Halfan Mrisho (Naibu Katibu Mkuu)
  1. Wizara ya Maji na Umwagiliaji
Mhandisi Mbogo Futakamba (Katibu Mkuu)
Mhandisi Kalobero Emmanuel (Naibu Katibu Mkuu)
  1.  Wizara ya Nishati na Madini
Profesa Justus W. Ntalikwa (Katibu Mkuu)
Profesa James Epifani Mdoe (Naibu Katibu Mkuu)
Dkt. Paulina Pallangyo (Naibu Katibu Mkuu)
  1.  Wizara ya Katiba na Sheria
Profesa Sifuni Mchome (Katibu Mkuu)
Suzan Paul Mlawi (Naibu Katibu Mkuu)
Amon Mpanju (Naibu Katibu Mkuu)
  1.  Wizara ya Mambo ya Ndani
Jaji Meja Jenerali Projest A. Rwegasira (Katibu Mkuu)
Balozi Hassan Simba Yahaya (Naibu Katibu Mkuu)
  1.  Wizara ya Fedha na Mipango
Dkt. Silvacius Likwelile (Katibu Mkuu)
Dorothy Mwanyika (Naibu Katibu Mkuu)
James Dotto (Naibu Katibu Mkuu)
Amina Hamis Shaban (Naibu Katibu Mkuu)
  1. Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa
Dkt. Aziz Mlima (Katibu Mkuu)
Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi ( Naibu Katibu Mkuu)
  1. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
Job D. Masima (Katibu Mkuu)
Immaculate Peter Ngwale (Naibu Katibu Mkuu
Makatibu wakuu na Manaibu Katibu Wakuu wote ambao hawajatajwa katika orodha hii watapangiwa kazi nyingine.
Katika hatua nyingine Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Bw. Eliakimu Maswi kuwa Kaimu Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na ametengua uteuzi wa Naibu Kamishina wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Bw. Lusekelo Mwaseba, ambaye atapangiwa kazi nyingine.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
30 Desemba, 2015

HALMASHAURI MADABA YAKAMILISHA UPIMAJI VIWANJA 500



Na Mwandishi wetu,
Songea.

HALMASHAURI ya wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma, imekamilisha mradi wa upimaji viwanja 500 katika kijiji cha Madaba  wilayani humo, ambavyo vitatumika kwa ajili ya ujenzi wa mji mpya wa wilaya hiyo.

Upangaji  mpya wa eneo hilo, umeanza na upimaji viwanja katika maeneo ambayo wananchi wanayatumia kama  mashamba ambapo wametakiwa kuyaachia ili kupisha kazi  hiyo, hatua inayotajwa kwamba itaweza kubadili sura ya  wilaya hiyo mpya na kuwa mji mdogo.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi mtendaji wa Halmshauri hiyo, Robert Mageni alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa upangaji mpya wa eneo  la kijiji cha Madaba na maeneo jirani, utazingatia ramani itakayochorwa na wataalamu husika kutoka idara ya ardhi.

WAHUKUMIWA KWENDA JELA KWA KOSA LA KUKUTWA NA LITA 60 ZA GONGO



Na Steven Augustino,
Tunduru.

WATU wawili ambao ni wakazi wa kijiji cha Mkapundwa wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wamehukumiwa kutumikia kifungo cha miezi 10 jela baada ya kupatikana na kosa la kukutwa na lita 60 za pombe ya moshi, maarufu kwa jina la gongo.

Adhabu hiyo ilitolewa na Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya wilaya hiyo, Gladys Barthy baada ya mahakama hiyo kujiridhisha na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.

Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka mkaguzi msaidizi wa Polisi Inspekta Songelaeli Jwagu alidai mahakamani hapo kuwa, watuhumiwa waliokuwa wanakabiliwa na shauri hilo kuwa ni, Mohamed Ally Buji aliyehukumiwa kutumikia kifungo cha miezi 6 au kulipa faini ya shilingi 350,000 na Mohamed Ally Mohamed aliyehukumiwa kifungo cha miezi 4 au kulipa faini ya shilingi 250,000.

Sunday, December 27, 2015

MAPATO YA GESI YAWEKWA HADHARANI



DAR ES SALAAM.

WAKATI eneo la kujenga kiwanda cha kuchakata gesi itakayovunwa baharini likitangazwa kupatikana wiki hii, uvunaji utakapoanza Serikali itapata mapato makubwa kutokana na mikataba minono iliyoingiwa.

Akizungumza katika mahojiano maalumu, Mkurugenzi wa Utafutaji na Uendelezaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Kelvin Komba, amesema mfumo wa sasa wa mikataba, unaihakikishia Serikali kupata mpaka asilimia 85 ya faida yote ya kitalu, baada ya kutoa gharama za uzalishaji na ukataji kodi. 

Kwa mujibu wa Komba, mwekezaji akigundua gesi au mafuta, anatakiwa kurudisha gharama zake zilizotumika katika utafiti na baada ya hapo, faida hugawanywa kati ya Taifa na mwekezaji.

Taarifa zinaonesha kuwa mpaka sasa Tanzania kumefanyika ugunduzi wa gesi asilia katika eneo la bahari na nchi kavu, inayofikia takribani futi za ujazo trilioni 55.21. “Hata hivyo utajiri huu ili uwe na tija kwa Taifa ni lazima sheria, kanuni, sera na mikataba iwekwe katika namna ambayo inanufaisha Taifa,” alisema Komba.

Mgawanyo Akifafanua zaidi, Komba amesema Tanzania kwa sasa inatumia mfumo wa Mkataba wa Ugawanaji Mapato (Production Sharing Agreement-PSA), kati ya Taifa na mwekezaji, ambao mgawanyo wa mapato umewekwa kwa asilimia na hutofautiana kulingana na kiwango cha uzalishaji na maeneo ugunduzi ulipofanyika. 

MWENYEKITI CCM MKOA WA IRINGA NA WENGINE WALIOTAJWA KUKISALITI CHAMA WAKATI WA UCHAGUZI MKUU KUANZA KUHOJIWA

Jesca Msambatavangu.

IRINGA.

KAMATI za Maadili Chama cha Mapinduzi (CCM) ngazi mbalimbali mkoani Iringa zinaanza kukutana leo Jumatatu Desemba 28, kusikiliza ushahidi toka kwa wanaCCM wanaodaiwa kukisaliti chama hicho wakati wa uchaguzi Mkuu ambao ulifanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Mmoja wa watakaoitwa na kamati hizo ni Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo, Jesca Msambatavangu na Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa, Mahamudu Madenge.

WANANCHI WAIBUA MADUDU YALIYOPO HOSPITALI YA WILAYA MBINGA

Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

BAADHI ya wananchi wanaoishi katika Jimbo la Mbinga mjini mkoani Ruvuma, wamelalamikia juu ya kero wanazozipata katika Hospitali ya wilaya ya Mbinga mkoani humo, ikiwemo baadhi ya waganga kuwa na tabia ya kuomba rushwa kutoka kwa wagonjwa wanaokwenda hospitalini hapo kwa ajili ya kupata matibabu.

Rais John Pombe Magufuli.
Aidha imedaiwa kuwa kundi kubwa linaloathirika wanapokuwa katika hospitali hiyo ni la watoto wadogo na akina mama wajawazito, ambapo wanapokuwa kwenye foleni kwa ajili ya kumuona daktari hukaa muda mrefu bila kuhudumiwa na kusababisha wakati mwingine, mgonjwa kupoteza maisha.

Hayo yalisemwa na wananchi hao leo, kwenye mkutano maalumu ambao uliitishwa na Mbunge wa Jimbo hilo la Mbinga mjini, Sixtus Mapunda katika ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.

Mkazi mmoja wa kitongoji cha Lusonga aliyejitambulisha kwa jina la, Gerwada Nchimbi alieleza kuwa hata mama mjamzito ambaye amejifungua kwa njia ya operesheni endapo asipotoa rushwa ya fedha, dawa za kusafishia kidonda hapati na anaambiwa akanunue kwenye duka la dawa muhimu ndipo ahudumiwe.

WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO WAO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA



Na Julius Konala,
Songea.

ZAIDI ya watoto 300 wamebatizwa Jumapili ya sherehe za krismasi kwenye Kanisa katoliki Parokia ya Bombambili, Jimbo kuu la Songea mkoani Ruvuma kitendo ambacho kimeelezwa kuwa ni cha kihistoria kwa madai kwamba, ni mara ya kwanza kutokea tangu kuanzishwa kwa Parokia hiyo.

Ibada hiyo ya misa takatifu ya ubatizo iliongozwa na Padri Godfrey Nchimbi, huku akisaidiwa na mapadre wengine mbalimbali wakiwemo Otieno Olwen na Simon Ndunguru ambaye ni Paroko wa parokia hiyo ya Bombambili.

Sambamba na hilo jumla ya watu 73 walipata sakramenti ya ndoa katika kanisa hilo, tukio ambalo lilitanguliwa na baadhi yao ambao hawakuweza kufuata hatua za sakramenti kwa kufuata utaratibu wa kanisa, walianza kupewa sakramenti ya ubatizo, kipaimara na kisha kufungishwa ndoa.

Matukio hayo yote mawili yalikwenda sambamba na kula chakula cha pamoja kilichoandaliwa na Paroko wa parokia hiyo, Padri Simon Ndunguru katika ukumbi wa mikutano wa parokia hiyo na kuhudhuriwa na waumini mbalimbali, wakiwemo wasimamizi wa watoto wa ubatizo na ndoa.

SIXTUS MAPUNDA : AKILI ZA KUGOMBANA KUTOKANA NA MAMBO YA KISIASA NI AKILI ZA MATOPE

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MBUNGE wa Jimbo la Mbinga mjini, Sixtus Mapunda amewataka Vijana wa jimbo hilo wakae na kutambua kwamba muda wa kampeni na siasa umekwisha, kilichobaki wanapaswa kushirikiana na kutengeneza mustakabali wa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Sixtus Mapunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini.
Aliwaonya pia wakiendelea kuwa na akili za kugombana na kujengeana chuki kutokana na mambo ya kisiasa, hawatafika mbali badala yake watarudi nyuma kimaendeleo.

“Niliona kuna sababu ya mimi kutafuta muda wa kukaa na kuzungumza na vijana, mkiendekeza akili za kugombana au kupigana kutokana na mambo ya kisiasa hizi ni akili za matope, tutumie muda wetu kujadili maendeleo yetu wapi tulipo na wapi tunapaswa kwenda”, alisema.

Mapunda alisema hayo leo katika kikao maalumu cha vijana, ambacho kiliketi kwenye ukumbi wa Umati uliopo Mbinga mjini na kuongeza kuwa sababu kuu ya kuzungumza na vijana hao, ni kuchukua mawazo yao ambayo yana manufaa kwa wananchi ili aweze kuyapeleka katika ngazi husika serikalini na yaweze kufanyiwa kazi.

Saturday, December 26, 2015

JE KULEWA, KUTOKUWA NA AKILI TIMAMU NI KINGA BAADA YA KUTENDA JINAI ?


 Na Bashir Yakub,

SOTE tunajua  kwamba  kila  atendaye  kosa  sharti  aadhibiwe. Na kuadhibiwa huko  lazima  kuwe  kwa mujibu  wa  sheria, pamoja  na  kuwa mtenda  kosa hustahili adhabu bado watenda kosa hutofautiana hadhi. Hadhi hapa  sio kuwa fulani ni mkuu wa mkoa au mkurugenzi na fulani ni mkulima  wa kawaida kijijini  Katanakya. 

Hadhi  ndio  kama  hizo  zilizotajwa katika  kichwa  cha  makala.  Wapo  watenda  makosa   lakini  wakiwa na  umri  mdogo,  wapo  watenda  makosa  lakini  wakiwa  hawana  akili  timamu  halikadhalika  wapo  watenda  makosa  lakini  wakiwa  na  akili  isiyo ya  kawaida  kwa  maana  ya  akili  ya ulevi.

Sheria inasemaje  juu ya hawa  wote  kuanzia  utendaji  wao  wa makosa,  kushitakiwa  na  kuwajibika    kwao.  Makala  haya yataeleza  ili   tujue   hadhi  ya  kimashitaka  ya makundi  haya.


1.JE  MWENYE  UGONJWA  WA  AKILI  ANAWEZA  KUSHITAKIWA ?

Jibu  ni  ndiyo  sheria  haikatazi  kumshitaki  mwenye  ugonjwa  wa  akili (chizi). Kuna  tofauti  kati ya  kushitakiwa  na  kuwajibika, kushitakiwa ni  kumfungulia  mashtaka  na  kuwajibika  ni  kupata  adhabu baada  ya  kupatikana  na  hatia. Hivyo kushitakiwa atashitakiwa,  isipokuwa  sheria  inatoa  mwongozo  kuhusu  kuwajibika kwake.

Thursday, December 24, 2015

MUUGUZI AKAMATWA AKIUZA DAWA ZA SERIKALI


Na Muhidin Amri,

Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma, linamshikilia Muuguzi msaidizi wa Zahanati ya kijiji cha Utwango wilaya ya Namtumbo mkoani humo, Agnera Luena kwa tuhuma ya kuuza dawa za serikali katika duka la mtu binafsi kinyume cha sheria.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Revocatus Malimi alisema tukio hilo lilitokea Disemba 23 mwaka huu majira ya saa nne asubuhi ambapo mtuhumiwa huyo akiwa kazini, aliiba dawa hizo na kwenda kuuza katika duka la Esha Tendwa lililopo katika kijiji cha Lusenti wilayani humo.

Revocatus Malimi.
Alisema mara baada ya kumkamata, Polisi walifanya upekuzi katika duka ambalo dawa hizo ziliuzwa na kukamata aina mbalimbali ambazo ziliibwa na mtuhumiwa huyo.

Kamanda Malimi alizitaja dawa zilizokutwa katika duka hilo ni, Paediatric cough Syrup chupa 13, Doxycline capsules kopo moja, Cotrimazole Syrup mbili, Diazepam Tables kopo moja, PPF injection moja na Amoxiline Oral Suspension mbili.

Aidha alizitaja dawa nyingine kuwa ni, Aspi -m- Chlorphenamine tablets moja, Alu 1x6 Packet 4, Alu 3x6 Packet 4, ambazo thamani yake bado haijajulikana.

SEKONDARI MAHANJE WANAFUNZI KUKOSA MADARASA YA KUSOMEA



Na Muhidin Amri,
Songea.

SHULE ya sekondari Mahanje iliyopo katika kata ya Mahanje wilayani Songea mkoa wa Ruvuma, inakabiliwa na uhaba mkubwa wa vyumba vya madarasa jambo ambalo linatishia watoto walioteuliwa kuanza kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo 2016, kukosa  mahali pa kusomea.

Kwa sasa shule hiyo ina vyumba  vinne vya madarasa kati ya 10 ambavyo vinahitajika ili viweze kutosheleza wanafunzi watakaoingia shuleni hapo kwa ajili ya kuanza masomo ya kidato cha kwanza hadi cha nne.

Aidha kutokana na hali hiyo, baadhi ya wadau wameanza kujitokeza akiwemo Mbunge wa jimbo la Madaba Joseph Mhagama aliyetoa bati 130 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa, katika shule hiyo.

HOSPITALI WILAYA YA MBINGA YAKABILIWA NA TATIZO LA UCHAKAVU JENGO LA UPASUAJI, SIXTUS MAPUNDA ASISITIZA KUJENGA USHIRIKIANO KUTATUA MATATIZO YALIYOPO

Sixtus Mapunda Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini upande wa kulia, akikabidhi vifaa tiba kwa Mganga mkuu wa Hospitali ya Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, Elisha Roberth ambapo zoezi hilo la makabidhiano hayo lilifanyika katika hospitali ya wilaya hiyo.
Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini, Sixtus Mapunda akiwagawia miswaki, dawa za kusafishia meno na sabuni za kuogea akina mama wajawazito ambao wanasubiri kujifungua waliopo Hospitali ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.
Sixtus Mapunda, akizungumza na akina mama wanaosubiri kujifungua katika wodi ya wazazi iliyopo Hospitali ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma. (Picha zote na gwiji la matukio Ruvuma)
Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

HOSPITALI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa jengo la kisasa la upasuaji jambo ambalo wagonjwa wengi wanaohitaji kupata huduma za upasuaji katika hospitali hiyo, hupata shida kutokana na jengo linalotumika sasa kuwa chakavu na halikidhi mahitaji husika.

Aidha imeelezwa kuwa hospitali hiyo, haina gari la kubebea wagonjwa ambapo hulazimika kutumia gari la kituo cha afya Mapera, kilichopo katika kata ya Mapera wilayani humo.

Sixtus Mapunda ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini, alielezwa hayo leo alipokuwa katika ziara ya kutembelea hospitali hiyo ya wilaya Mbinga kwa lengo la kujionea changamoto mbalimbali, ambazo hospitali hukabiliana  nazo.

Aliweza kutoa mchango wa vifaa tiba kama vile dawa za kufanyia usafi, bandeji za kufungia na kusafishia vidonda na mipira ya kuvaa mikononi (Gloves).
 
Vilevile aliwapatia akina mama wajawazito na waliojifungua watoto ambao wapo wodini wamelazwa; sabuni za kuogea, miswaki na dawa za kusafishia meno ikiwa ni lengo la kuboresha afya zao ziweze kuwa katika hali nzuri.

MKURUGENZI TUNDURU ASHAURI HALMASHAURI YAKE ISHTAKIWE BARAZA LA ARDHI



Na Steven Augustino,
Tunduru.

BAADHI ya wananchi wa kijiji cha Nakayaya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wamegoma kupokea fidia zao walizotakiwa kulipwa na Halmashauri ya wilaya hiyo, ikiwa ni malipo ya fidia ya ardhi na mashamba yakiwemo na majumba wanayoishi ambayo yalipimwa na kuwataka wahame.

Mgomo huo wameufanya takribani miaka mitatu sasa, ambapo maeneo hayo yalipimwa kwa lengo la kuweka makazi kwa mfumo wa ramani ya mipango miji ya wilaya hiyo.

Kufuatia hali hiyo wananchi hao, wamemuomba Waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi,  William Lukuvi kuingilia kati na kuwasaidia kupata haki zao za msingi zinazoonekana kutaka kuporwa na viongozi hao wa Halmashauri, wanaotumia mbinu za ujanja ili kutaka kupora haki za wananchi hao kwa lengo la kujinufaisha wenyewe baada ya kupima, kuyagawa kwa watu wengine na kuwatimua katika maeneo yao.

NGAGA AWATAKA WANAMBINGA KUPANDA MITI KWA WINGI



Na Muhidin Amri,
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga amewataka wananchi wa wilaya hiyo kutumia mvua zinazoendelea kunyesha  katika msimu wa mwaka huu, kwa kupanda miti  kwa wingi  ili kujiongezea kipato baada ya kuonekana zao hilo ni miongoni mwa vyanzo vikubwa vya kukuza mapato na uchumi, kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Senyi Ngaga.
 
Aidha aliwataka waache tabia ya kukata miti hovyo na kuchoma moto misitu hasa nyakati za kiangazi kipindi wanapoandaa mashamba yao, kwa ajili ya shughuli za kilimo huku akiongeza kuwa tabia hiyo imekuwa ikisababisha uharibifu wa mazingira na  virutubisho vya  udongo hupotea.
 
Ngaga alitoa wito huo  mwishoni mwa wiki, alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Amani Makolo wakati walipokuwa katika kazi ya upandaji miti, kata ya Amani Makolo wilayani humo.

MAJAMBAZI YAPORA MILIONI 2.7 MKOWELA TUNDURU



Na Steven Augustino,
Tunduru.

ZUHURA Ngaharo ambaye anaishi katika kijiji cha Mkowela wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, amevamiwa nyumbani kwake na watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi na kumpora fedha shilingi milioni 2.7 za mauzo ya duka lake.

Tukio hilo lilitokea majira ya usiku, Disemba 21 mwaka huu baada ya majambazi hao kumteka na kumlazimisha kuwapatia fedha hizo za mauzo.

Diwani wa kata ya Nakapanya, Kubodola Ambali alisema kuwa katika tukio hilo mama huyo ambaye ni mjane alivamiwa na watu wawili huku wakiwa na silaha ya moto, bunduki  na za jadi ambazo ni visu na mapanga jambo ambalo lilimtisha maisha yake.

Wednesday, December 23, 2015

UKOSEFU WA FEDHA WAKWAMISHA MAENDELEO MBIUWASA



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

IMEBAINIKA kuwa, Mamlaka ya maji safi na Usafi wa Mazingira (MBIUWASA) katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, inashindwa kutimiza mahitaji halisi ya utoaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wateja waliopo katika mji huo, kutokana na miundombinu iliyopo kuwa chakavu.

Vilevile uzalishaji wa maji safi na salama kwa sasa katika mji huo ni mita za ujazo 2,100 kwa siku, ikilinganishwa na mahitaji halisi yanayotakiwa kuzalishwa ni mita za ujazo 3,640 kwa siku ambapo Mamlaka hiyo inashindwa kufikia malengo hayo, kutokana na tatizo hilo linalowakabili.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu umebaini kuwa mji wa Mbinga, una wakazi 43,674 kati ya hao wakazi 26,204 wanaishi katika eneo lilipopita bomba la usambazaji maji huku maeneo mengine yaliyo pembezoni mwa mji, yakiwa hayana mtandao wa maji safi na salama.

Tuesday, December 22, 2015

UVCCM MBINGA WASHIRIKI JUKUMU LA KUFANYA USAFI


Wanachama wa Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wakishiriki katika zoezi la kufanya usafi.


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WANACHAMA wa Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamesema wataendelea kuunga mkono jukumu la kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya mji wa Mbinga, ili kuweza kuepukana na magonjwa yatokanayo na uchafu.

Aidha walieleza kuwa katika kuhakikisha kwamba jambo hilo linakuwa endelevu ndani ya mji huo, watahamasisha watu wengine kufanya hivyo na ni wajibu kwa kila mtu kuzingatia usafi katika eneo analoishi na sio kutupa taka hovyo.
 
Wanachama wa UVCCM wilayani humo, walisema hayo walipokuwa wakihojiwa na mwandishi wa habari hizi wakati walipokuwa wakifanya usafi kuzunguka Ofisi za CCM wilaya na maeneo mengine, ya uwanja wa mpira wa miguu ambao humilikiwa na chama hicho.

“Jukumu la usafi ni letu sote wananchi, sisi vijana tumeungana kwa pamoja kufanya kazi hii katika eneo hili, tunawaomba wananchi wengine watekeleze kwa vitendo suala hili ambalo ni muhimu mbele ya maisha yetu ya kila siku”, walisema.

Monday, December 21, 2015

MKUU WA MKOA IRINGA NA WENZAKE WAFUNGIWA OFISINI





IRINGA.

ZAIDI ya vijana 50 wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Iringa mjini, wanaojiita “wafia chama” kwa zaidi ya saa mbili juzi waliwafungia ndani ya Ofisi za Chama hicho mkoa wa Iringa wajumbe wa kamati ya siasa ya mkoa huo, akiwemo na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu wakishinikiza aachie ngazi.

Msambatavangu anatuhumiwa na baadhi ya makada wa chama hicho, kukihujumu chama jimbo la Iringa mjini wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu, jambo walilosema limesababisha wapoteze kata 14 kati ya 18 na jimbo hilo kwa mara nyingine tena, kwenda kwa Mchungaji Peter Msigwa wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).  

Wengine waliokutwa na kadhia hiyo ni pamoja na Mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza, Kaimu Katibu wa CCM mkoa wa Iringa Elisha Mwampashi, Katibu Mwenezi wa CCM mkoa wa Iringa, Dokta Yahaya Msigwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi mkoa wa Iringa, Ephraim Mhekwa.

Wengine ni pamoja na aliyekuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Mufindi Kaskazini, Mahamudu Mgimwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kilolo, Joseph Muhumba.