Meno ya Tembo. |
Na Mwandishi wetu,
Songea.
JANATI Haji (32)
mkazi wa kijiji cha Rwinga wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, ametiwa mbaroni
baada ya kukamatwa na meno sita ya Tembo, ambayo alikuwa anayasafirisha kwa
kutumia pikipiki, akitokea katika kijiji hicho kwenda Songea mjini, mkoani humo.
Kamanda wa polisi
wa mkoa huo, Mihayo Msikhela akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa
alisema, tukio hilo lilitokea juzi katika katika kijiji hicho.
Msikhela alisema
kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio askari ambao walikuwa doria, waliweza kufanikiwa
kumkamata mtuhumiwa huyo, akiwa na meno hayo ambayo aliyabeba kwenye pikipiki
yenye namba ya usajili, T 448 CZT aina ya Sanlg.
Alifafanua kuwa Haji
alikuwa akiyasafirisha meno hayo ya Tembo, kwenda Songea ambako inadaiwa ndiko
alikokuwa anatarajia kuyauza kwa mtu anayemjua yeye, ambapo upelelezi
unaendelea kufanyika, ili kuweza kujua ni nani ambaye alikuwa akimpelekea kwa
ajili ya kumuuzia.
Polisi kwa
kushirikiana na maafisa wa idara ya wanyama pori, wanafanya jitihada ili kupata
thamani ya nyara hizo na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani wakati wowote, mara
tu upelelezi utakapokamilika.
Kamanda Msikhela
alisema kuwa jeshi la polisi mkoani Ruvuma, bado linaendelea na msako mkali ili
kuwabaini watu wanaojihusisha na biashara hiyo, kwenye mbuga ya wanyama ya Selou
iliyopo mkoani humo, ambapo tembo wengi huuawa.
No comments:
Post a Comment