Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MWENYEKITI wa maandalizi ya sherehe za miaka 38 ya Chama
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Mbunge wa Songea mjini, Dokta Emmanuel
Nchimbi amesema, chama chake kina kila sababu ya kushinda kwa kishindo kwenye
uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, kwa kuwa kina mfumo na muundo
imara.
Akizungumza muda mfupi baada ya maadhimisho hayo mjini
Songea, Dokta Nchimbi alisema kuwa chama hicho, hakina tatizo la kimfumo wa
muundo na kuongeza kuwa ushindi ni lazima.
“Chama hakina tatizo la muundo wala mfumo, tutakachofanya ni
kubadilisha mikakati tu ili kujihakikishia ushindi katika uchaguzi ujao”,
alisema.
Akizungumzia kuhusu kauli ya Mwenyekiti wa chama hicho taifa,
Rais Jakaya Kikwete kuwataka viongozi wa chama kuwatembelea wanachama na
kushawishi wanachama wapya, alisema CCM ni chama kikubwa na ndani yake
wapo viongozi waliolala ambao mwenyekiti wa taifa aliwakumbusha kuamka na
kufanya kazi.
“Chama hakiwezi kuwa na maisha marefu kama viongozi katika
ngazi zote hawajitumi, katika jeshi kubwa kama hili la CCM wapo watu ambao
lazima wasukumwe na ndiyo hawa mwenyekiti wetu wa taifa, aliwasukuma kupitia
hotuba yake.
Alifafanua kuwa wanatakiwa kuamka na kufanya kazi kwa
bidii ili kukiwezesha chama kushinda kwa kishindo, kama ambavyo kimekuwa
kikishinda tangu kuanza kwa siasa za vyama vingi.
Dokta Nchimbi aliishukuru Halmashauri kuu ya chama kwa kuweza
kuuchagua mkoa wa Ruvuma, kuwa mwenyeji wa maazimisho ya miaka 38 ya chama
hicho na kueleza kuwa miaka mingi mkoa huo umekuwa ngome imara ya chama cha
mapinduzi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho
alisema chama chake kimeshaanza kujipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu na
kuweka mikakati ambayo itakipatia ushindi mnono.
“Nimeshawaagiza viongozi wa chama katika ngazi ya mkoa na
wilaya kuanza vikao kwa ajili ya kuweka mikakati thabiti ya ushindi, katika
uchaguzi mkuu ujao”, alisema.
Hata hivyo aliongeza kuwa, chama katika mkoa wake tayari
kilishaanza mikakati ya kujitegemeza ikiwa ni kufuata agizo la Mwenyekiti huyo wa
taifa, ambapo tayari kimejipanga vyema kuendeleza vyanzo vyake vya mapato
pamoja na kuanzisha vyanzo vipya kwa ajili ya kukifanya kijitegemee.
No comments:
Post a Comment