Na Mwandishi wetu,
Songea.
MWALIMU mmoja ambaye anafundisha shule ya msingi Kaijere, kijiji
cha Namabengo wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Shaibu Niali (30) amekutwa akiwa
amefariki dunia na mwili wake ukining’inia chumbani kwake, baada ya kujinyonga
kwa kutumia khanga.
Habari zilizopatikana mjini hapa, na kuthibitishwa na Kamanda
wa Polisi mkoa huo, Mihayo Msikhela alisema kuwa tukio hilo lilitokea Februari
14 mwaka huu, majira ya usiku kwenye chumba chake alichokuwa analala.
Msikhela alifafanua kuwa mnamo majira ya saa moja usiku, Niali
kabla hajajinyonga alimpigia simu dada yake aitwaye, Asia Niali mkazi wa Majengo
Manispaa ya Songea, kwa kumjulisha kuwa anaumwa sana akimuomba aende haraka kijijini
Namabengo, akamuone na ampeleke nyumbani kwa mama yake mzazi kijijini Lusewa
wilayani humo.
Alifafanua kuwa marehemu huyo, kwa muda mrefu alikuwa ana
ugomvi mkubwa na mke wake ambaye baadaye walilazimika kutengana, lakini alionekana
kutokubali kukaa na watoto, jambo ambalo lilikuwa linaleta ugomvi mara kwa mara
kati ya wandani hao wawili.
Niali wakati anampigia simu huyo dada yake akimtaka aende kumuona,
tayari alikuwa ameandaa Khanga ya kujinyongea, na panga kwa lengo la kutaka
kwenda kumcharanga kwanza mke wake, ambaye anaishi mbali kidogo na nyumba yake
ndipo arudi na kuchukua maamuzi hayo magumu.
Msikhela aliongeza kuwa dada yake baada ya kupigiwa simu
ambaye ni Asia, alichukua uamuzi wa kuwasiliana na majirani, ambao walikuwa
wanaishi na mwalimu huyo kwa lengo la kujua kipi kilichomkuta kaka yake, ndipo
majirani hao wakaenda nyumbani kwa Niali, na kumkuta akiwa amejinyonga.
Baada ya kuona hali hiyo majirani waliwasiliana na uongozi wa
serikali ya kijiji cha Namabengo, na kutoa taarifa kituo cha Polisi wilaya ya
Namtumbo, ndugu na jamaa wa marehemu huyo.
Hata hivyo Kamanda huyo wa polisi mkoani Ruvuma, alieleza
kuwa polisi walipopata taarifa juu ya tukio hilo, walikwenda haraka huku wakiwa
wameongozana na daktari kwa ajili ya uchunguzi wa mwili wa marehemu huyo, ili
kuweza kuthibitisha juu ya kifo chake.
No comments:
Post a Comment