Na Thobias Mwanakatwe,
ZOEZI la uandikishaji wapigakura katika Daftari la Kudumu la
Wapigakura limeanza katika Mkoa wa Njombe, huku likikabiliwa na changamoto
nyingi, ikiwamo mashine za Biometric Voter Registration (BVR) kushindwa
kutambua watu wenye vidole vyenye michilizi.
Kujitokeza kwa kasoro hizo kumekuja siku tatu tangu
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe,
alipoeleza kuwa amenasa nyaraka zinazoonyesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec),
ilishauriwa na mtaalam kutoka Marekani kwamba Tanzania haijawa tayari kwa
teknolojia ya BVR.
Mwenyekiti wa Nec, Jaji mstaafu Damian Lubuva, akizungumza na
NIPASHE alisema zoezi la uandikishaji limeanza katika mkoa wa Njombe na kwamba
viongozi wa tume hiyo wapo kwa ajili ya kusimamia kuhakikisha kunakuwa na
mafanikio.
Jaji Lubuva alipoulizwa kama tume imeanza na BVR ngapi,
alisema suala hilo hawezi kulijibu. Hivi karibuni kuriripotiwa kuwa Nec imepata
BVR 250 tu kati ya 8,000 zinazotakiwa.
“Nipo Njombe ndiyo tumeanza zoezi la kuandikisha, suala
la kwamba tumeanza na BVR ngapi sina jibu, kwanza nipo kwenye
kikao,”alisema Lubuva na kukata simu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Nec, Julius Malaba, alisema
uzinduzi rasmi wa uandikishaji katika mkoa wa Njombe utafanyika leo.
Malaba alisema dosari ambazo zimeelezwa kujitokeza
watazitolea ufafanuzi na kuzitafutia ufumbuzi.
Kasoro nyingine zilizojitokeza ni uchache wa vifaa,watoa
huduma waliopewa jukumu hilo kushindwa kutumia mashine na kulazimika kutumia
muda mwingi kumwandikisha mtu mmoja hali inayotia wasiwasi kwamba huenda siku
saba zilizopagwa kufanyika kwa kila mkoa kushindwa kufikia malengo.
Uandikishaji huo ulianza jana katika Halmashauri ya Mji wa
Makambako na mamia ya wananchi wakijitokeza katika vituo vya kujiandikisha
lakini baadhi yao walijikuta wakikwama kutokana na mashine za BVR kushindwa
kuwatambua kutokana na aina ya vidole walivyokuwa navyo.
Mmoja wa wakazi wa mji wa Makambako, Orahp Mhema, alisema
katika vituo walivyoenda kujiandikisha wameshidwa kuingiza maelezo yao ya
kibaolojia kwa sababu mashine zinazotumika kushindwa kutambua vidole vyao
kutokana na mikono yao kuwa na michilizi inayotokana na shughuli za kila siku,
ikiwamo kilimo.
Alisema katika zoezi hilo kuna wasiwasi wa watu wengi
kushindwa kuandikishwa kutokana na muda wa siku saba uliopangwa kuwa
mdogo hasa ikizingatiwa kuwa waandikishaji wanatumia muda mrefu kuhudumia mtu
mmoja. Mhema alisema mbali na changamoto ya mashine kufanyakazi taratibu
pia katika zoezi hilo kumejitokeza tatizo la watoa huduma kushindwa kuzitumia
mashine kikamilifu kutokana na elimu ya kutumia mashine hizo kutowafukia
mapema.
"Katika zoezi hili wananchi wamehamasika kujiandikisha
lakini wanakwamishwa na mashine hizo kufanya taratibu na baadhi yao kushindwa
kuzitumia kikamilifu na nimeshuhudia mmoja akishindwa kubonyeza baadhi ya
batani katika mashIne," alisema Mhema.
Aliongeza : "Watu wengine wamechukuliwa taarifa nyingine
kwa kuwa vidole vyao vimeshindwa kutambuliwa na mashine hizo kwa kuwa inamikwaruzo
mbalimbali inayotokana na ufanyaji wa kazi za kila siku," aliongeza.
Watu walioshindwa kutambuliwa na mashine wengi wao wamejaribu
kurudia zaidi ya mara moja, baadhi yao mashine zimekubali na wengine
zimeshindwa kabisa kuwatambua.
Naye Sifaely Msigala alisema licha ya wananchi
kujitokeza kwa wingi, lakini wameshindwa kufanikiwa na kukwama kuendelea na
shughuli zao kutokana na kushinda mda mrefu katika vituo vya uandikishaji
wa daftari hilo.
Alisema kama kasi ya mashine hizo itaendelea kama ilivyo kuna
uwezekano mkubwa zoezi hilo kushindwa kufanikiwa kwani wananchi wengine
watakuwa wameshindwa kuandikishwa.
Februari 12, mwaka huu, Nec ilikutana na vyama vya siasa 21 ,
ambao ni wadau muhimu katika suala zima la uchaguzi na agenda kuu ilikuwa
kuzungumzia mfumo wa BVR. Nec ilitoa taarifa ya jinsi zoezi la majaribio katika
baadhi ya kata za majimbo ya Kawe, Kilombero na Mlele lilivyoendeshwa na
changamoto zilizojitokeza na matarajio ya kuendesha katika mikoa ya Lindi,
Ruvuma na Njombe, lakini kutokana na uhaba wa vifaa wataanza na wa
Njombe.
Katika mkutano huo, Jaji Lubuva alisema vifaa vilivyopo
ni 250 na kwamba 7,750 vinasubiriwa ili kufanikisha zoezi hilo kufanyika
nchi nzima.
Kuhusu fedha, alisema zimetolewa asilimia 50 na wana imani
kubwa serikali itatoa kiasi kilichobaki kwa wakati.
Kwa upande wa ratiba, alisema itawekwa wazi baada ya kumaliza
zoezi la Njombe na vifaa vinavyosubiriwa kuwasili.
Katika moja ya maelezo ya Tume huko nyuma ni kuwa wangetoa
elimu na taarifa mbalimbali kupitia tovuti yao, lakini hadi sasa ina taarifa za
mwaka 2007 na majibu ya Mwenyekiti ni kuwa kwa sasa wanaifanyia kazi.
CHADEMA WAZUNGUMZA
Nacho Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kisema
kimebaini kasoro mbalimbali zilizojitokeza kwenye mji wa Makambako.
Dosari hizo zimebainika baada ya Naibu Katibu wa
Chadema Bara, John Mnyika na viongozi wengine wa chama hicho kufanya ziara ya
kutembelea kwenye vituo vya uandikishaji
Mnyika alitaja dosari walizozibaini kuwa ni mashine za BVR
kutofanya kazi kwa zaidi ya saa sita na kugoma kuchukua alama za vidole sugu
ambazo zimetokana na kazi ngumu.
Alivitaja vituo ambavyo mashine zilizogoma kufanya kazi kuwa
ni cha Malombwe na Liamkena ambako uandikishaji ulikuwa ni wa kusuasua na
kusababisha watu watano kuandikishwa kwa saa nne.
Februari 12, mwaka huu, Nec ilikutana na vyama vya siasa 21 ,
ambao ni wadau muhimu katika suala zima la uchaguzi na agenda kuu ilikuwa
kuzungumzia mfumo wa BVR. Nec ilitoa taarifa ya jinsi zoezi la majaribio katika
baadhi ya kata za majimbo ya Kawe, Kilombero na Mlele lilivyoendeshwa na
changamoto zilizojitokeza na matarajio ya kuendesha katika mikoa ya Lindi,
Ruvuma na Njombe, lakini kutokana na uhaba wa vifaa wataanza na wa
Njombe.
Katika mkutano huo, Jaji Lubuva alisema vifaa vilivyopo
ni 250 na kwamba 7,750 vinasubiriwa ili kufanikisha zoezi hilo kufanyika
nchi nzima.
Kuhusu fedha, alisema zimetolewa asilimia 50 na wana imani
kubwa serikali itatoa kiasi kilichobaki kwa wakati.
Kwa upande wa ratiba, alisema itawekwa wazi baada ya kumaliza
zoezi la Njombe na vifaa vinavyosubiriwa kuwasili.
Katika moja ya maelezo ya Tume huko nyuma ni kuwa wangetoa
elimu na taarifa mbalimbali kupitia tovuti yao, lakini hadi sasa ina taarifa za
mwaka 2007 na majibu ya Mwenyekiti ni kuwa kwa sasa wanaifanyia kazi. Chanzo
Nipashe.
No comments:
Post a Comment