Tuesday, February 24, 2015

MFUKO WA KOROSHO WAPONGEZWA KWA JITIHADA YA KUENDELEZA ZAO HILO

Mwenyekiti wa mfuko wa kuendeleza zao la korosho Tanzania (WAKFU) Athuman Nkinde, akizungumza na wakulima wa kijiji cha Litumbakuhamba kata ya Lituhi (hawapo pichani) wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, ambapo alikuwa akiwahamasisha kuzalisha zao hilo kwa wingi ili kuweza kuondokana na umasikini.
Na Kassian Nyandindi,

Nyasa.

MWENYEKITI wa Halmashauri wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Oddo Mwisho amepongeza jitihada zinazofanywa na Mfuko wa kuendeleza zao hilo Tanzania (WAKFU) kwa kuwapatia mikorosho mipya wananchi wake, ili waweze kuzalisha zao hilo kwa wingi na kuinua uchumi wa wilaya hiyo.

Aidha Mwenyekiti huyo amewataka wakulima wa zao hilo wilayani humo, kuhamasisha wakulima wenzao kushiriki kikamilifu, katika uzalishaji wa zao hilo jambo ambalo litawafanya waweze kuwa na kipato ikiwemo pia kuondokana na umasikini.  

Mwisho alisema hayo alipokuwa mgeni rasmi kwenye mkutano wa kuhamasisha upandaji wa miche bora ya korosho, uliofanyika katika kijiji cha Litumba kuhamba kata ya Lituhi wilayani humo, ambao ulihudhuriwa na baadhi ya viongozi wa mfuko wa kuendeleza zao hilo hapa nchini.

“Ndugu zangu wakulima, ninyi ndio mabalozi wakuhamasisha wananchi wenzenu wazalishe zao hili kwa wingi kwa maendeleo ya wilaya yetu, tunapotoka hapa tuondoke na sura mpya kila mmoja ajifikirie kuweka jitihada katika uzalishaji wa zao hili, kwa manufaa ya sasa na baadaye”, alisema Mwisho.


Kadhalika aliwataka wakulima hao kuwa na maandalizi, juu ya uendelezaji wa kilimo cha korosho wilayani Nyasa na sio wakati wote, kutegemea serikali au wahisani mbalimbali.

“Tuonyeshe upya wetu kwa mageuzi ya kiuchumi, tuhakikishe tunalima kwa kasi kubwa kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo ninyi wenyewe mmeona jinsi gani mfuko wa WAKFU, unavyothamini wakulima wa korosho hapa nchini”, alisema.

Awali akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa WAKFU Tanzania, Athuman Nkinde alisema kuwa madhumuni ya mfuko huo ni kuratibu maendeleo ya tasnia ya korosho hapa nchini, ikiwemo kuwainua wakulima wake kwa kuwapatia bure miche ya zao hilo na ruzuku katika pembejeo za kilimo. 

Nkinde alifafanua kuwa hili linatokana na mwongozo wa serikali, ambao uliagiza bodi za mazao ikiwemo ya korosho (CBT) kujikita zaidi katika shughuli za usimamizi wa kisekta, ikiwemo kugharimia mafunzo na hata huduma za ugani kwa wakulima wake.

Alisema, huduma za ugani zinahusisha upelekaji wa tekinolojia zinazotafitiwa na kugunduliwa na taasisi za utafiti kwa walengwa, yaani wakulima na wabanguaji wa zao hilo kwa kuwapatia elimu ya kilimo bora na matumizi sahihi ya pembejeo.

Hata hivyo Mwenyekiti huyo alibainisha kuwa, mfuko umekuwa na jukumu la utafutaji wa masoko ndani na nje ya nchi kwa kuzingatia sifa ya ubora wa korosho kwa kufanya pia matangazo, ili iweze kujulikana kwa walaji na hivyo nchi kupata faida.

No comments: