Maurus Zenda ambaye aliambulia kipigo kikali, baada ya kutuhumiwa kuwa ni mshirikina na kumficha mtoto. |
Hilda Pilly, ambaye anatuhumiwa kumficha mtoto katika mazingira ya ushirikina. |
Na Stephano Mango,
Songea.
LICHA ya serikali kukemea wakati wote raia kuacha kuchukua
sheria mkononi, hali hiyo imekuwa kinyume kwa baadhi ya wakazi wa kijiji cha Muungano
zomba, kata ya Kilagano wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, ambapo Hilda Pilly (79)
na Maurus Zenda (46) wamenusurika kuuawa baada ya kushambuliwa kwa mapanga na
rungu, wakidaiwa kuwa ni wachawi.
Shambulio hilo lilifanywa na kundi la watu wenye hasira kali,
ambao imeelezwa kuwa ni wanandugu kutoka katika kijiji hicho, mapema majira ya
asubuhi Februari 3 mwaka huu, kwa madai kuwa Hilda na Maurus wamemficha mtoto
Adam Mselewa (4) katika mazingira ya ushirikina.
Aidha kufuatia hali hiyo walijeruhiwa vibaya sehemu
mbalimbali za miili yao, kutokana na kipigo walichokipata na kulazwa katika hospitali
ya mkoa Songea, huku wakiwa katika hali mbaya.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alifafanua
kuwa watuhumiwa kumi wamekamatwa ambao walihusika na tukio hilo, aliwataja kwa
majina ambao ni; Ambros Mselewa (24) ambaye ni baba mzazi wa mtoto aliyepotea, Maria
Zenda (45) Lameck Zenda (22) Pautas Komba (24) Fredy Mende (24) Gerold Ngonyani
(27) Odilo Mwingira (21) Shadrack Ngonyani (22) na Hilda Zenda (36).
Alisema kuwa chanzo cha tukio hilo ni kupotea kwa mtoto Adam
katika mazingira ya kutatanisha, na kuhisiwa kuwa walimficha katika mazingira
ya ushirikina ambapo baba mzazi wa mtoto huyo, Ambros Mselewa alikuwa
akishirikiana na hao wenzake kufanya mashambulizi hayo dhidi ya watu hao waliokuwa
wakidai kuwa ni wachawi.
Msikhela alifafanua kwamba, Polisi baada ya kupata taarifa walifika
kwenye eneo la tukio na kuwakuta watu hao wawili, wakiwa wamejeruhiwa vibaya na
jitihada za kuwaokoa zilifanikiwa kwa kuwapeleka hospital ya mkoa Songea ili waweze
kupatiwa matibabu na kunusuru uhai wao.
Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wote wa mkoa wa
Ruvuma, kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake wanapokuwa
na watuhumiwa wahakikishe wanawapeleka kwenye vyombo vya dola.
Kwa upande wake Daktari mfawidhi wa hospital ya mkoa huo, Benedict
Ngaiza alithibitisha kupokea majeruhi hao, na kwamba wamelazwa katika hospital
hiyo kwa ajili ya matibabu zaidi.
No comments:
Post a Comment