Tunduru.
MTOTO mchanga mwenye jinsia ya kike wilayani Tunduru mkoa wa
Ruvuma, amezaliwa katika Hospitali ya wilaya hiyo, huku akiwa na ulemavu ambapo
utumbo wake umejitokeza kwa nje.
Taarifa za tukio hilo ambalo limesisimua baadhi ya wananchi wa
wilaya hiyo, zinaeleza kuwa mtoto huyo ambaye amezaliwa na Bi. Theresia George
(25) lilitokea usiku wa kuamkia Februari 2 mwaka huu.
Wauguzi waliokuwa zamu katika hospitali hiyo, walionesha
kushitushwa na tukio hilo na kuwafanya watoe taarifa za kuomba msaada kwa
madaktari wenzao, ili waweze kupatiwa ufumbuzi zaidi juu ya tukio hilo.
Akizungumzia tukio hilo, mama wa mtoto huyo Theresia George
alisema, yeye asili yake ametokea mkoani Mbeya na sasa anaishi katika kijiji
cha Mtina wilayani Tunduru.
Maafisa tabibu ambao waloshudia tukio hilo, akiwemo mganga
mkuu wa wilaya hiyo Dokta Alex Kazula alisema kuzaliwa kwa mtoto huyo akiwa na
ulemavu huo wa viungo utumbo kutoka nje, ni miongoni mwa matukio ya kawaida ambayo
yamekuwa yakijitokeza hapa duniani.
Dokta Kazula alifafanua kuwa, baada ya tukio hilo yeye kwa
kushirikiana na madaktari wenzake wa hospitalini hapo, walifanya uchunguzi
pamoja na kufanya mawasiliano na madaktari bingwa ikiwa ni lengo na juhudi za
kuokoa maisha ya mtoto huyo.
Alisema wakati hayo yanafanyika, mtoto huyo alipelekwa hospitali
ya misheni Mbesa wilayani humo, ambayo ina dakatari bingwa wa magonjwa ya upasuaji
ambako baadaye mtoto alifariki dunia akiwa ameishi kwa muda wa siku mbili.
Kwa mujibu wa Dokta Kazula, alisema alizaliwa akiwa na
upungufu ambao kwa lugha ya kitaalamu unaitwa (Congnital malfamation) ambao
hutokea wakati wa uumbaji wa viungo vya mwili, vinapokuwa vikitengenezwa au
kuundwa tumboni mwa mama.
“Ukosefu wa baadhi ya viungo vya mwili, hujitokeza wakati
vinapoundwa mtoto akiwa tumboni (Organ genesis) ugonjwa huu, Ophalocele hujitokeza
sehemu yoyote ya mwili”, alisema.
Pamoja na mambo mengine alieleza kuwa, ugonjwa huo huweza
kuathiri viungo mbalimbali vya mwili wa mtoto, na kuleta madhara makubwa katika
moyo, tumbo na kwenye ubongo.
Dokta Kazula aliendelea kusema kuwa miongoni mwa vyanzo vya
matukio ya mtoto kupata ugonjwa wa namna hiyo, husababishwa na mama mjamzito kunywa
pombe kupita kiasi, uvutaji wa sigara pamoja na matumizi ya dawa bila kupata
ushauri wa maafisa tabibu, hasa katika kipindi cha miezi mitatu ya kwanza ya
ujauzito wake.
Hata hivyo mganga huyo aliwataka watu kuacha tabia ya kuwanyanyapaa
wanawake ambao wamekuwa wakijifungua watoto wenye ulemavu,ambao kwa namna moja
au nyingi huwa na mapungufu ya viungo vya mwili.
No comments:
Post a Comment