Na Steven Augustino,
Tunduru.
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida mnyama mkali ambaye ni Fisi
wa ajabu, amevamia kijiji cha Malombe wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, na
kuanzisha tabia ya kuwapigia hodi wakazi wa kijiji hicho nyakati za usiku, na
inapotokea wanafungua mlango huwadhuru kwa kuwajeruhi.
Sambamba na hilo mnyama huyo amekuwa na tabia mpya ya kwenda
kufukua makaburi ya watu ambao wamekuwa wakizikwa, katika makaburi yaliyopo
kijijini hapo.
Kwa mujibu wa taarifa za matukio hayo, imeelezwa kuwa fisi
huyo alianza kuonekana mwanzoni mwa mwezi huu, hali ambayo imekuwa ikiwafanya
wananchi wa kijiji hicho kuishi katika hofu kubwa.
Akizungumzia tukio hilo Diwani wa kata ya Mlingoti Magharibi,
Mchemela Abdallah alisema kuwa baada ya kupata taarifa hizo, alizipeleka katika
ofisi ya idara ya ardhi na wanayamapori wilayani humo, ili wawasaidie kumuondoa
fisi huyo kabla hajasababisha madhara makubwa kwa wananchi.
Mchemela alilitaja tukio la kusisimua la fisi huyo kufukua
kaburi la marehemu, Said Daimu Mjase ambaye aliyefariki na kuzikwa katika
makaburi yaliyopo kijijini hapo, kuwa lilitokea Februari 3 mwaka huu.
Alisema sambamba na mnyama huyo kufanya matukio hayo, pia
amekuwa akishika mbuzi, mbwa ambapo hadi sasa amekwisha kamata mifugo ya watu wa nne ambao ni wakazi wa kijiji cha Malombe.
Alipotakiwa kuzungumzia matukio hayo Kaimu afisa wanyamapori,
hamashauri ya wilaya ya Tunduru, Peter Matani pamoja na mambo mengine alikiri
kuwepo kwa matukio hayo na akaongeza kuwa tayari amekwisha peleka askari wa
idara hiyo, ili kumsaka na kumuua fisi huyo kabla hajaleta madhara makubwa kwa
wananchi.
No comments:
Post a Comment