Mtoto Sophia Abdul, ambaye ana tatizo la jicho. |
Na Amon Mtega,
Songea.
MTOTO Sophia Abdul (14) ambaye ana matatizo ya ugonjwa ambao bado haufahamiki jina lake, umejitokeza katika jicho lake la upande wa kulia ambalo limevimba na kujitokeza nje, anaomba msaada wa matibabu ili aweze kunusuru afya yake.
Sophia anasoma shule ya msingi Lilahi darasa la tano, iliyopo
kata ya Mhukulu wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, amekumbwa na ugonjwa huo ambao
unamletea maumivu makali na kushindwa kwenda shule, kuhudhuruia masomo yake.
Akizungumza na waandishi wa habari, katika ofisi za elimu
wilayani humo mama wa mtoto huyo ambaye alijitambulisha kwa jina la, Joyce
Nyoni alisema mwanae alianza kupatwa na ugonjwa huo tangu mwezi Aprili mwaka
jana, ambapo jicho hilo lilianza kuwasha na kujitokeza uvimbe, ambao kwa
sasa umesababisha kushindwa hata kuona.
Mama huyo alisema anaomba wasamaria wema popote pale walipo,
wamsadie ili mwanae aweze kutibiwa na hatimaye kupona, ili aweze kuendelea na
masomo yake.
Aidha alifafanua kuwa baada ya kuona hali ya mwanae inazidi
kuwa mbaya, alimpeleka katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Ruvuma na kukutana
na madaktari ambao walimwambia kuwa ugonjwa huo, hawataweza kuutibu na kutambua
ni waina gani na nini hasa kinachomsumbua Sophia, badala yake walimtaka atafute
fedha ampeleke katika hospitali ya rufaa ya Muhimbili.
Joyce baada ya kupata maelekezo ya madaktari, aliamua kupita
kuomba msaada kwa wasamaria wema ili kunusuru maisha ya mwanae kwa kuwa yeye
mwenyewe hivi sasa hana uwezo wa kifedha na kwamba baba wa mtoto huyo, Abdul
Rashid alimtelekeza toka akiwa na umri wa mwaka mmoja.
Alisema kufuatia hali hiyo mwanae hajahudhuria masomo toka
walipofungua shule mapema Januari mwaka huu, jambo ambalo linaweza kumrudisha
nyuma katika maendeleo yake kimasomo na haki ya kupata elimu.
Kadhalika aliongeza kuwa wakati akiwa katika hospitali hiyo ya
mkoa, aliambiwa na madaktari hao kuwa, pindi atakapopata fedha za matibabu
watamwandikia kibali cha kumruhusu kwenda kupata matibabu huko Muhimbili.
Hata hivyo, mama wa mtoto huyo anawaomba wasamaria wema kutoa
mchango wao wa hali na mali ili aweze kufanikiwa kumpeleka mwanae kwenye
matibabu, kiwango cha fedha kinachohitajika hadi sasa hakifahamu kutokana na
ugonjwa wenyewe kutojulikana ni wa aina gani, ambapo kwa atakayeguswa na tatizo
hilo la mtoto Sophia, watoe michango yao kwa simu namba; 0683115075 ambayo ni ya mama ya mtoto huyo.
No comments:
Post a Comment