Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Chande Nalicho akisisitiza jambo katika mikutano mbalimbali aliyokuwa akiifanya wilayani humo.
|
Na Steven Augustino,
Tunduru.
SERIKALI wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, imemtaka
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Tinna Sekambo kuongeza nguvu katika
usimamiaji wa zoezi la upandaji wa mikorosho mipya kwa wakulima wa zao hilo wilayani humo,
ili waweze kuondokana na hali ya kipato duni walichonayo sasa, na hatimaye waweze
kusonga mbele kimaendeleo.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho, alitoa agizo hilo
wakati akimkabidhi miche ya mikorosho kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo,
Chiza Marando ikiwa ni muda mfupi baada ya mkuu huyo wa wilaya, naye
kukabidhiwa miche 30,000 yenye thamani ya shilingi milioni 85 kutoka kwa
mwenyekiti wa mfuko wa kuendeleza zao la korosho Tanzania. (WAKUF)
Aidha Nalicho alimweleza mkurugenzi huyo kuwa ili
kufanikisha ugawaji wa miche hiyo kwenda kwa wakulima, maafisa ugani wanatakiwa
kwenda katika vituo vyao vya kazi vijijini, na kuacha kukaa maofisini.
Mkuu huyo wa wilaya ya Tunduru, aliahidi kufanya ziara ya
ufuatiliaji juu ya zoezi hilo, la upandaji wa mikorosho ambalo linaendelea wilayani
humo kwa lengo la kujionea utekelezaji wake.
Awali akimkabidhi miche ya mikorosho hiyo, Mwenyekiti wa mfuko
wa kuendeleza korosho Tanzania, Athuman Nkinde alimweleza Nalicho kuwa mfuko
huo umeazimia kutekeleza kwa vitendo, kauli mbiu ya Kilimo kwanza.
Nkinde alifafanua kuwa mikorosho hiyo ambayo inasambazwa na
kugawiwa bure kwa wakulima wote hapa nchini, imegharimiwa na mfuko huo ikiwa ni mpango wa kuendeleza na
kuongeza uzalishaji wa zao hilo kila mwaka, ambapo matarajio yao ni kusambaza
miche milioni 10 yenye thamani ya shilingi milioni 500 ifikapo mwaka 2015
na 2016.
Alisema miche hiyo husambazwa kwa wakulima, baada ya kufanyiwa
usanifu na wataalamu wa mimea kutoka kituo cha utafiti Naliendele, ambacho
kimeweka matawi yake katika wilaya ya Tunduru, ambacho kinahudumia nyanda za
juu kusini, Mpwapwa ambacho kinahudumia wakulima kanda ya ziwa na Mkuranga
wakulima wa kanda ya Mashariki na kaskazini.
Ili kwenda na ongezeko la uzalishaji, pia mfuko huo umeandaa
utaratibu wa kugawa mashine maalum ambazo zitatumika kuwasaidia wakulima kupulizia
mikorosho yao ili waweze kuongeza uzalishaji.
Sambamba na utekelezaji wa zoezi hilo WAKUF imeandaa
utaratibu wa kujenga viwanda vitatu, ambavyo ujenzi wake utagharimu shilingi bilioni
6 kwa ajili ya Kubangulia korosho za wakulima, kwa lengo la kuziongezea thamani
na kupata bei nzuri sokoni.
Viwanda hivyo vitajengwa katika wilaya ya Tunduru mkoani
Ruvuma, Mtwara, na wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani ambapo ujenzi wake
unatarajiwa kuanza mapema mwaka huu.
Katika makabidhiano hayo, kaimu mkurugezni wa halmashauri ya wilaya hiyo, Chiza Marando aliushukuru mfuko huo kwa msaada wake huku
akimhakikishia mkuu wa wilaya hiyo, Nalicho kuwa halmashauri yake imejipanga katika
kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa na kutekelezwa kwa wakati ili wakulima waweze
kupiga hatua.
Marando alieleza kuwa mbali na zoezi hilo kuwa na changamoto
ya wakulima wengi kutochangamkia fursa hiyo, kwa madai ya kutegemea mikorosho
waliyorithi kutoka kwa babu zao, alisema miche hiyo ina faida nyingi ikiwemo ya
kuzaa katika kipindi cha miaka miwili baada ya kupandwa, na huzaa mazao mengi
kuliko mikorosho ya zamani.
Wakizungumza kwa niaba ya wakulima wenzao, Mussa Nasoro kutoka
kijiji cha Namasakata, Mwajuma Nakayaya na Mussa Kaisi wote wa kijiji cha Mchoteka
kwa nyakati tofauti waliipongeza serikali kwa kuwapelekea mradi huo, na kutoa
wito kwa wakulima wenzao kuchangamkia miche hiyo, ili iweze kuwaletea faida ya
kuvuna mikorosho mingi na hatimaye kusonga mbele kimaendeleo.
Meneja wa kituo cha utafiti wa zao hilo, katika kituo cha
Nakayaya wilayani Tunduru, Said Mawanje aliwaomba viongozi wa mfuko huo kuandaa
utaratibu na kupeleka oda iliyobakia ya uzalishaji wa mikorosho hiyo mapema,
ili kuwawezesha kuandaa na kukabidhi miche hiyo kabla ya mwezi wa kwanza
mwakani.
No comments:
Post a Comment