Yustina Chagaka, Mkuu wa TAKUKURU mkoani Ruvuma.
|
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
HAKIMU wa Mahakama ya Mwanzo, Deusdedith Malembo na Michael Haulle
aliyekuwa askari wa kituo kikuu cha Polisi Songea mjini mkoani Ruvuma, wote kwa
pamoja wameburutwa katika Mahakama ya mkoa huo, kwa kosa la kuomba na kupokea
rushwa.
Watuhumiwa hao wamefikishwa katika mahakama hiyo, baada ya kufunguliwa
kesi ya jinai namba 15/2015 huku ikiendeshwa na mwendesha mashitaka wa TAKUKURU,
Herman Malima mbele ya Hakimu, Simon Kobelo.
Mwendesha mashtaka huyo aliieleza Mahakama kuwa, mnamo
Januari 2 mwaka huu washtakiwa hao waliomba hongo ya shilingi 150,000 kutoka
kwa mlalamikaji mmoja, ili wasimpeleke mahabusu kwa madai kuwa hakuitikia wito
wa mahakama katika kesi ya madai ambayo ilifunguliwa dhidi yake.
Pamoja na mambo mengine, Malima alieleza kuwa siku hiyo ya
tukio watuhumiwa hao walipokea kwanza shilingi elfu hamsini, kwa ahadi kuwa
kiasi kilichobakia shilingi laki moja wangepewa tena Januari 6 mwaka huu,
ambapo baada ya taasisi hiyo kunasa taarifa hizo na kufanya uchunguzi wa kina,
ilibaini kwamba watuhumiwa hao walitenda kosa hilo la kuomba na kupokea rushwa,
ndipo mtego ulipotengenezwa na hatimaye walikamatwa.
Watuhumiwa wote wawili wamekana mashtaka, wapo nje kwa
dhamana ambapo shauri lao litatajwa tena Machi 5 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment