Thursday, February 12, 2015

MAADHIMISHO YA KUZALIWA CCM NA HOFU YA UCHAGUZI MKUU

Padre Baptiste Mapunda.

Na Padre Baptiste Mapunda,

TAREHE mosi  mwezi Februari mwaka huu, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilisherehekea siku yake ya kuzaliwa ikitimiza miaka 38. Kawaida mtu mwenye umri huu sio mtoto tena, bali ni mtu mzima anayepaswa kuwajibika katika maisha yake na ya wenzake.

Sikukuu hii ya kuzaliwa kwa CCM kwa kawaida inafanyika tarehe 5 mwezi Februari  ambapo mwaka huu ingeangukia siku ya alhamisi, lakini cha kushangaza ilirudishwa nyuma na kuadhimishwa siku ya Bwana yaani Jumapili,  kwa sababu zipi  bado hazijulikani, lakini inaruhusiwa.

Mimi binafsi nilibahatika kuwa katika mji huu wa Songea  mkoani Ruvuma, huko ni nyumbani kabisa, “kunyumba”. 

Ni heshima kubwa sana kwa mkoa huo, kupewa  nafasi ya kuandaa sherehe ya kitaifa kama hii,  pia ni nafasi nyeti na kila mkoa inatafuta. Bado haikufahamika kigezo cha kupeleka  sherehe hizi mkoa wa Ruvuma, ambao kimaendeleo bado upo nyuma katika nyanja mbalimbali kaqma vile elimu, afya, miundo mbinu ya barabara maji, umeme, na kipato cha wananchi wake na mwamko katika demokrasia na  siasa za mageuzi.


Umati wa wananchi waliojaa katika uwanja wa maji maji haukuwa haba, lakini kwa upande mmoja  ukipita mitaani uliweza kuona  watu wengi wakiendelea na shughuli zao huku wengine wamefungua maduka, sokoni nako kunafurika watu, boda boda  wamejipanga nakadhalika. 

Nilipojaribu kudodosa baadhi ya wananchi inakuwaje uwanja umefurika na wanasongea wanaonekana barabarani, jibu nililopewa ni kwamba; “watu waliofurika ndani ya uwanja wa maji maji  walikuwa wameletwa na malori na mabasi kutoka katika kila kata ndani ya mkoa huo”.  

“Padre  Mapunda, hawa watu waliofurika hapa uwanjani sio wanasongea pekee, bali wengi wao wametoka mkoa mzima labda na hata kanda ya nyanda za juu kusini. Ndani ya mkoa  kila kata waliletwa watu kumi  na pia shule zote za msingi na sekondari hapa mjini, waliamrishwa lazima wahudhurie na sharti  wafike bila uniform”, alifahamisha  mwananchi mmoja.

Leo hoja yangu sio watu waliofurika tu, nikijua kwamba mkoa wa Ruvuma hauna matukio mengi ya kitaifa kama hayo kwa hiyo tukio kama hilo, wanaruvuma wengi wangelipenda kuhudhuria. Mimi hoja  yangu kubwa leo ni hotuba iliyotolewa na mheshimiwa Rais wetu Jakaya Kikwete, kwa upande wangu hotuba ile ilikuwa imejaa hofu ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Mwezi Oktoba mwaka huu Watanzania, tutapata tena fursa ya kumchagua Rais wetu mpya wa awamu ya tano, ambaye atakuwa mrithi wa Rais tuliyekuwa naye sasa.

Ni wazi huu ni uchaguzi wa kihistoria, kwanza kwa sababu unatanguliwa na kura ya maoni ya katiba mpya iliyopendekezwa ambayo mimi naiita, “katiba haramu ya CCM”. Ni haramu kwa sababu ni katiba iliyotupilia mbali maoni ya wananchi wake chini ya tume ya Warioba na wakapachika  maoni wanayotaka wao wanaccm, kwa nini isiitwe haramu na pandikizi?

Lakini pia  ni  uchaguzi wa kihistoria  kwa sababu ya ukomavu wa mfumo wa vyama vingi, ambapo ukichunguza  nchi yetu hivi sasa ni takribani miaka 20 imepita tangu mfumo wa vyama vingi ulipokubaliwa uwepo na Baba wa taifa, hayati mwalimu Julius Nyerere kinyume na matakwa ya wengi waliokataa.

Vyama vya upinzani vimekomaa kwa kiasi kikubwa, na vinatoa changamoto kubwa sana kwa chama cha mapinduzi kiasi cha kuwa tishio. 

UKAWA unaendelea kuwa tishio kwa chama tawala, pamoja na porojo au propaganda zake zote, umoja huu unaonekana kukomaa kila kukicha. Je mwisho wa umoja huu ni nini? lakini tunajua kwamba Baba wa taifa hayati mwalimu Nyerere alitufundisha kwamba, “umoja ni nguvu”.

Kutokana na nguvu, mbinu na hamasa wanayoionyesha WANAUKAWA, CCM imekumbwa na kihoro juu ya uhai wake hasa wakati huu tunakoelekea uchaguzi mkuu. Hii ilisababisha Mwenyekiti wake wa CCM taifa ambaye ni Rais Kikwete  atoe hotuba ya hofu ya uchaguzi mkuu mwaka huu.

Pamoja kwamba alifurahia umati uliojaa  pale uwanja wa maji maji, ulipambwa na halaiki ya wanafunzi hotuba ya mheshimiwa Rais, hakuficha hisia zake za hofu ya uchaguzi unaokuja.

Mtu aliyesoma saikolojia kidogo, atatambua mara moja kwamba hotuba ya Rais Kikwete kama Mwenyekiti wa CCM taifa ilijaa hofu. “CCM bado ni  imara na tutashinda kwa kishindo, lakini tusibweteke.” Maneno haya ni mazito kwa kiongozi mkuu kama yeye.

Aliendelea kuwaasa wanaccm kwamba, “katika kampeni msichukue kila pesa, pesa zingine zina moto mtakuja kuungua”, alisema. Mwenyekiti huyo alikwepa kabisa kutumia neno la “Escrow” likimaanisha wizi wa mabilioni ya pesa uliotokea hivi karibuni na kusababisha baadhi ya viongozi wa serikali yake kama Mwanasheria mkuu, Waziri wa ardhi na Waziri wa nishati na madini kujiuzuru.

Mimi najiuliza, ile hofu iliyoonekana katika hotuba ya Rais wetu ilipata majibu kule Songea? kwa upande mmoja  sikuona  alama ya mwitikio na hamasa kubwa ya wananchi katika salamu na vibwagizo mbali mbali. 

Bado sijafahamu ni kiashirio  gani wanaruvuma walitoa kwa kiongozi wao hata akaanza kupata hofu. Nionavyo mimi hofu hii inaweza kutokana na ukweli  kwamba viongozi wengi wa CCM na serikali wamezoea kuiona Ruvuma kama sehemu ya kuvuna kura nyingi, lakini huenda walishituka kuona mwamko ni kidogo.

Wakulima wa mahindi wamekuwa na malalamiko kibao juu ya kulipwa pesa zao, ruzuku za mbolea zimekuwa zikitolewa kwa rushwa na pengine  kuchakachuliwa kabisa. Je, hawa wanaruvuma wanaweza kuendelea kukipenda chama chao kama zamani? 

Nimalize kwa kuuliza swali lile lile, je hotuba ya Kikwete  iliyojaa hofu ya uchaguzi msingi wake ni nini kule Songea? na je Mwenyekiti huyu wa CCM taifa anafahamu kwamba hotuba yake,  ilijaa hofu ya uchaguzi mkuu  na  uwezekano wa kuanguka kwa chama chake katika uchaguzi ujao?

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa barua pepe; Frmapunda91@gmail.com

No comments: