Tuesday, February 3, 2015

KATIKA HILI MADIWANI MBINGA TUNAPASWA KUBEBA LAWAMA, TULICHAGULIWA TUZINGATIE KANUNI NA TARATIBU ZILIZOWEKWA


Na Kassian Nyandindi,

DIWANI ni kiongozi ambaye hudumisha maendeleo ya wananchi wake katika serikali za mitaa, ikiwa ni wajibu wake muhimu kwa kiongozi waliyemchagua na wenye kujenga imani naye, katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo mbalimbali kwenye eneo husika ambalo amepewa ridhaa ya kulitawala.

Siku zote diwani akiwa kwenye baraza lililokuwa imara, hupinga vitendo vya rushwa na kuweka misingi imara ambayo hujenga uhusiano mzuri baina ya baraza na wafanyakazi wake, na haya yasipozingatiwa huleta mipasuko isiyokuwa ya lazima na hata mifarakano ambayo husababisha kuharibu wajibu wa kutathmini utendaji kazi wa idara katika halmashauri.

Wahenga wetu husema; Kibuyu kilichokuwa na shimo chini hakiwezi kujazwa na ukipanda nyasi huwezi kuvuna mchele. Maneno haya ni moja kati ya misamiati michache ambayo huelimisha namna tu tunavyotakiwa kuwa makini, katika utekelezaji na utoaji wa maamuzi katika mambo mbalimbali.

Kabla sijaenda mbali makala hii ya uchambuzi, mwandishi wetu anazungumzia juu ya mwenendo wa baraza la madiwani Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, ambao wananchi wake hivi sasa wamefikia hatua ya kulalamikia kwamba wamekosa imani nao, limekosa mvuto na kupoteza mwelekeo katika baadhi ya maamuzi mbalimbali.

Mnamo Januari 23 mwaka huu, Madiwani wa wilaya hiyo walifanya baraza lao lengo ikiwa kujadili, kupitisha na kutoa maamuzi ya kimaendeleo ambayo yaliwasilishwa kwa manufaa ya wanambinga na taifa letu kwa ujumla.

Ninachotaka kuzungumzia hapa licha ya baraza hilo kutekeleza hayo, lakini agenda kuu na mwisho ilikuwa juu ya kutoa maamuzi ya kumwajibisha Afisa elimu msingi wa wilaya hiyo, Mathias Mkali kuhusiana na tuhuma kadhaa walizokuwa wakimtuhumu ambazo zilitolewa na Mkurugenzi wake mtendaji, Hussein Ngaga.


Nilikuwa nikifuatilia kwa karibu juu ya jambo hili, ambalo lilikuwa limegubikwa na mizengwe ya hapa na pale huku baraza likilazimika kuketi kama kamati kwa zaidi ya masaa mawili kujadili hilo, huku watendaji wake na wasikilizaji ambao walikuwepo ndani ya kikao hicho wakitolewa nje kupisha mjadala uweze kufanyika, na hatimaye maamuzi yaweze kutolewa baadaye.

Mvutano mkubwa ulikuwepo kati ya Mkurugenzi huyo na baadhi ya madiwani ambao walikuwa hawaungi mkono juu ya hoja hiyo, ambayo ililenga kumfikisha mahakamani afisa elimu huyo na kumshusha cheo kutokana na sababu kadhaa ambazo ziliwasilishwa ndani ya baraza hilo, ambapo mwishoni walifikia maamuzi tu ya kumvua madaraka (kumshusha cheo) kutoka nafasi hiyo aliyonayo ya ukuu wa idara kwenda kuwa mwalimu mkuu.

Baadhi ya madiwani wachache waliokuwa wakipinga maamuzi hayo walisema ni ubabe tu umetumika katika kuamua hilo na kutozingatia haki, kwa kile walichoeleza kuwa baraza lililopita lilikubaliana kwamba kabla ya kutolewa maamuzi yoyote, ni lazima mtuhumiwa ajieleze mbele ya baraza dhidi ya tuhuma alizokuwa akituhumiwa jambo ambalo lilipingwa na mkurugenzi huyo mtendaji na kufikia hatua ya kuunda tume, hatimaye kutoa maamuzi hayo magumu.

“Kama duniani kila mtu haki yake hupatikana hapa hapa duniani, basi ipo siku tuna imani suala hili litafikia mwisho kwa sababu tokea mchakato wake ulivyoanza na kufikia hatua ya kumwajibisha huyu mtu sio mzuri, baadhi ya taratibu zimekiukwa na hili linatokana tu na madiwani kutokuwa na mshikamano wa dhati kwa sababu ya kutanguliza maslahi yao mbele kuliko ya wananchi waliotuchagua na ndio maana leo tunatoa maamuzi yasiyotenda haki”, walisema.

Wengine walikuwa wakilaumu kwamba tume iliyoundwa na mkurugenzi Ngaga licha ya kwamba sheria inamruhusu kufanya hivyo haijatenda haki, badala yake walishauri ni vyema ingeundwa na watu walio nje ya mkoa huu ili kuweza kutenda haki na kumpatia mtuhumiwa, uhuru wa kujieleza na kutoa vielelezo vyake dhidi ya mambo aliyokuwa akituhumiwa.

Nionavyo, hata kama baraza la madiwani leo hii lina mamlaka ya kumvua madaraka afisa elimu msingi, Bw. Mkali kwenda kuwa mwalimu mkuu bado kuna mambo kadhaa ambayo bado najiuliza; mpaka maamuzi haya yanafanyika na baraza hili la madiwani Mbinga, sasa ni wakati kwa Mamlaka ya nidhamu (TSD) katika halmashauri hiyo na hata ngazi ya juu taifa, kuchunguza ukweli wa jambo hili ili mwisho wa siku wananchi waweze kupata majibu sahihi.

Natambua cheo alichonacho, afisa elimu huyo msingi ni uteuzi ambao ulifanywa na Wizara husika, hivyo ni wakati muafaka sasa nao wakafanya uchunguzi ili kuweza kujiridhisha na suala hili ambalo linaleta malalamiko miongoni mwa jamii, na kuleta mifarakano isiyokuwa ya lazima.

Pia natambua kuna haki kwa mtuhumiwa kukata rufaa sehemu husika, kupinga maamuzi haya yaliyotolewa ili kuweza kutoa mwanya kwa wizara kuunda tume kuja kuchunguza hili na kumpatia nafasi ya kutosha mtuhumiwa kujieleza kwa kina, dhidi ya maamuzi haya yaliyotolewa na baraza hilo la madiwani.

Madiwani wa Mbinga leo hii wadau wa elimu wanawanyoshea kidole, huenda hamjatenda haki kutokana na kumpoteza mtu ambaye ameinua wilaya yenu kielimu huku sasa iking’ara kitaifa, ambayo awali ilikuwa katika sifa mbaya ikishika mkia katika kufaulisha watoto mashuleni.

Katika vikao vya tathmini ya elimu ambavyo kila mwaka mmekuwa mkivifanya, Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga muda mwingi nilikuwa nikimnukuu akionekana kupongeza, huku akiapa yeyote atakayeonekana kuharibu mipango na mikakati iliyowekwa juu ya ufaulishaji watoto darasa la saba atachukuliwa hatua za kisheria, lakini sasa ni kichekesho ambapo mikakati ile ambayo ilibuniwa na afisa elimu huyo ambaye leo anapigwa vita, tayari imeanza kudorola na hakuna jitihada zinazoonekana kuzaa matunda.

Wadau wa elimu wanasema hii ni dhambi ambayo itaendelea kutafuna viongozi walioanzisha malumbano haya, na kizazi hiki ambacho kinadondosha machozi kila kukicha huenda baadaye kikawajengea laana ambayo mwisho wa uhai hapa duniani, ipo siku pale watakapotukumbuka watatamani hata makaburi yetu yachapwe viboko, na maneno yenye laana yakitamkwa.

Bila shaka ni jambo ambalo linajulikana kwa kila mtu, elimu wilayani Mbinga ilianza kuimarika lakini sasa inasikitisha tunakoelekea sio kuzuri kuna kila sababu ya kujutia kwa hiki tulichofanya, kwa sababu tu ya kutanguliza maslahi yetu mbele kuliko kujali kwa kujiongeza mbele juu ya athari zinazoweza kujitokeza baadae kwa watoto wetu, ambao wamezaliwa bado wachanga na hata wale waliokuwa tumboni ambao nao watahitaji elimu iliyokuwa bora.

Natamka haya kwa sababu mipango na mikakati ambayo ilibuniwa na Bw. Mkali katika kuendeleza elimu wilayani humo, tayari imevurugwa na malumbano haya walimu mashuleni wameanza kurudisha moyo wa kufundisha darasani, nina hakika hata matokeo ya darasa la saba mwaka huu huenda yakashuka tusipokuwa imara.

Diwani kuwa mkweli, wazi na mwajibikaji katika mambo mbalimbali, kwa kuzingatia taratibu au sheria bila kuonea mtu ndio silaha pekee ya maendeleo kwa kizazi hiki, ambacho kila siku kinatutegemea katika kukiongoza.

Mashirika binafsi na ya serikali ulimwenguni kote yanashughulika zaidi namna ya kuboresha maisha ya wananchi wake, na kuzingatia utendaji kazi uliokuwa bora hasa katika sekta ya elimu ambayo ndiyo mhimili mkuu wa maendeleo ya binadamu kutoka katika tabaka la watu wajinga wasiojua Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).

Wepesi wa usuluhishaji wa matatizo uzoefu wangu serikali nyingi za mitaa nchini huchelewesha kumaliza matatizo waliyonayo, kutokana na kuelekeza nguvu na rasilimali zao kwenye matatizo ambayo yamekuwepo kwa muda mrefu mara nyingine yalisababishwa na madiwani waliowatangulia, hivyo kubadili mtindo huu halitakuwa jambo rahisi.

Rais wa 26 wa Marekani, Theodore Roosevelt aliwahi kusema, na nukuu; “In a moment of decision the best thing you can do is the right thing to do. The worst thing you can do is nothing”.

Tunapaswa kutoa maamuzi sahihi kila mmoja awajibike ipasavyo katika nafasi yake kwa mujibu wa sheria na taratibu za serikali zilizopo, kwa kujenga msingi wa kiuchumi na kisasa wa taifa, na kutekeleza sera ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Kadhalika serikali za mitaa nchini Sri Lanka imekuwa na tabia ya kushindania zawadi na utambuzi katika utendaji kazi, kulingana na idadi ya watu wao na sio kuendekeza malumbano kazini, hii ni njia nzuri ya kuhimiza baraza na wafanyakazi wake kuboresha utendaji wao.

Pia nakumbuka Waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa katika hotuba zake alikuwa akisisitiza suala la ushirikiano kazini hasa kwa halmashauri ambazo huundwa na kamati mbalimbali, zenye wajumbe wakiwemo madiwani ambao wamechaguliwa na wananchi kusimamia utekelezaji wa majukumu husika.

Lowassa alikuwa akisema umezuka mtindo wa mahusiano yasiyoridhisha baina ya viongozi wa juu katika halmashauri na wakuu wao wa idara, huku wengine kati yao wakiishangaza jamii wakiimba wimbo halmashauri ni yangu, yangu, yangu…………. huku wengine wanasema shauri yao na kundi jingine limekuwa watazamaji wakijisemea moyoni kwamba hayawahusu. 

Katika hali hii naweza nikasema hatuwezi kufikia malengo tuliyojiwekea endapo viongozi au watendaji wa ngazi hata ya chini tutakuwa hivi, kazi iliyopo mbele yetu inahitaji ushirikiano na kutambua majukumu na mchango wa mwenzako. Hivi kweli kama tuna nia njema kwa umma wa watanzania, kwa nini tugombanie fito wakati tunajenga nyumba moja? 

Serikali inataka kusikia mahusiano mema katika ngazi zote za utawala, yenye lengo moja la kufanikisha malengo tuliyojiwekea pamoja na kwamba kila mmoja wetu anayomajukumu aliyopangiwa kuyatekeleza, nasema tena tushirikiane katika kulifikisha jahazi hili la maendeleo ya wanambinga ambalo sasa linasakamwa na mawimbi mengi baharini, huenda likapinduka kabla ya kuwasili mwisho wa safari yake hapa duniani.

Mungu ibariki Tanzania, mwandishi wa makala haya ni mpenda amani na maendeleo katika jamii, anapatikana kwa barua pepe; nyandindi2006@yahoo.com au simu namba 0762 578960.

No comments: