Sunday, February 22, 2015

SONAMCU WAGOMEA MKUTANO BAADA YA KUKOSA POSHO



Na Nathan Mtega,
Songea.

MKUTANO Mkuu maalumu wa Chama cha ushirika cha wakulima wa tumbaku Songea na Namtumbo, mkoani Ruvuma (SONAMCU) uliopangwa kufanyika Februari 18 mwaka huu umeshindwa kufanyika, baada ya Wajumbe wa mkutano huo kugoma baada ya kuambiwa na uongozi wa juu wa chama hicho kwamba,  hakuna fedha ya posho kwa ajili ya kujikimu siku mkutano huo ulipotakiwa kufanyika.

Hatua hiyo ya wajumbe wa mkutano huo kugomea, ilianza baada ya kutokea kwa mvutano miongoni mwao na uongozi wa juu wa chama hicho mjini hapa, pamoja na Meneja wa SONAMCU,  Christopther Ugulumo ambaye alitoa taarifa kwa wajumbe kuwa mkutano huo hautakuwa na posho na yeye hakuitisha bali umeitishwa na mrajisi wa vyama vya ushirika mkoani humo.

Baada ya kauli hiyo, ndipo wajumbe wa mkutano huo walipoanza kueleza kuhusu msimamo wao wa kutoshiriki katika mkutano mpaka suala la malipo ya posho stahiki yatapowekwa wazi, na kwamba wakati malumbano hayo yakiendelea kwa muda wa zaidi ya dakika 45 ndipo mrajisi msaidizi alishauri kupigwa kura ili kujua wanaokubali mkutano ufanyike na posho zitalipwa baada ya fedha kupatikana, na wanaokataa kufanyika kwa mkutano mkuu wa uchaguzi.


Wakati zoezi hilo likiendelea baadhi ya wajumbe waliamua kutoka nje ya ukumbi wa mkutano huo, huku Mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika, Ally Bango akikaa kimya na kushindwa kutoa maamuzi kwa kujenga hoja ya kuwashawishi wajumbe wakubali kufanyika kwa mkutano na malipo ya posho zao stahili yatafanyika baadae, kwa sababu kushindwa kufanyika kwa mkutano huo wa uchaguzi kunaweza kukigharimu chama hicho kwa mujibu wa sheria za ushirika, na jukumu hilo la kushauri likifanywa na kaimu meneja wa SONAMCU Christopher Ugulumo pamoja na maafisa ushirika wa wilaya za Namtumbo, Mbinga na Songea bila mafanikio.

Kitendo cha mwenyekiti kukaa kimya na kushindwa kutoa maamuzi, huku akijua madhara yanayoweza kukipata chama kwa kutofanya mkutano mkuu huo wa uchaguzi kimetafsiriwa na baadhi ya wajumbe wa mkutano huo, ambao ni viongozi wa vyama vya msingi kuwa ni udhaifu mkubwa ambao unazidi kukiweka chama hicho kwenye wakati mgumu, kwa sababu uongozi uliopo ambao yeye ndiye mwenyekiti na msemaji ni wa muda na mkutano huo ulikuwa kwa ajili ya kuchagua uongozi wa kudumu, kwa mujibu wa sheria ya ushirika. 

Akizungumza mmoja wa wajumbe wa mkutano huo, Salum Brashi ambaye pia ni mwenyekiti wa chama msingi cha ushirika cha Minazini wilayani Namtumbo alisema kimsingi mkutano mkuu wa uchaguzi ulivurugika na kuvunjika kutokana na njama za makusudi za mwenyekiti wa muda, Ally Bango na bodi yake kwa kitendo cha kuwaita wajumbe nane wa mkutano huo na kudaiwa kuwagawia wajumbe hao kiasi cha shilingi elfu arobaini kila mmoja, pamoja na vinywaji ili wamsaidie kushawishi wajumbe wengine wa mkutano huo wamchague kwenye uchaguzi huo, na jambo hilo lilifanyika kwenye hoteli ya Angon Arms mjini Songea.

Aidha alisema kuwa siku iliyofuata ambayo ni Februri 17 mwaka huu, mwenyekiti huyo alipogundua kuwa wajumbe wengine wamegundua jambo hilo la kugawiwa fedha kwa wajumbe wachache aliamua kuwaalika wajumbe wengine na kuwajulisha kuwa yeye ameshatenga fedha kwa ajili ya posho zao, lakini tatizo lipo kwa kaimu meneja wa SONAMCU, Christopher Ugulumo amekataa kutoa fedha hizo ndipo alipoamua kuwashawishi wajumbe, wagomee mkutano huo pamoja na kumkataa meneja huyo.

Aidha Brashi alisema kitendo hicho cha kususia uchaguzi, siyo cha kiungwana ni fedheha na aibu kubwa kwa wanaushirika wote siyo kwa mkoa wa Ruvuma tu, bali kwa nchi nzima ni lazima wanaushirika wakajenga utamaduni wa kuvumiliana na kuaminiana pamoja na kutatua migogoro yao kupitia vikao halali vya ushirika, kwa mujibu wa sheria ya ushirika.

Kwa mujibu wa barua za wajumbe kuitwa kwenye mkutano huo, ilitolewa na uongozi wa SONAMCU baadhi ya wajumbe walisema hapakuwa na sababu ya msingi ya mwenyekiti huyo, kuwaita baadhi ya wajumbe mafichoni kabla ya mkutano na kuwapa msimamo wajumbe kugomea uchaguzi huo usifanyike.

Akizungumza kwa njia ya simu Mwenyekiti, Ally Bango kuhusiana na tuhuma hizo zinazotajwa dhidi yake alisema hayo hayana ukweli wowote bali ni maneno yanayozushwa kwa sababu ya uchaguzi uliopo mbele, ambao na yeye ni miongoni mwa wagombea huku naye Meneja wa SONAMCU alipotafutwa hakuwa tayari kuzungumzia lolote huku akiishia kusema yeye yupo safarini.

No comments: