Bomu lililookotwa wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, kisha
kuteguliwa na JWTZ.
|
Na Steven Augustino,
Tunduru.
JESHI la Polisi wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, kwa
kushirikiana na Jeshi la wananchi JWTZ wametegua na kulipua bomu lenye
ukubwa wa milimita 82 ikiwa ni lengo la kuzuia madhara yanayoweza kutokea
baadae, kama vile usalama wananchi wa kijiji cha Wenje wilayani humo, ambako
bomu hilo lilionekana.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Mihayo Msikhela alisema
kuwa bomu hilo lilionekana karibu na nyumba ya mkulima mmoja, aliyefahamika kwa
jina la Ngaunje Sadick.
Alifafanua kuwa bomu hilo ni la kurushwa na bunduki yenye
uwezo mkubwa, huenda lilitelekezwa katika maeneo hayo miaka ya 1960 wakati wa
harakati za wapigania uhuru wa nchi jirani ya Msumbiji, na kuangukia upande wa
Tanzania ambapo inaonesha halikulipuka kutokana na matatizo ya kutokuwa na nguvu.
Kamanda Msikhela alifafanua kuwa bomu liliteguliwa kwa
kulipuliwa kwa kuunguzwa na moto mkubwa, uliowashwa kwa kutumia kuni nyingi huku
akiongeza kuwa kutokana na kukosa nguvu na kushindwa kulipuka wakati
liliporushwa, lilitoa mwanga mdogo ulioonesha kuwa tayari limekwisha haribika.
Kufuatia hali hiyo Wananchi wa mkoa wa Ruvuma, na maeneo mengine
wameshauriwa pale wanapoona kitu cha ajabu mfano wa bomu, wasikiguse badala
yake watoe taarifa haraka katika vyombo vya ulinzi na usalama, ambavyo vipo
karibu nao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wa kijiji
cha Wenje wilayani Tunduru mkoani humo, ambacho kipo mpakani mwa Tanzania na
nchi jirani ya Msumbiji walikiri kupatwa nahofu ya kuwa katika taharuki kubwa,
baada ya kupata taarifa kuwa mkulima mwenzao kijijini hapo kaleta bomu hilo,
hadi nyumbani kwake akidhani kuwa kaokota kitu cha thamani.
Walisema Kufutia hali hiyo mamia ya wakanachi wa kijiji hicho
wote walikimbia kijijini hapo na kutelekeza watoto, mali na vitu mbalimbali.
Kwamujibu wa taarifa za tukio hilo, zinaeleza kuwa mkulima
huyo aliyefahamika kwa jina la Ngaunje Sadiki aliliokota bomu hilo wakati
akilima shambani kwake katika eneo la mto Ruvuma, na kulazimika kulibeba hadi
nyumbani kwake akiwa na matumaini kuwa kitu hicho kingemsaidia kujikwamua
katika maisha magumu baada ya kukiuza.
Taarifa hizo zilifafanua kuwa Sadiki aliliokota Januari 24 mwaka
huu na kulibeba hadi nyumbani kwake, na kukaa nalo ndani ya nyumba yake kwa
zaidi ya siku 4 hadi alipokutana na mtu aliyefahamika kwa jina moja la Mandiko
kwa madai kuwa ndiye aliyemtegemea kuwa na ujuzi wa kukitambua kitu hicho na
kumkabidhi ili akakiuze Mjini Tunduru, na aweze kupata fedha.
Mashuhuda hao waliendelea kufafanua kuwa wakati Sadiki akiwa
na matumaini hayo Januari 27, alikutana na mtu huyo aliyemlenga kumhusisha katika
uuzaji wa dili hilo ambapo baada ya kuliona tu alihamaki na kumweleza kuwa kitu
alichokuwa amekihifhadhi ndani ya nyumba yake ni bomu, na hatari kwa maisha
yake, familia na majirani zake kijijini hapo.
Kwa mujibu wa mashuhuda hao baada ya maelezo hayo taarifa za
kuwepo kwa bomu hilo, zilianza kusambaa kijijini hapo na kuwafikia watu wengi
hali ambayo ilisababisha wananchi hao kutimua mbio na kuacha nyumba zao
wakihofia kulipukiwa na kupoteza maisha.
Akizungumzia hali hiyo Ngaunje Sadiki pamoja na mambo mengine
alikiri kukibeba kitu hicho na kukihifadhi ndani ya nyumba yake, huku akieleza
kuwa chanzo chake kilijengwa katika matumaini ya kukiuza kitu hicho hata kama
kwa kukipima kama chuma chakavu, lakini angeweza kupata kiasi kidogo cha fedha
ambazo zingemsaidia kujikwamua na hali ngumu ya maisha ambayo imekuwa
ikimkabili kwa kipindi kirefu.
Sadiki alisema kuwa baada ya matumaini yake kuyeyuka na
kuonekana kitu hicho ni hatari hata kwa maisha yake, alipiga konde moyo na
kulazimika kukibeba kwa siri na kwenda kukitupa porini katika eneo la mto
Ruvuma, ikiwa ni matumaini yake ya kuondoa taharuki hiyo aliyonayo yeye na
majirani wenzake kijijini hapo.
No comments:
Post a Comment