Wadau ambao walishiriki katika maadhimisho ya siku ya sheria nchini, wakiwa katika picha ya pamoja kwenye viwanja vya Mahakama ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma. |
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa Mahakama, serikali na wadau wa utoaji haki
ikiwemo mashirika na taasisi zisizo za kiserikali na jamii kwa ujumla, ndio wenye
wajibu na fursa ya kuwezesha jamii, juu ya kujua upatikanaji wa haki zao za
msingi Mahakamani.
Sambamba na hilo, mustakabali wa haki za wananchi unategemea
uwajibikaji na usimamizi mzuri kwa kila mdau wa mahakama, katika kutekeleza majukumu
yake ikiwemo kuzingatia haki na sheria zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.
Aidha mawakili binafsi wamenyoshewa kidole kuacha tabia ya
kutumia vifungu vya kisheria ambavyo, vinapokonya haki ya mtu na kusababisha
mlundikano wa kesi mahakamani, hasa mahabusu gerezani kwa mashauri ya jinai yasiyokuwa
yalazima.
Rai hiyo ilitolewa na Hakimu mkazi mwandamizi, mfawidhi wa
wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Geofrey Mhini katika maadhimisho ya siku ya
sheria nchini yaliyofanyika wilayani humo, yakiwa na maudhui ya; fursa ya
kupata haki ni wajibu wa mahakama, serikali na wadau mbalimbali.
Hakimu huyo alisema mfumo wowote imara duniani, ni lazima uzingatie
haki na mfumo wa sheria ambao unajitosheleza katika kulinda haki za raia wake,
pamoja na utoaji wa haki sawa kwa wakati na ukamilifu, ndio dira ya uwepo wa
sheria na utawala bora.
Mhini alisema, kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977 toleo la ibara ya 13 (1) inasema na kutambua haki, ikiwa
ni pamoja ya kusikilizwa, kukata rufaa na kutochukuliwa kama mkosaji mpaka pale
inapothibitika mbele ya mahakama.
Hivyo mamlaka zinazohusika na utoaji wa haki hasa katika
mashauri ya jinai ni zile ambazo
mtuhumiwa anapatikana na kosa hilo, ikiwemo taratibu za kukamatwa,
kushitakiwa mahakamani, kutiwa hatiani na kupewa adhabu mpaka anapomaliza
kutumikia adhabu yake husika.
Katika hili mamlaka hizi ambazo jamii inazitegemea ni zile
ambazo serikali wakati wote inahitaji kuzingatia haki za binadamu kama vile
jeshi la polisi, magereza pamoja na mkurugenzi wa mashtaka ya jinai (DPP) na
ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali.
Alisema serikali siku zote inahusika katika kuwezesha wadau
wake wa utoaji wa haki kutekeleza majukumu yao ya msingi, ambayo yameanishwa na
sheria za nchi ikiwa ni lengo la kuwawezesha wananchi kupata haki wanazostahili
kwa wakati.
Pamoja na mambo mengine, Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga
ambaye alikuwa mgeni rasmi siku ya maadhimisho hayo ya sheria nchini wilayani humo,
aliitaka jamii kuzingatia taratibu na
sheria zilizowekwa, hususani katika suala zima la maendeleo hasa kupeleka
watoto wao shule.
Ngaga alisema wilaya hiyo, imekuwa ni tatizo kubwa la Wazazi,
kutopeleka watoto wao shule hasa kwa wale ambao waliomaliza darasa la saba,
wanatakiwa kwenda kuanza kidato cha kwanza.
“Nashukuru na kumpongeza Hakimu mkazi, mwandamizi mfawidhi wa
wilaya hii, kwa kutupatia ushirikiano juu ya kupambana na kuhakikisha watoto
wale ambao hawakwenda shule za sekondari kipindi cha mwaka jana, sasa
wamekwenda baada ya kukaa na kukubaliana tuanzishe mfumo wa “Mobile court”, alisema
Ngaga baada ya mfumo huo kuonekana umeleta manufaa kwa kuwabana, wazazi wengi
wilayani Mbinga kupeleka watoto wao shule.
No comments:
Post a Comment